Kibaha. Mchumba wa marehemu, Fortunatus Msofe, ambaye ni mmoja wa wapiganaji wa JWTZ, waliofia Darfur, ameondoka kwenda Tanga kumzika mwenza wake huyo.
Mwanamke huyo Amina Juma, amekataliwa na ndugu wa marehemu ambao wameifunga kwa kufuli nyumba inayodaiwa kuwa amejenga marehemu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Amina alisema ingawa awali alikata tamaa ya kumzika mwenzake, lakini jana aliamua kwenda Tanga kuhudhuria mazishi na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya kujishauri sana.
Baba wa marehemu, Wilbad Msofe Tanga kuwa alishangazwa na hatua ya Amina kutowafahamisha kuhusu msiba huo.
Alisema hiyo ndiyo sababu za yeye kuamua kutaka mwanawe apelekwe Kange kwa mazishi.
Akizungumza na Mwananchi akiwa njiani kwenda Kange, Amina alisema: “Nilikuwa ninataka sana kumzika mwenzangu lakini ile hali ilikuwa imenichanganya pamoja na kwamba nilishauriwa, sasa nimekata shauri nakwenda Tanga.
“Najua kuna kitu hapa, lakini ‘Fortu’ kwa kuwa nilikuwa naye, na wana ndugu wa upande wa wake wameshanikana, mimi nitamzika tu mwenzangu na kurudi,” alisisitiza.
Miili ya wapiganaji hao iliagwa jana katika Makao Makuu ya Jeshi, yaliyoko Upanga na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, makamanda na wanajeshi walishiriki kuwaaga wanajeshi hao.
Akizungumza kwa masikitiko na huku sauti ikiwa imemkauka kutokana na kulia muda mrefu, Amina alisema: “Siwazii mtafaruku uliopo, moyo umenituma kwenda kumzika mume wangu, niliwaza usiku kucha na leo (jana) Jumatatu asubuhi nikaamua kwenda Tanga.”
“Msofe amekufa tulikuwa tuna mipango mingi, tulipanga harusi kubwa lakini haikuwahi kufanyika, niliongea naye alfajiri ya Jumamosi ya Julai 13, akaniambia tutaongea baadaye maana wanakwenda kwenye operesheni...
“Unajua tuliishi maisha ya kipekee sana tulipendana kiukweli hata majirani tuliokuwa tukiishi nao Mbezi na Visiga wanajua hilo na wengi walikuwa wakinisihi sana nisije kumuudhi huyu kijana.
Baadaye akiwa Tanga alisema: “Nafsi yangu inaniuma sana, yaani kila muda na saa zinavyozidi kwenda. Alisema hatua ya wakwe zangu kudai kutonitambua si ya kiungwana.
“Jana (juzi) usiku nikiwa nimejipumzisha nilihisi marehemu ananiambia niyashinde majaribu,” alisema Amina na kuangua kilio.
Akizungumzia kuhusu kufungwa kwa nyumba yao ya Visiga, alisema anamuachia Mungu, kwa sasa yeye haangalii mali na kwamba akili yake ikafikiria msiba uliopo.
chanzo:mwannchi
No comments:
Post a Comment