UMEKUWA ni kama wimbo wa taifa unaoimbwa kwa ajili ya wasanii wa kike Tanzania, kutokana na kurudiwa kwa maneno hayo hayo kila kunapokucha.
Serikali na baadhi ya mashirikisho husika ya sanaa yamekuwa yakikemea suala la wasanii wa kike kuvaa nguo za nusu uchi katika maonesho yao, lakini kwa asilimia kubwa hakuna linalorekebishwa.
Sitaki kuamini kama msanii anapovaa nguo za aina hiyo ndiyo anaimba vizuri au anacheza vizuri tofauti na akivaa nguo za kumstiri mwili wake.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, Kimela Billa, aliutaka uongozi wa Shirikisho la Muziki Tanzania, umchukulie hatua za kinidhamu msanii wa muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, kwa kosa la kuvaa nguo ambazo hazikustahili kuvaliwa kwenye umati wa watu.
Sijajua kama msanii huyo alichukuliwa hatua zozote au kuonywa, kwa sababu hadi sasa anaendelea kuvaa nguo hizo katika matamasha mbalimbali ya Serengeti Fiesta 2013, ambayo yanaendelea mikoani.
Ilikuwa ni tamasha la mkoani Iringa ambako kiongozi huyo aliona msanii huyo amevuka mipaka, lakini baada ya hapo akazunguka zaidi ya mikoa mitano akiwa anaendelea kuvaa nguo hizo ambazo zinaijengea tafsiri mbaya tamasha la Serengeti Fiesta, ambalo lipo kwa ajili ya kutoa burudani kwa wapenzi wa muziki.
Kwa mtu ambaye anaona mbali na mwenye kujiheshimu, hawezi kwenda kushiriki katika matamasha hayo kutokana na uvaaji wa wasanii wa kike kuwadhalilisha wanawake wote hatawale ambao wanajiheshimu.
Si Shilole peke yake, ni karibu wasanii wote wa kike kama kina Linnah, Recho, Snura na wengine, naomba mbadilike, hata mkivaa nguo zenye maadili ya Kitanzania nyimbo zenu zitasikilizwa, tena mtapata na wadau, ambao kwa sasa wanawashusha thamani kutokana na mnavyojidhalilisha wenyewe kutokana na mavazi yenu.
Kwanini msiige mfano wa msanii mwenzenu, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’? Nafikiri yeye anajikubali na anajua umuhimu alionao katika jamii, ndiyo maana anavaa nguo za kujisitiri na kumfanya aheshimike na kila mtu bila kuchagua rika.
Hata ukiangalia katika shoo zake, watu ambao wanakwenda ni wale wenye kujiheshimu huku wengine wakiongozana na wake zao, kutokana na kumkubali msanii huyo, kuanzia kazi zake mpaka mavazi.
Huwezi kumkuta mtu mzima na akili zake anakwenda kuangalia shoo ya Shilole na wenzake, hata kama ana nyimbo nzuri, ataishia kuzisikiliza redioni tu, hiyo yote ni kutokana na kukera watu na mavazi yao.
Matamasha ya Serengeti Fiesta yamekuwa ni sehemu ya kuonesha maumbile yao jinsi yalivyo na kujipotezea soko kwa mashabiki wao pasipo wao kujua.
Nawashauri wanawake wenzangu, mjitahidi kuvaa nguo za kujisitiri angalau hata kidogo ili muweze kulinda heshima zenu pamoja na vipaji vyenu kwa wadau wenu.
Msanii unatakiwa kuwa kioo cha jamii, unapovaa nguo za aina hiyo unakuwa unaifundisha nini jamii inayokuzunguka? Kwa asilimia kubwa hata wale mabinti ambao wanakuwa wanaiga mifano ya dada zao kwa kuwaona katika nyimbo zao au matamasha mbalimbali.
Hata serikali nayo pia inatakiwa kukemea jambo hili na kuwachukulia hatua wahusika wanaoruhusu hali hii ili wasiharibu kizazi kinachokuja.
Ingekuwa ni mtu wa mtaani anavaa hivyo, ingekuwa haina maana ya kukemea kadhia hii, lakini kwa kuwa msanii ni kioo cha jamii na kila mmoja anamuangalia yeye, anapofanya hivyo anaidhalilisha hata nchi yake, kwa kuwa dunia hivi sasa ni kijiji, hivyo hakuna siri.
Wahusika wa matamasha mbalimbali ya binadamu, hususan Fiesta, mjitafakati na kadhia hii, vinginevyo hata malengo yenu mema yatapotea mbele ya jamii
No comments:
Post a Comment