Friday, 13 September 2013

Shilole kikaangoni kwa kuanika maungo Fiesta

SHIRIKISHO la Muziki Tanzania, limetakiwa kumchukulia hatua za kinidhamu, msanii wa muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ kutokana na vitendo vyake vya kukiuka maadili ya Kitanzania wakati wa tamasha la Serengeti Fiesta, mkoani Iringa, hivi karibuni.
Shilole, anadaiwa alipanda jukwaani akicheza wimbo wake wa ‘Nakomaa na Jiji’ huku akiwa amevaa nguo ambazo zinaonesha maumbile yake yote ya mwili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, Kimela Billa, alisema Shirikisho la Muziki chini ya rais wake, Addo Novemba, wanatakiwa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Shilole kwa kosa la kuwadhalilisha wanawake, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ya Kitanzania.
“Hatukatai hayo mambo yapo, lakini kwa staili ile sisi kama viongozi wa sanaa hatutaweza kuvumilia, shirikisho la muziki wakishindwa kutekeleza hili, lazima kamati ilivalie njuga suala hilo, kiukweli wanalidhalilisha taifa hawa wasanii, mbona wanaume hawafanyi shoo zao uchi?” alihoji Billa.
Alisema Shirikisho la Muziki liige mfano wa lile la filamu, kama lilivyowaonya Wema Sepetu na Aunt Ezekiel kwa makosa kama hayo, ambapo anaamini kwa asilimia kubwa kunachangia kuwa na nidhamu wanapopanda jukwaani.
“Angekuwa ameenda kwa shughuli za filamu wangelifanya wao, lakini hili Shirikisho la Muziki wanatakiwa wakae meza moja na Shilole kulizungumzia hilo, wao wanakuwa wazito kuwachukulia hatua wasanii wa muziki kuliko filamu, lakini kwa hili haitawezekana,” alisema.

No comments:

Post a Comment