Saturday 5 October 2013

MUSWADA WA SHERIA: JK awaita wapinzani mezani

HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amekata mzizi wa fitina kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba unaopigiwa kelele na vyama vya siasa na wadau, akiwataka warudi mezani kujadiliana na serikali.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo jana katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita akisema: “Kama dhamira yetu ni kutaka kupata katiba mpya kwa mujibu wa katiba na sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia.”
Badala yake aliwataka watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba.
“Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika serikali tuko tayari,” alisema.
Katika hotuba hiyo, pia aligusia masuala mbalimbali kama vile operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini, shambulio la kigaidi nchini Kenya na mafanikio ya ziara yake nje ya nchi.
Alisema kuwa hivi sasa tume inaandaa mapendekezo ya rasimu ya pili ya katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalumu.
Kwamba baada ya tafakuri zake, Bunge Maalumu litatoa rasimu ya mwisho ya katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Alisema kuwa baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha sheria ya mabadiliko ya katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na chama tawala.
“Majadiliano yalifanyika baina ya serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu,” alisema.
Kwa mujibu wa rais, awamu ya kwanza ilihusisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalumu na mwisho kura ya maoni.
Alisema kuwa kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.

Kwamba yalifanyika mazungumzo kati yao na serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya muswada na kuuwasilisha kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.
“Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalumu litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga sheria, serikali ilifikisha muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala.
Kama ilivyo ada, kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu muswada. Kwamba aliambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau.
Alisema kisha wajumbe wa kamati walikaa wenyewe kujadili muswada, wakiwepo pia wabunge ambao si wajumbe wa kamati walioshiriki kwa vile kanuni zinaruhusu.
“Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi.  Mapendekezo kadhaa yalitolewa na wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya muswada,” alisema.
Rais aliongeza kuwa alifahamishwa kuwa wabunge wa vyama vyote walichangia, na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa magumu mawazo mazuri ya baadhi ya wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi.
Alisema kuwa aliambiwa pia kwamba wajumbe wa kamati na upande wa serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke bungeni ili wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Kwamba baada ya kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe aliwasilisha muswada bungeni, akifuatiwa na Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya kamati.
Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alitoa maoni yake. Kuwa baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa wabunge wangeanza kujadili muswada.
“Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya wabunge wa upinzani wakitaka muswada usijadiliwe.
“Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili,” alisema.
Rais alisema kitendo hicho kimewanyima wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya msemaji wao, na kwamba walijinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Alisema uwa wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha.
“Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha miswada bungeni.
“Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.  Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa bungeni na si vinginevyo,” alisema.
Alisema kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hiyo.
“Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema.
Aliongeza kuwa kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na kutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.
“Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata katiba mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?” alisema.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani bali katiba ya nchi, katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko wote.
“Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote.  Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa, ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa wajumbe, hivyo wale wachache watakaobahatika lazima wawasemee wote,” alisema. 
Ushirikishwaji wa Z’bar
Katika hilo, rais alisema kuwa alieleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika muswada.
“Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini!  Labda kuna kitu sikuambiwa,” alisema.
Alisema kuwa aliulizia kuhusu hoja ya kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, akaambiwa kuwa kanuni za Bunge hazina sharti hilo, hivyo kamati haistahili kulaumiwa.
“Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulaumiana isivyostahili,” alisema.
Alisema kuwa aliambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais alifafanua kuwa ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia.
Alisema kuwa Bunge Maalumu lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
“Hivyo basi, katika Bunge Maalumu nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata, bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar,” alisema.
Alisema kuwa anadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama wabunge wataamua waongeze idadi, itakuwa kwa sababu nyingine siyo hiyo ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume ya Warioba
“Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani, lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalumu bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato.
“Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
“Kwa hiyo kuilaumu serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii. Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalumu hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya tume,” alisema.
Alihoji kuwa ushiriki huo uwe vipi? Je, ni wajumbe wote au baadhi yao na kusema kuwa hilo ni jambo linaloweza kujadiliwa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment