Friday, 6 September 2013

Diamond awe mfano wa kuigwa katika jamii

ASALAAM ALAIKUM 
Ama baada ya salaam, sina shaka kila mmoja wetu atakumbuka furaha, mshangao uliowakuta watu wengi ikiwemo familia ya aliyekuwa muimbaji nguli wa muziki wa dansi Maalim Gurumo (73), pindi alipopewa zawadi ya gari na Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’.
Ilikuwa Alhamisi iliyopita katika ukumbi wa Serena jijini Dar es Salaam ambapo kulikuwa na hafla ya uzinduzi wa wimbo wa video wa ‘My Number One’ wa Diamond aliourekodi nchini Afrika Kusini.
Katika hafla hiyo Diamond aliitumia kumpa zawadi ya gari Gurumo ambaye siyo peke yake tu aliyeishiwa maneno bali na wadau kadhaa waliofurika walishikwa na butwaa.
Binafsi namfahamu Diamond na familia yake hivyo katika hili naweza kusema kwamba msanii huyu ameitafuta pepo na Inshaallah mungu atampa na kumfanyia wepesi katika kila jambo la kheri analoliomba katika maisha yake na hasa ikizingatiwa bado anatafuta.
Katika hili Diamond ametoa bila kuangalia mjomba wala shangazi yake ana nini pale kwa Gurumo ametoa hata Mungu na walimwengu wote tumemshuhudia.
Hivyo basi katika hili Diamond awe mfano kwa wasanii wengine pia na kwa watu na taasisi binafsi ziwe zina utaratibu wa kuthamini kazi za watu.

Nasema hivyo kwa sababu ziko taasisi nyingi ambazo hutumia watu, wasanii na hata wanahabari kwa manufaa yao na pindi wakishapata wanageuka wanakuwa hawakumbuki tena ikhsani na kazi walizofanyiwa.
Lakini pia tunapaswa kujiuliza hivi Diamond analipa fadhila gani kwa Gurumo jibu ni hapana, kwa nini nasema hivi ni kwa sababu hawakuwahi kuonana zaidi ya siku ile ndipo ilipokuwa mara ya kwanza kuonana huku Diamond akiamua kumpa zawadi ile kwa sababu alisoma kwenye vyombo vya habari Gurumo alilia mbele ya waandishi wa habari katika mkutano wake uliofanyika Idara ya Habari MAELEZO, alipotangaza kuacha muziki.
Kuguswa huku kusiishie kwa Diamond kwani tuna imani kubwa kwamba kwa kupitia sanaa hii ya muziki Gurumo alichangia kufanikisha mambo mengi ikiwemo ya chama na serikali tawala.
Hivyo basi tunatarajia kuona kwamba serikali yetu haitaishia kuwapatia nishani tu wasanii waanzishe utaratibu wa kuwapa kifuta jasho jambo ambalo litakuwa lenye manufaa kwa mhusika na familia yake kwa ujumla
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment