Monday, 30 September 2013

Dada yake Mbowe na Mume wake wafariki dunia ajalini

Dada wa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja na mume wake wamefariki dunia huku watu wengine watatu kukijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupasuka tairi na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Costatine Massawe, alisema kupitia kwa Mkuu wa Upelelezi mkoa huo (RCO), Aziz Kimata, kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 1:30 asubuhi  eneo la Kabuku Wilaya ya Handeni barabara kuu ya Tanga-Chalinze.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Grace Aikaeli Mbowe (Dada yake na Mbowe)  na mumewe, Ibrahim Lukindo (52).

Kimata alisema majeruhi wa ajali hiyo ni Ridhiwani Bakari (29) aliyekuwa na mkewe Zeddy Nzuke (29) raia wa Kenya pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili na miezi minne, Mariam Ridhiwan ambao wamelazwa katika Hospitali ya Magunga wilayani Korogwe.

Alisema walipata ajali hiyo wakati wakitoka jijini Tanga na ghafla gari namba T 277 CAJ aina ya Crestawaliyokuwa wakisafiria ilipasuka tairi la mbele na kupinduka.

Aliongeza kuwa baada ya kupasuka tairi, gari hilo liliingia chini ya daraja na kusababisha vifo na majeruhi.

Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Magunga, Nayela Missingo, alisema alipokea majeruhi watatu na kwamba jitihada za kuwahamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinafanyika kwa kuwa hali zao siyo nzuri.

Missingo alisema mtoto Mariam ndiye amejeruhiwa sana katika kichwa na kwamba tangu alipofikishwa hospitaini, hakuwa katika hali nzuri.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment