Monday 7 October 2013

Mke anapomgeuza mume gari la kuzoa majitaka! Utadhani sinema vile, kumbe ni ukweli mtupu.

Huyu ni kaka anayepambana kumnasua mdogo wake wa kiume ambaye amenaswa ulimboni na mwanamama anayemlazimisha kumtolea kinyesi nje badala ya mke huyu kwenda kujisaidia chooni anatumia kisado( ndoo ndogo ambayo hujulikana kama kisado). Ni kituko juu ya kituko. Yaani mume amegeuka gari la kuzoa majitaka? Makubwa, kwani madogo yana unafuu.
Hebu sikia kituko hiki; Ujumbe unaanza hivi;- Kama haya ni maisha hatutoki nisaidie kwani familia tumeshindwa na huyu ndugu yangu wa damu.
Dogo tulimpa ushauri wa maisha ila yeye anaishi hivi:- Huambatana na mkewe popote aendapo, tukajiuliza huyu shemeji anafunika uso katoka Kishumundu au. Tulipouliza tukaambiwa ni Mhehe wa Iringa ambaye alikuja Moshi kama hausigeli.
Basi tukavuta subira tukisema labda ni ugeni. Dogo hatoki nje na anapotoka bibie huwa anabana mlango na kufuli, ah! Tukajiuliza anakwenda msalani(chooni) na huwa anakwenda haja ndogo na kubwa wapi?
Tukaitisha kikao cha familia tukamuuliza dogo, mbona mkeo hatokagi nje? Anaoga wapi, kujisaidia je? Ana tatizo gani na kwanini unamfungia ndani kwa kufuli? Akajibu: Hor! Ni mke wangu, haiwahusu maisha yetu ni ya kizungu!
Yaani kwa jibu hilo tulivunjika mbavu kwa kicheko cha masikitiko. Nikamuuliza; mzungu anamfungiaga mke ndani? Hata mbwa hapendi kufungwa na kwanini? Eti bro tusitafutane. Akaingia ndani nikamwambia mama mwambie shem apike kesho Jumapili maana tupo tutamuona ili tumuulize na yeye.
Dada huwezi amini, ilitokea balaa na vituko. Eti kila mtu apike kimpango wake. Nilikoma nikashirikishababa na mama zetu wakubwa, baba yetu ni marehemu.
Akagoma kikao ikabidi tusubiri matokeo kumbe mke kwenda haja kubwa na ndogo ni ndani, halafu dogo anakwenda kumwaga nje…Heeee! Makubwa! Nilichoka nikamwambia aniachie kazi. Za mwizi ni arobaini ila za mjinga 2.
Huwezi amini mwana anachuma mboga anapika mwenyewe. Nikasema ni limbwata gani hii? Nikakemea wapi. Nikiuliza kimya nikimpiga hapana. Roho inaniuma kwa kuwa tupo wawili tu wa kiume na dada zetu watatu.
Basi nikachukia sana maana dogo mwenyewe anabangaiza kazi ngumu hataki.
Dada nimechoka siku moja sijui nimpe Mungu sifa gani. Ile natoka tu geto kwangu nakutana na dogo kabeba sado nikamwahi, nilipandwa na hasira nikamkamata mkono kucheki kinyesi na mkojo. Nilimmwagia nikawachapa bakora za kutosha wote na vibao juu, na kwangu wakahama. Faida ya kukaa ndani mtoto wa miaka minne hajatembea na akaongeza mwingine.
Kila aendapo dogo huyu hufukuzwa kwa hiyo tabia ya kuzoa kinyesi, kumfungia mke ndani kutooga…ni wachafu ile mbaya wananukia ndafu… Nifanyeje? Si majanga hayo dada Filo eh! Niambie eti inauma jamani si bora tungezaliwa hata wa kiume watano sasa nitashauriana na nani au itokee nikifa nani kiongozi wa familia na dada wote wameolewa? Ni kisa cha kweli. Najiuliza ni limbwata gani hii?  (Kiba Lyimo mjukuu wa mboso).
 Eti dogo kapenda mke, hataki atoke nje na yu radhi kuzoa kinyesi na mkojo wake kumwaga nje pengine chooni kuliko kazi hiyo ifanyike moja kwa moja chooni.
Kama kweli hicho ndicho kinachotokea, siyo bure. Kuna tatizo hapo. Inavyoonekana hawa wawili hawajitambui, wako kwenye mateso ambayo wamefikia mahali wanaona hayo ndiyo maisha au kama nipendavyo kusema mimi kwamba Maisha Ndivyo Yalivyo.
Lakini kwa hili siyo sawa kabisa. Kwanini mwanamama huyu asitoke kwenda kujisaidia nje na badala yake kutumia kisado ambacho pia mume ndiye mwenye kibarua cha kupeleka nje kumwaga na kukisafisha?
Kama alivyosema kaka yake ni kwamba hawa jamaa ni wachafu, wananukia kindafu ndafu. Kule uchagani yupo yule mbuzi dume(beberu) aliyenona mkubwa-ndafu- ambaye kabla ya kuhasiwa anatoa harufu fulani kali. Ni liharufu fulani baya baya, limejaa shombo. Sasa hilo harufu ndilo wanalonuka jamaa hao. Kazi ipo!
Angalia, kila mahali wanapokwenda kupanga chumba, tabia yao ya kufanyia mambo yote ndani imewashinda wenye nyumba na ndiyo maana kaka yake akasema hufukuzwa.
Hebu tuulizane maswali hapa kisha tuyatafutie majibu; je, tatizo hapa ni nini? Je, ni umri kwa maana ya utoto unawasumbua wawili hawa? Au kijana kamzimikia (kampenda bibie kupindukia) ndiyo maana anakubali kuwa mtumwa wa kumzolea majitaka?
Je, au huyu bibie ipo namna amemfanyia kijana huyu kumpumbaza hata kufanya yote hayo? Eti anamjibu kaka yake kuwa kumfungia mkewe ndani ni maisha ya kizungu. Hebu aache hizo kwani wazungu wakimsikia watamvamia kama nyuki. Yaani wazungu na ustaarabu wao wote wanafanyia mambo yao kwenye visado? Du! Mbona jamaa huyu kawadhalilisha kiasi hiki?
Yeye aseme penzi la kijinga limemkolea na siyo eti wanaishi maisha ya kizungu. Uzungu gani wa kunukia kimbuzi mbuzi au kindafu ndafu? Hawa ni wachafu koge na penzi lao wamelipalilia kwenye dimbwi la uchafu. Au siyo msomaji wangu?
Hawa jamaa wako kwenye mateso ambayo hawatambui watokeje huko. Kama siyo nguvu za giza zimewazunguka, basi lipo tatizo la kitabibu ambalo yafaa atafutwe mtaalamu wa saikolojia au mshauri nasaha akae nao awasikilize pengine wanaweza kufunguka. Au siyo msomaji wangu? Mimi niishie hapa ili nikupe fursa nawe utoe kisa ukijuacho cha kimaisha na pia maoni namna ya kuwasaidia jamaa hawa.

No comments:

Post a Comment