Friday, 1 November 2013

Ahukumiwa akiwa uchi

MAHAKAMA ya Mwanzo ya Kyagoro, iliyopo wilayani Rorya, imemhukumu kufungo cha miezi sita jela, Patrik Nyojwang (70), akiwa uchi baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumtorosha mtuhumiwa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina moja la Steven, alisema tukio hilo limetokea hivi karibuni mahakamani hapo.
Alisema Nyojwang alikumbwa na mkasa huo baada ya mtuhumiwa aliyemdhamini kutoroka huku akishindwa kutoa taarifa mapema.
Kutokana na hali hiyo, hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, aliyetajwa kwa jina moja la Gundula, aliagiza mdhamini akakamatwe kwa sababu ya kutotoa taarifa.
Steven alisema hakimu huyo alimueleza Nyojwang kuwa kosa alilolitenda faini yake ni sh 500,000. Aliachiwa na kesi kupangwa siku nyingine.
Alisema siku ya kutajwa kesi hiyo, Nyojwang alichelewa kufika mahakamani kitendo kilichomfanya akakamatwe na kutiwa mahabusu, na siku iliyofuata alitakiwa mahakamani tena.
Steven alisema wakati akisubiri kupelekwa mahakamani, Nyojwang alivua nguo na kubaki uchi ikiwa ni ishara ya kupinga kitendo hicho.
Alisema walijaribu kumsihi avae nguo, lakini alikataa akidai yuko tayari hata kufa kutokana na manyanyaso hayo.
Baada ya mvutano huo, hakimu aliamuru mgambo kumpeleka mahakamani na kuendesha kesi hiyo. Alimuhukumu kifungo cha miezi sita jela pamoja na kumtaka kulipa faini hiyo.
Alieleza hadi anapelekwa gerezani alikuwa ameshalipa sh 390,000.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kama kuna sheria inayoelekeza hivyo, Hakimu Gundula alisema haikuwa rahisi kwake kuizungumzia hukumu hiyo kwa kuwa yeye siyo msemaji.
Alisema wanaopaswa kulalamika ni wahusika tena kwa kuandika barua inayohusu hukumu hiyo na sio vinginevyo.
Akizungumzia hukumu hiyo, mmoja wa wanasheria alisema kabla ya hukumu mtu huyo alipaswa akapimwe akili, ili kubaini kama alikuwa kichaa au la.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment