Thursday, 12 September 2013

Ushuru Dola 500 watesa madereva Rusumo

Rwanda jana ilianza rasmi kutoza ushuru mpya wa barabara wa Dola za Marekani 500 kwa malori kutokaTanzania, hali iliyosababisha athari kubwa kwa madereva waliokuwa wakisafirisha mizigo kuelekea nchini humo kukwama katika mpaka wa Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera, baada ya kushindwa kulipia.

Kuanzia jana, serikali ya Rwanda ilipandisha kiwango cha ushuru wa barabara kutoka Dola za Marekani 152 hadi Dola 500 ongezeko la asilimia 229, hatua ambayo imekwamisha madereva wa malori ya mizigo kutoka Tanzania kukwama kuendelea na safari kutokana na kutokuwa na fedha za kulipia.

Wakizungumza na NIPASHE wakiwa mpakani Rusumo jana, baadhi ya madereva hao walisema kwamba wamelazimika kutoendelea na safari hadi pale wamiliki wa magari watakapokuwa wamewatumia fedha kwa ajili ya kulipia kiwango hicho kipya cha ushuru.

Dereva wa Kampuni ya Yahaya Topstory ya jijini Dar es Salaam, Said Salum, alisema alifika mpakani Rusumo tangu Jumapili, lakini hakufanikiwa kulipia ushuru kwa kiwango cha zamani kutokana na msururu mrefu wa malori ambayo pia madereva wake walikuwa wakiwania kulipia mapema.

“Mimi nimefika hapa tangu juzi, lakini sikuweza kuwahi kulipia kutokana na msururu mrefu wa magari, leo (jana) ndiyo nimepata nafasi ya kwenda kulipia, lakini nimekuta tayari ushuru umepanda hadi Dola 500, hivyo nimeshindwa na ndiyo sababu unaniona bado niko hapa,” alisema.

Aliongeza kwamba tayari amewasiliana na mwajiri wake amtumie fedha za ziada ili alipie na kuendelea na safari ya kupekea mzigo jijini Kigali, Rwanda.

Isaya Mmbando wa kampuni ya Barwaaqo Investment Ltd pia ya Jijini Dar es Salaam, alisema amekwama kuendelea na safari kutokana na kukosa Dola 500.

“Nimeshawasiliana na tajiri (mwajiri) kumweleza hali halisi iliyopo hapa, naye ameniambia anafanya mawasiliano na mfanyabiashara aliyetukodi kumweleza ongezeko hili, wakishaafikiana ndipo atatuma pesa zaidi ili tulipie na kuendelea na safari,” alisema.

Naye Mohamed Kipande wa kampuni ya Mapelele Transport Co. Ltd, alisema ameshangazwa na ongezeko la ghafla la ushuru wa barabara, lakini aliongeza watakaoathirika zaidi ni wananchi wa Rwanda ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa bidhaa wanazosafirisha.

“Kama serikali ya Rwanda imeamua kuongeza ushuru wa barabara ni wazi gharama za usafirishaji pia zitaongezeka na hii itaathiri wananchi wa Rwanda kwa sababu wafanyabiashara nao wataongeza bei ya bidhaa,” alisema.  

Edward Leonard wa kampuni ya Victoria Moulders ya jijini Mwanza, alisema huenda lengo la serikali ya Rwanda kuongeza ushuru kwa magari ya Tanzania pekee yanayopitia mpaka wa Rusumo ni kutaka kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi hiyo kutumia bandari ya Mombasa na kuachana na bandari ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, alisema iwapo sababu ndiyo hiyo bado wafanyabiashara wa Rwanda watapata taabu kuingiza mizigo yao kupitia Mombasa kwa sababu kuna umbali mrefu hadi kufika Kigali na pia watalazimika kuvuka mipaka miwili ya Kenya na Uganga kabla ya kuingia nchini kwao.

Kaimu Ofisa wa Forodha wa Tanzania katika mpaka wa Rusumo, Sure Mohamed, alithibitisha ushuru wa barabara kwa upande wa Rwanda kupanda kuanzia jana baada ya tangazo ambalo hata hivyo baadaye waliliondoa kwa sababu zisizojulikana.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu, alisema kwamba hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa maofisa wa Forodha waliopo mpakani Rusumo, lakini alisema anafuatilia ili kujua nini kinaendelea.

“Kwa siku nzima leo (jana) nilikuwa kwenye kikao wilayani Karagwe, sijapokea taarifa zozote kutoka kwa maofisa wa Forodha, lakini nitafuatilia ili kama ni kweli wameanza kutoza ushuru mpya kwa Dola 500 nimjulishe mkuu wa mkoa ambaye atawasiliana na waziri anayehusika kwa hatua zaidi,” alisema Kanyasu alipozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu.

WAZIRI MGIMWA AZUNGUMZA

Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana jioni, alisema kuwa alikuwa na mazungumzo na Waziri husika wa Rwanda mjini Kampala jana na wameshatatua tatizo hilo. Dk. Mgimwa alisema wameafikiana kuwa kuanzia leo ushuru utakaokuwa unalipwa ni Dola 152 na siyo Dola 500 zilizoanza kutozwa jana.

Aidha, Dk. Mgimwa aliwataka madereva wa malori kutoka Tanzania kuwa na amani kwa kuwa suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi. 

“Nipo Kampala sasa hivi na Waziri wa Uchukuzi wa Rwanda, tulikuwa na mazungumzo kuhusiana na hiyo nyongeza ya ushuru wa barabara, na hivi sasa ndo tumemaliza na tumeafikiana ushuru uwe Dola 152,” alisema Dk. Mgimwa.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alipotafutwa kuelezea hali hiyo hakupatikana kwani simu zake zilikuwa zimefungwa.

Hata hivyo, Naibu wake, Dk. Charles Tizeba, alipotafutwa naye simu zake zilikuwa zinaita bila majibu.
 chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment