Friday, 8 November 2013

Mbunge wa chadema aswekwa lupango

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, imemwamuru kwenda gerezani siku 14 Mbunge wa Ukerewe, Salvatori Machemli (CHADEMA), kwa kosa la kudharau mahakama.
Machemli ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi, aliamriwa kwenda gerezani jana baada ya kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi yake.
Taarifa kutoka mahakamani hapo, zilisema kuwa katika kesi hiyo, Machemli anadaiwa kutumia maneno ya uchochezi katika mikutano mbalimbali ya hadhara wilayani humo mwaka jana, na kwamba amekuwa akienda nje ya wilaya hiyo na hata nje ya nchi bila idhini ya mahakama.
Inadaiwa kwamba, Machemli alipofika mahakamani hapo jana kwa lengo la kuhudhuria kesi yake hiyo, alifutiwa dhamana kisha kuamriwa kuwekwa ndani.
“Ni kweli mahakama imetoa amri ya kuwekwa ndani mheshimiwa Machemli kwa kosa la kudharau mahakama. Alikuwa hahudhurii tarehe za kesi yake, kutokana na hali hiyo, leo alipokuja mahakamani kuhudhuria kesi yake aliondolewa dhamana kisha akaswekwa ndani,” kilisema chanzo chetu.
Ilidaiwa kwamba, hakimu anayesikiliza kesi hiyo alimtaka Machemli kuwasilisha wadhamini wawili wapya wanaomiliki hati ya nyumba, ambao walipatikana, lakini hakimu akabaki na uamuzi wake wa kutaka mbunge huyo aende gerezani kwa siku hizo 14.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu, Machemli alithibitisha kuondolewa dhamana kisha kuwekwa ndani kwa kosa la kudharau mahakama.
“Ni kweli wameniweka ndani. Ninapozungumza na wewe hapa nipo mahakamani nasubiri wanipeleke ndani…daah haya ni majanga! Nilikuwa nahudhuria vikao vya Bunge huku mahakamani sikuweza kufika.
“Lakini nilikuwa natuma watu wawili kuniombea ruhusa, sasa yawezekana pengine hawakuwa wanakwenda ndiyo maana nimewekwa ndani,” alisema Machemli
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment