Wakati Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda, akiwa anaendelea na matibabu katika Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi), Jeshi la Polisi limemfungulia mashtaka ya uchochezi.
Ponda alisomewa mashitaka hayo akiwa kitandani Moi jana alasiri.
Wakati mashitaka hayo yakisomwa Jeshi la Polisi lilikuwa limeimarisha ulinzi kwa kumwaga askari wengi wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa kwenye magari matano.
Magari hayo ni Land Rover Defender tatu na Toyota Land Cruiser yakiwa yameegeshwa nje ya hispitali hiyo.
Aidha, lilikuwapo kundi la askari kanzu wakiwamo waliokuwa wamekaa mapokezi, wengine sehemu ya kusubiria wagonjwa kuingia kwa madaktari na wengine waliweka kambi nje ya chumba alicholazwa Sheikh Ponda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Marieta Minagi, alikuwapo muda wote huku akizunguka kutoka sehemu moja kwenda nyingine akiwa amefuatana na maofisa wengine waandamizi wa polisi.
Wakati polisi wakimfungulia mashitaka Sheikh Ponda wodini hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuingia wakiwamo waandishi wa habari na wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Taarifa za Sheikh Ponda kufunguliwa mashtaka zilitolewa na wakili wake, Juma Nassoro, ambaye alisema kesi hiyo itakuwa chini ya Hakimu Hellen Riwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu.
Nassoro akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kwa mashitaka hayo, alisema Sheikh Ponda alisomewa shitaka hilo la kuhamasisha watu kufanya makosa akiwa kitandani Moi ambako anaendelea na matibabu baada ya kudaiwa kujeruhiwa kwa risasi mkoani Morogoro Jumamosi iliyopita.
Alisema anashangaa mteja wake kufunguliwa mashtaka wakati jana ilikuwa siku ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo.
“Polisi walipanga jana kumuhoji kwa kufanya vurugu Zanzibar na Morogoro na waliopangwa kumhoji ilikuwa watoke makao makuu ya Jeshi la Polisi na wengine Kituo Kikuu cha Polisi,” alisema Nassoro.
Aliongeza kuwa kutokana na kupewa taarifa za kuhojiwa Sheikh Ponda, yeye (Nassoro) na wakili mwenzake walifika mapema Moi saa 8:00 mchana na kusubiri Polisi kwa muda mrefu bila kufika na walipotoka kidogo na kurejea wakakuta ameshasomewa mashtaka.
Wakili huyo alisema baada ya kupitia mashtaka hayo, wanapinga kwa sababu tayari walishawasilisha malalamiko yao kwenye Tume ya Haki za Binadamu kupinga timu iliyounda na Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la Ponda kupigwa risasi kwa kuwa polisi ni watuhumiwa wa kwanza.
“Tulijiandaa kuzuia mahojiano kati ya Sheikh Ponda na timu kwa sababu hali yake bado siyo nzuri, alikuwa analalamika maumivu ya kidonda na kichwa,” alisema.
Alisema baada ya kupitia hati ya mashtaka, wamebaini ina makosa ambayo watayapinga Agosti 28, mwaka huu ambayo ni siku ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Nassoro alisema makosa yaliyopo katika hati hiyo kwamba Sheikh Ponda alifanya makosa sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Juni 6 na Agosti 11, mwaka huu siyo ya kweli kwa sababu Agosti 11 ni siku aliyoalazwa hospitali.
Kosa la pili ambalo lipo katika hati ya mashtaka ni kwamba Sheikh Ponda alifanya makosa sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar na kuhoji kwa nini kesi hiyo isimamiwe na Hakimu wa Mahakama wa Kisutu.
Nasorro alisema kuwa upande wa mshtakiwa ulipinga uamuzi uliotolewa na Polisi kuwa mshtakiwa atabaki kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi hilo kwa kuondolewa hospitali kwa kuwa hali yake siyo nzuri na hivyo ikaamuliwa abaki chini ya uangalizi wa hospitali.
Katika hatua nyingine, nusura kutokea vurugu hospitalini hapo baada ya askari kuwazuia wananchi waliokwenda kumuona Sheikh Ponda wakati wa muda wa kuona wagonjwa saa 10:00 jioni baada polisi kuwaeleza kuwa wasubiri kwanza kwa kuwa kulikuwa na taratibu za kiserikali zikiendelea.
Uamuzi huo ulipingwa vikali na wananchi ambao walihoji kwanini jambo hilo linafanyika muda wa kuona wagonjwa na lisifanyike kabla.
Sheikh Ponda alijeruhiwa Jumamosi iliyopita akiwa mkoani Morogoro baada ya kuhutubia mhadhara wa Sikukuu ya Idd El Fitri ulioandaliwa na wanazuoni wa dini ya Kiislamu mkoani humo.
Inadaiwa kuwa wafuasi wake walimpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, lakini baadaye walimhamishia katika hospitali ambayo haikufahamika.
Kesho yake alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya kuhamishiwa Moi.
Wafuasi wake wanadai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na kumjeruhi sehemu ya bega.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi linakanusha na Moi inasema haijabaini kilichosababisha jeraha lake kwa kuwa alipokelewa kutokea hospitali nyingine ambayo ilishamfanyia upasuaji na kumshona.
Hii si mara ya kwanza Sheikh Ponda kujeruhiwa kwa risasi kwani miaka ya tisini alikuwa miongoni mwa watu waliojeruhiwa kwa risasi wakisafiri kwa boti katika ziwa Tanganyika.
Ponda alibainika kujeruhiwa baada ya polisi kwenda kuwapeleka majeruhi hao hospitali ya Maweni Kigoma, wakati huo sheikh huyo alikuwa anasakwa na serikali kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uraia ambazo hata hivyo zilitupwa bila kufikishwa mahakamani.
Ponda amekuwa kwenye msukosuko na serikali kuanzia mwaka jana alipokamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kuhamasisha watu kufanya jinai na kuingia kwenye mali ya watu kinyume cha sheria.
Alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambacho bado hakijamalizika.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment