Tuesday, 3 September 2013

Msichana akata minyororo ya kukeketwa, kuolewa

“Ni lazima ukeketwe....,” Mama mzazi alikaririwa akimwamuru binti yake, Bahati Mwema,14,(siyo jina halisi), mwanafunzi wa darasa la tano,Shule ya Msingi Nyamikoma mjini Mwanza.

“Sitaki kukeketwa, mimi bado mwanafunzi nataka kusoma,” msichana huyo, alifafanua msimamo wake huo  hivi karibuni jijini Dar es Salaam, akiwa chini ya uangalizi wa polisi Magomeni, baada ya kunusurika kukeketwa, kuozeshwa kwa nguvu na kujisalimisha kituoni hapo.

Bahati alifika kituoni hapo kibahatibahati, baada ya kufanikiwa kumtoroka mumewe mtarajiwa Marwa Mashauri, 29,  aliyemsafirisha toka kwao hadi jijini Dar es Salaam baada ya kulipa mahari ya ng’ombe.

Akisimulia mkasa mzima wa maisha yake, anasema, alianza  kusumbuliwa wa wazazi wake kwamba lazima akeketwe akiwa darasa la tatu katika shule ya msingi Nyamikoma mjini Mwanza.


Mkakati uliokuwa ukitekelezwa kwa mujibu wa  msichana huyo ni  kusimamishwa shule mara kwa mara na kupelekwa kijijini Musoma ili akeketwe na baadaye aozeshwe mume.

“Nilipopelekwa na kufika kijijini Musoma; kitu cha kwanza kuambiwa na mama yangu mzazi kilikuwa ni kukeketwa.. nilikataa kata kata,” anasimulia. 

Hata hivyo, anasema mara baada ya kupewa taarifa hiyo na kutoa msimamo wake, mama yake mzazi  alikuwa akipenda kunywa pombe,na kuondoka baada ya muda kwenda kilabuni.
Bahati anasema bahati nzuri  alikuwa na akiba ya sh.5,000 na kuamua kutumia mwanya huo kutoroka na  kurudi Mwanza kwa mama yake mdogo.

Alipofika Mwanza anasema, alimfahamisha  mama yake mdogo kisa cha kutoroka kijijini Musoma, lakini badala ya kumpa hifadhi na kumuunga mkono msimamo wake, akapigilia msumari wa moto kwamba lazima akakeketwe kwa sababu hata wao walikeketwa, na kwamba  kama hataki  ni vyema aondoke na asilale nyumbani hapo.

Katika kuhakikisha azma yake inafanikiwa ya kukataa kukeketwa,Bahati alipoona hivyo akaamua kukimbilia kwa rafiki wa mama yake mzazi anayeishi jirani na mama mdogo jijini Mwanza.

Mama huyo naye, kumbe alikuwa na msimamo unaofanana na wa mama zake akaamua kuvujisha siri kijijini Musoma kwamba yuko hapo kwake.

Taarifa hizo,anasema zikamshawishi mama yake mzazi kusafiri toka Musoma hadi  Mwanza kwa lengo la kuhakikisha kuwa azma ya  binti yake kukeketwa inatimia.

“Mama alipokuja Mwanza, nilikataa kuonana naye kwa sababu nilijua fika kwamba angelazimisha wanikamate kwa nguvu na kunipeleka Musoma ili nikeketwe,” anasema. 

“Nilikimbia na kujificha  ili mama asinione hadi alipoondoka kurudi Musoma,” anasema Bahati huku machozi yakiporomoka.

Baada ya hapo, aliendelea na shule lakini kwa taabu huku akifahamishwa kuwa,  ni lazima afanyiwe mila hiyo. Alipofika darasa la tano akiwa na mama yake mdogo mjini Mwanza anasema migogoro ya kukeketwa ilianza tena.

“Waliendelea kunitaka niende kijijini nikawa nagoma...hatimaye nikaamua kwenda.Kabla sijafika hata ndani ya nyumba walinikamata na kuninyang’anya  mfuko wangu wa nguo....”   anasema na kuendelea
Mama akasema “Sasa ni safari.Unaenda kuolewa si ulikataa kukeketwa?” anasimulia kwa uchungu akiwa Magomeni Polisi jijini Dar es Salaam. 

Mwanafunzi huyo anasema, alishtuka sana kusikia taarifa hiyo  mpya kwamba anakwenda kuolewa wakati bado ni mwanafunzi aliyeenda Musoma kwa lengo la  kuwasalimia  wazazi tu kisha arudi Mwanza kuendelea na masomo. “Mama mbona unataka kuniozesha wakati nikiwa bado mdogo? “aliuliza.
 
“Kabla sijamaliza kusema na kujibiwa baba, mama na mwanamume mmoja wakanivamia,kunikamata na kunipandisha kwenye gari kwa nguvu. Baba akamwambia yule mwanamume Huu hapa mzigo wako! Ushike vizuri uende nao hadi ufike nao huko, usimwachie...!” alifafanua.

Wazazi wa Bahati Mwema walisema wakati wakimkabidhi Marwa Mashauri,29, kijijini Musoma hivi karibuni.

Walisafiri kwa  basi kutoka Musoma hadi Mwanza na kufikia kwa ndugu wa Mashauri na kulala huko. Msichana Bahati hakulala na mwanaume huyo, alilala chumba kingine hadi siku inayofuata. 

“Kesho yake tulipandishwa basi jingine. Nilikuwa sijui napelekwa wapi?,” anasema.

Baada ya kuondoka Mwanza na kusafiri kwa saa nyingi baadaye,Bahati akaanza kulalamika njaa.Mashauri akamjibu kuwa bado hawajafika na kumtaka aendelee kuvumilia hadi wafike ndipo atamnunulia chakula.

Wakiwa safarini, Bahati alimuomba mwananume huyo aitwaye Mashauri namba yake ya simu na kumpatia.

Hatimaye, wakajikuta wamefika jijini  Dar es Salaam wakashuka na kupanda basi jingine kwenda kusikojulikana. Bahati aliendelea kulalamika njaa inamuuma  kwa sababu alikuwa hajala chakula chochote tangu msafara ulipoanza.

Baadaye kidogo walishuka sehemu asiyoijua na Mashauri akamwambia Bahati kwamba amsubiri hapo ili akamnunulie chips za kula.

Msichana huyo alikuwa na akiba ya  sh. 200 tu mfukoni. Alipoona mwanamume huyo kaenda   kununua chips alipotazama vyema akakiona kituo cha polisi na kuamua kukimbilia kituo hapo na kujieleza mkasa 
mzima unaomkabili kisha akawapa namba ya simu ya Mashauri.

Polisi walimpokea na kumpa hifadhi ili kuyaokoa maisha yake na kuamua kuwasiliana na Mashauri kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi za sheria.

“Nilikuwa naogopa kukeketwa kwa sababu hata dada yangu mkubwa alikeketwa kwa nguvu na kuolewa.

Baadaye mume wake alimtelekeza akiwa mjamzito,” alifafanua akikumbukia mkasa huo. 

“Nawashauri wanaolazimishwa kukeketwa wasikubali wakimbilie polisi. 

Wasikubali kukeketwa wala kuozeshwa kwa nguvu; wasome..!” anawashauri wasichana wengine.

Bahati anapata hifadhi baada ya kukabidhiwa Idara ya Ustawi wa Jamii  inayomtafutia shule  ili aendelee na masomo  huku Mashauri akitakiwa kuwapeleka kwa  wazazi  wake na  kufahamishwa kuwa yupo chini ya uangalizi maalum.

Wakati Bahati anakimbia kukeketwa na kuozeshwa, Mashauri baada ya kufika kituo cha polisi na kuambiwa  mkasa huo alidai kulalamika na kushangaa hatua ya Bahati kumtoroka kinyume  na makubaliano yao tangu wakiwa Musoma kwamba waoane.

“Nilikutana naye njiani tukazungumza na kukubaliana kisha akanipeleka kwa wazazi wake.Nao walipozungumza naye akakubali. Wazazi walitaka niwalipe mahari ng’ombe kumi.

Tayari  nimelipa watano na bado nadaiwa  waliobaki,” alisema  Mashauri katika kituo cha polisi Magomeni.
 
Mashauri ni mkazi wa Tabata, Dar es Salaam. Anadai kuwa baada ya kumpata mchumba huyo, walisafiri toka kijijini na kwenda  Dar es Salaam. 

Walipofika eneo la Manzese walishuka ili wakapande basi la kupitia Mburahati kisha liwapeleke Tabata Dampo anakoishi. Hapo ndipo Bahati akapata mwanya wa kutoroka na kukimbilia polisi.
“Bahati akanitoroka na kunikimbia. 

Nikaangaza macho nimtafute sikumuona kabisa na kuamua kupanda gari kisha nikaenda nyumbani peke yangu.

Baada ya kufika  sikupata usingizi, nikafikiria kuwa jijini Dar es Salaam msichana huyo ni  mgeni kabisa nitampata wapi mtoto wa watu?,” Akajiuliza  sana bila ya kupata ufumbuzi.

Baadaye anasema, alilazimika kwenda kituo cha polisi Tabata usiku huo kutoa taarifa na  polisi wakamshauri aendelee kumtafuta hadi zitimie saa 24 ndipo hatua zaifdi zichukuliwe. Aliendelea bila mafanikio.

Mashauri anasema, baadaye alipigiwa simu kuwa anahitajika afike kituo cha polisi Magomeni akaonane na mgeni wake anayemtafuta. 

“Yeye anasema amelazimishwa wakati ukweli ni kwamba  niliongea naye akakubali na kunifahamisha kuwa amemaliza shule. Sasa kwa nini huku amebadilika?. Nilipofika kituoni niliwekwa chini ya ulinzi na kulala mahabusu hadi maarafiki zangu wakaja na kuniwekea dhamana” alisema.

Mradi wa kujenga na kuimarisha usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (GEWE II) umesaidia kuelimisha jamii hasa wasichana nchini wamepata uelewa wa kupata ujasiri wa kukataa mila kandamizi hata kuvikimbia vitendo vya kikatili wanavyolazimishwa na wazazi wao. 
 
Mradi huo, unaongozwa na Chama cha Wanahabari Wanawake  Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na mashirika mengine manne yanayotetea haki za binadamu hasa wanawake na watoto yakiwemo Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Jumuiya ya Wanawake Wanasheria Zanzibar (ZAFELA), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Kituo cha Usuluhishi ( CRC).

Mashauri anakiri kuwa licha ya kwamba hatomuoa tena Bahati, lakini mahari yake ya ng’ombe aliyotoa kwa ajili ya binti huyo atadai arudishwe kwa sababu ni haki yake.

Alipoulizwa kwa nini wanapenda kutoa ng’ombe kama mahari badala ya vitu vingine, Mashauri alijibu kuwa “Huyu ni mtu, unatakiwa utoe ng’ombe mwenye damu kama binti uliyemchukua. Huwezi  kutoa thamani ya kitu kingine kama fedha”.

Mashauri anasema kuwa  shughuli yake ni kuuza viatu. Ameiomba serikali, taasisi na mashirika yaandae mfumo wa somo maalumu la kuwafundisha watoto kuhusu hali ya maisha kwani nyumbani peke yake haitoshi.

Afande Pendo  wa dawati la jinsia kituo cha polisi Magomeni,Dar es Salaam anasema itolewe elimu ya kutosha huko vijijini ili kuondokana na mila potofu zinazokandamiza wanawake.

“Elimu kule kwetu hakuna kabisa.Watu hawaelewi mila hizi kama ni mbaya. Elimu hii ipelekwe kwetu vijijini ili kuondokana na hali hii kwa sababu watu wakielimishwa wataelewa,” alisema.
 
Sista Gernabe Baibika mkuu na mlezi wa kituo cha Ushirika wa Kutokomeza ukeketaji (UKU) ambacho anasema  kuwa watoto wa kike 160 walikimbilia kituo cha polisi mwaka 2009 mkoani Mara. 

Mwaka 2010 walikuwa 180, mwaka 2011 walikimbia wasichana 207 na mwaka jana 2012 waliokimbilia polisi ni 350.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment