Friday, 6 September 2013

Mtoto aibiwa katika mazingira yakutatanisha na mwanamke anayedaiwa kuwa JINI Dar,

                                                    Mtoto aliyeibiwa, Rahma Ally.
                                      Mama wa mtoto aliyeibiwa, Shamsa Amiri (27).
                                                     Mwanamke aliyeiba mtoto alivaa hivi.

HATARI imeingia jijini Dar baada ya Shamsa Amiri (27) mkazi wa Buguruni Ghana, kuangua kilio baada ya hivi karibuni kuibiwa mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili katika mazingira ya kutatanisha na mwanamke anayedaiwa kuwa ni jini.
KWA mujibu wa Shamsa, siku ya tukio ambayo ni takriban mwezi umepita alimchukua mwanaye aitwaye Rahma Ally na kwenda naye kliniki katika zahanati moja iitwayo Plan International iliyopo Buguruni kwa Mnyamani.
Shamsa amesema kuwa alipokuwa akitoka kliniki alimuona mwanamke aliyekuwa amevaa kininja ambaye alimchangamkia huku akimfuata na kumsemesha kwa bashasha. 
“Tukiwa njiani mtoto wangu alianza kulia, mwanamke yule akaniuliza kinachomliza, nikamjibu kwamba labda amejisaidia,” alisema na kudai kwamba mwanamke huyo alimshauri waende dukani ili akapate nafasi ya kumbadili.

Shamsa alisema pamoja na kumwambia mwanamke huyo kwamba hakuwa na uwezo wa kununua kitu chochote dukani ili kupata nafasi ya kumsafisha mtoto, mwanamke huyo alimhakikishia kwamba angemsaidia kumnunulia soda ili waweze kupata nafasi ya kumsafisha mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo aliendelea kusema kwamba akiwa anakunywa soda, ghafla alibanwa na haja ndogo, akamwachia mtoto wake mwanamke huyo ili akajisaidie.
“Nikiwa msalani mwanamke yule, alinifuata na kuniambia kwamba niwahi kutoka kwa kuwa mwanangu alikuwa akilia sana,” alisema Shamsa.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka, mwanamke yule alimsisitiza Shamsa amalizie soda yake kisha waongozane kwa kuwa mwelekeo wao ulikuwa ni mmoja.

Shamsa alisema walipitia Buguruni sokoni na alipokuwa ameinama ili anunue kitu, alipogeuka ghafla hakuona mtu na alipouliza watu walidai kuwa mbona alifika pale peke yake.
“Wakati nainama nilikuwa namsemesha lakini nikashangaa kimya, ile nanyanyuka nakuta hamna mtu, kwa mshtuko nilianguka chini na kupoteza fahamu,” alisema Shamsa.
Mama wa mtoto huyo alisema kuwa alipozinduka alijikuta Polisi Buguruni akiwa hakumbuki chochote. Alipokaa kwa muda mrefu ndipo picha nzima ikamrudia na kusema kuwa mwanamke yule hakuwa mtu wa kawaida.
Baada ya kuhadithia kilichotokea, Shamsa alifungua hati ya mashtaka namba BUG/RB/10574/2013.
Hata hivyo, mmoja wa watu waliokuwa kituoni hapo alisema katika siku za hivi karibuni amekuwa akionekana mwanamke mwenye vazi hilo la kininja maeneo ya Buguruni na kwamba wengi wamekuwa wakihisi si mtu wa kawaida yaani jini.
Kwa yeyote atakayemuona mtoto huyo ambaye picha yake iko ukurasa wa mbele, atoe taarifa kupitia simu namba 0656 757690 au 0652 455 809.

CHANZO:globalpublishers

No comments:

Post a Comment