Monday 19 August 2013

Mke ajifanya kunywa sumu akificha bomu la watoto aliozaa nje ya ndoa!

Naam. Kinababa mpo? Haya, tafakari kwa makini kisa hicho hapo juu na jinsi familia hiyo inavyofanyiana shere(utani) katika maisha.
Mke aliyejaribu kunywa sumu kwa kumtishia nyau mumewe, kumbe naye watoto wawili kati ya wanne wamepatikana nje ya ndoa.
Mumewe naye mke aliyemuoa wala siye yule aliyezaa naye mtoto nje ya ndoa. Kwa ujumla, viongozi wa kaya hii wote wanafanyiana mzaha kila mmoja akionyesha ubabe wa kuwa na mahusiano nje ya ndoa.
Sasa katika hali kama hiyo nani wa kumnyooshea kidole mwenzake? Uaminifu umetoweka ndani ya nyumba nyingi na matokeo yake kila mmoja anafanya vile atakavyo na wala hakuna anayeonyesha kujali. Je, ni familia gani hii?
Baba kama ilivyo sheria za dini yake anaruhusiwa kuoa mwanamke zaidi ya mmoja. Lakini je, huyu bi mkubwa, mume huyu kwanini hafuatilii nyendo zake?
Kama ana mahusiano nje ya ndoa na ana wanaume tofauti kama ambavyo watoto wanaonyesha sura tofauti, linapokuja suala la maambukizi ya virusi vya ukimwi nani atamkamatisha mwenzake?

Huu utandawazi hadi kwenye familia zetu, nani alaumiwe? Binafsi nadhani wajibu ndani ya familia zetu umekosa mwelekeo. Maadili katika usimamizi wa familia zetu yametoweka kabisa. Watu wanaishi ili mradi kumekucha na kila mtu anashika lake bila kutathmini athari zake kimaisha.
Watu wanapeana uhuru wa kufanya mambo bila kuzingatia miiko, miongozo ikiwamo ya kidini na matokeo yake maisha yanaparaganyika pasipo mwelekeo sahihi wenye tija na maslahi kwa familia husika.
Kwa mfano, mwanamke mwenye mume ndani, anapatiwa huduma zote, inakuwaje anatafuta mahusiano nje ya ndoa hata kuzaa mtoto/watoto wa nje? Kama ni wivu ambapo mumewe naye anatoka nje, hakuna njia ya kuweka kikao kupatia ufumbuzi badala ya kufanyiana mashindano eti ukifanya hivi nami nitafanya vile?
Mbona mashindano ya aina hii yameleta mauti kwa wengi? Hivi ni vita ambavyo havina mshindi kwani mwisho wa siku wote mtakuwa majeruhi. Au siyo msomaji wangu? Na kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.
Familia ikifikia hatua kama hiyo tuliyojadili hapo juu, ujue jahazi linakwenda mrama, mawasiliano ni sifuri na kinachokaribishwa hapo ni majanga tu. Si ndiyo msomaji wangu? Wiki ijayo baada ya kusikia maoni yenu kuhusu mada ya leo, nitawaletea kituko kipya eti mke anamlazimisha mumewe aache kazi wakodoleane mimacho, kisa wivu mjinga.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment