Thursday, 31 October 2013

Wanafunzi wasimamishwa kwa kufanyia wengine mtihani, Mwalimu Mkuu awatoroka polisi


Wakati wanafunzi sita wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari  Nazarene wakisimamishwa masomo kwa kuwafanyia wenzao mtihani wa taifa wa kidato pili, mwalimu mkuu anayetuhumiwa kusuka mipango hiyo anadaiwa kuwatoroka polisi sita waliokuwa wamekwenda kumkamata. 

Hayo yalibainika jana katika shule hiyo iliyoko jijini Mbeya baada Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, aliyefanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.

Mulugo aliamua kuwasimamisha masomo kwa mwezi mmoja wanafunzi hao baada ya kupewa taarifa hizo, lakini kwa mshangao wa wengi mwalimu mkuu aliyetajwa kwa jina la Posiano Mlelwa, anadaiwa hajulikani alipo baada ya kuwatoroka polisi kukwepa mkono wa sheria.

Mbali na kuwasimamisha masomo wanafunzi hao, Mulugo pia aliagiza kukamatwa mara moja Mwalimu Mlelwa ili afikishwe mahakamani kwa tuhuma hizo.

Akizungumza mbele ya Mulugo, Mkaguzi wa Shule wa Kanda ya Nyanda za Juu, Mechant Mtandika, alisema wanafunzi hao walibainika kuwafanyia wenzao mitihani Oktoba 7, mwaka huu ikiwa ni siku ya pili ya mtihani huo huku wakiwa wameshawafanyia masomo matatu.

Alisema mbinu iliyotumika ni wanafunzi hao kupewa namba za mtihani za wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kimasomo wawafanyie mtihani huo.

Alisema wanafunzi hao walipohojiwa walikiri kuagizwa na mkuu wao wa shule kwenda kufanya mtihani huo, lakini wanafunzi waliokuwa wakiwafanyia mitihani hawawafahamu.

Akijibu maswali ya Mulugo, mmoja wa walimu alidai kuwa chanzo cha tatizo hilo ni tamaa ya mkuu wa shule hiyo ambaye aliamua kuwaingiza wanafunzi hao kwenye chumba cha mtihani.

Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Protas Mpogole, alisema kitendo cha mkuu wa shule hiyo cha kutoroka hakiizuii serikali kuchukua hatua kwa kuwa shule ni taasisi ambayo inapaswa muda wote kuwa na mkuu wake.

“Aliyetoroka ni mtu na nafsi yake, lakini tunachojua sisi ni kwamba mwalimu mkuu muda wote yupo na huyo aliyepo ndiye anayepaswa kuwajibika kwa kosa hili,” alisema Mpogole
.

Mulugo alisema amesikitishwa na kitendo cha mkuu wa shule hiyo kutoroka katika mazingira ya kutatanisha mbele ya askari sita wa Jeshi la Polisi na wakaguzi wa shule waliofika shuleni hapo kushughulikia tatizo hilo.

Aidha, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha Polisi kutolipatia uzito unaotakiwa suala hilo kwa kuwa baada ya mwalimu huyo kutoroka hakuna jitihada za dhati za kumtafuta, hata kutangaza kuwa mtuhumiwa ametoroka.

Mulugo alisema kuwa ili kesi hiyo iliyofunguliwa katika kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya ipate msukumo, anaamua kuwasimamisha masomo wanafunzi sita wa kidato cha tatu ambao waliwafanyia wenzao mitihani.

Alisema wanafunzi hao hawajafukuzwa shule isipokuwa wamesimamishwa masomo kwa kipindi cha mwezi mmoja na kuwa baada ya muda huo wazazi wao wawahamishe shuleni hapo ili waendelee na masomo katika shule nyingine kwa ajili ya usalama wao.

“Kuanzia sasa hawa wanafunzi sita hawatakuwa tena wanafunzi wa shule hii, nimewasimamisha masomo kwa mwezi mmoja na baada ya hapo watahamishiwa shule nyingine waendelee na masomo,” alisema Mulugo.

Mulugo aliagiza mwalimu huyo popote alipo akamatwe na Polisi na kurejeshwa Mbeya huku akitahadharisha kuwa shule yoyote itakayomuajiri kabla ya kumalizika kwa kesi hiyo itafutiwa usajili.

“Mwalimu huyu ni afadhali ajisalimishe mwenyewe, kwa sababu kuanzia sasa haruhusiwi kufundisha katika shule yoyote nchini na shule itakayomwajiri nikigundua naifutia usajili,” alisema.

Katika hatua nyingine Mulugo alitembelea katika Shule ya Sekondari ya Hollywood ya wilayani Mbozi, ambako wanafunzi 69 wa kidato cha pili walizuiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili kwa madai kuwa hawakufikisha wastani uliowekwa na shule hiyo kwenye mitihani yao ya shule.

Akiwa shuleni hapo, Mulugo alisema kuwa mtihani pekee halali ambao umewekwa kisheria ambao mwanafunzi akishindwa anaruhusiwa kukariri kidato ni mtihani wa taifa wa kidato cha pili.

Alisema kitendo cha uongozi wa shule hiyo kuwazuia wanafunzi hao kufanya mtihani huo ni kosa kubwa kwa mujibu wa sheria na kuwa kitendo hicho hakikubaliki kwa vile bila ya mwanafunzi kufanya mtihani wa kidato cha pili haruhusiwi kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne.

Mulugo ameamuru wanafunzi hao kurudia  kidato cha pili na kuuagiza uongozi wa shule hiyo kuwalipia gharama zote za masomo.

Alisema kuwa wanafunzi hao watasoma tena upya masomo ya kidato cha pili kuanzia Januari mwakani na hatakiwi kulipishwa fedha yoyote kwa kipindi chote cha mwaka watakapokuwa wakisoma kidato cha pili.

“Naamuru wanafunzi wote 69 warudie upya kidato cha pili na nimeuagiza uongozi wa shule kuwalipia gharama zote za masomo hata kama wataamua kuhamia shule nyingine,” alisema Naibu Waziri huyo.

Aidha, alimuagiza mmiliki wa shule hiyo kumuondoa madarakani mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Mtafya, kwa kosa la kukiuka taratibu na sheria za nchi.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment