Tuesday, 8 October 2013

Polisi wadai kukamata `magaidi` 11

Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linadai kuwa limewakamata vijana 11 wakifanya mazoezi ya kigaidi wakiwa na CD 25 za mitandao ya kigaidi ya Al Qaeda na Al Shaabab.

Jeshi hilo linadai kuwa limewakamata vijana hao katika milima mirefu iliyopo msitu wa Makolionga wilaya ya Nanyumbu wakiwa na vifaa mbalimbali vikiwamo vyakula na silaha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema jana kuwa kuwa vijana hao walikamatwa baada polisi kupewa taarifa na kuanza kuwafuatilia huko milimani na kwamba mwishoni mwa mwezi uliopita walifanikiwa kuwatia mbaroni.

Alisema baada ya kuwahoji kwa kina walibaini vijana hao walikuwa wanafanya mazoezi ya hatari ambayo yana uhusiano na makundi ya kigaidi ya Al Qaeda na Al Shaabab. 

Alifafanua kuwa vijana hao walikuwa eneo ambalo watu wa kawaida hawawezi kufika kutokana na msitu mkubwa na milima iliyopo na kwamba walitumia mbinu za kipolisi kuwafikia na kuwakamata bila kuleta madhara yoyote.

“Tulitumia mbinu za kitalaamu na tukafanikiwa kuwakamata wote bila ya kumdhuru hata mmoja na kuwafanyia mahojiano ya kina kabla ya kuwafikisha mahakamani Oktoba 3, mwaka huu a na kusomewa makosa ya ugaidi,” alidai Kamanda Stephen. 

Alisema walisomewa mashitaka hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu.

Aliongeza kuwa watu hao walikuwa kwenye maficho na kwamba walitumia CD zipatazo 25 zenye mafunzo mbali mbali, baadhi zikuhusu Al Shaabab, mauaji ya Osama Bin Laden, Zinduka Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu sniper.

Vitu vingine walivyokutwa navyo ni pamoja na DVD player moja, Solar panel moja (Watts 30), mapanga mawili, visu viwili, tochi moja, betri moja ya pikipiki namba 12, simu tano za viganjani, vyombo mbali mbali vya chakula, jiko moja la mkaa na jiko moja la mafuta ya taa.

Alitaja vitu vingine kuwa ni pamoja na taa moja ya chemli, baiskeli tatu, ndoo nne za maji, vitabu mbali mbali vya dini ya Kiislamu, unga wa mahindi kilo 50, mbaazi kiroba kimoja (kilogramu 50), mahindi viroba vitatu (kilo 150), virago vya kulalia na mfuko wa kijani unaosadikiwa ni wa kijeshi (Kit bag) wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.


Vijana hao ambao kwa sasa majina yao tunayahifadhi, umri wao ni kuanzia miaka 18 hadi 39 na ni wakazi wa mkoa huo. 

Wa kwanza mwenye miaka 39 ni mkazi wa kijiji cha Sengenye (kiongozi wa kundi hilo); wa pili (39), mkazi  wa Nalunyu; wa tatu ( 27), mkazi wa Likokona na wa nne (32) ni  mkazi wa Likokona.
 
Wa tano (38), mkazi wa Likokona; wa sita (26), mkazi wa Likokona, wa saba (20), mkazi wa Likokona; wa nane (32), mkazi wa Likokona; wa tisa  (18), mkazi wa Likokona wa kumi (21), mkazi wa Likokona na wa 11 (21), mkazi wa Likokona.

Kamanda Stephen alisema wanaendelea na upelelezi wa kina kuhusu tukio hilo ambalo alisema siyo la kawaida kwa kushirikiana na Makao Makuu ya Polisi pamoja na mikoa mingine ili kuwanasa watu wote ambao wanatajwa kuhusika na tukio hilo.

Licha ya kuwakamata vijana hao, Kamanda Stephen alisema hali ya usalama katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Mtwara siyo salama na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi ili kuwafichua watu wabaya wanaopanga kufanya uhalifu.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na tukio hilo, alisema wasemaji wa matukio ya mikoani ni makamanda wa polisi wa mikoa
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment