Monday 2 September 2013

Tamwa kuwavalia njuga ‘mashugamami’

Dar es Salaam. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimesema kitapaza sauti kama kutakuwa na  madai ya wanawake wenye umri mkubwa kutembea na watoto wadogo.
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa Tamwa, Valeri Msoka alipokuwa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam.
“Tunasikia kuna kesi hizi za wanawake wenye umri mkubwa kuishi na watoto wa umri mdogo, huu ni unyanyasaji wa kijinsia, lakini ukweli hatujapata malalamiko hayo na kama yakiwepo, tutayashughulikia,” alisema Msoka.
Msoka mmoja wa wanahabari wakongwe aliwataka waandishi wa habari kupaza sauti kwenye masuala ya unyanyasaji wa kijinsia maeneo mbalimbali kwani tatizo ni kubwa.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake, Tawla, Tike Mwambikile alitaka Katiba Mpya isiyaweke kando masuala ya unyanyasaji wa jinsia kwani ni tatizo kubwa hasa maeneo ya vijijini.
Mwambikile pia alihimiza kuhusu mirathi kwamba kuna haja ya kuingizwa kwenye katiba ijayo.
Akichangia katika mkutano huo, Mary Msemwa kutoka Mtandao wa Jinsia, (TGNP), alisema asilimia 44 ya wanawake walioolewa wananyanyaswa, kubakwa na wakati mwingine kuuawa.
Alisema huo ni ukatili mkubwa dhidi ya watu wa kundi hilo na kwamba kuna haja kwa jamii kuchukua hatua za kuzuia hali hiyo.
Inasemekana kuwa vitendo vya unyanyasaji wa wanawake na watoto vinazidi kukithiri licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali na mashirika yasiyokuwa na Serikali  katika kujaribu kuvikomesha kabisa.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment