Saturday 16 November 2013

Mwili wa , Dk. Sengondo Mvungi kuwasili leo

Mwili wa aliyekuwa Mjumbe Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, ambaye alifarikia dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini, unatarajiwa kuwasili nchini leo saa 12:50 jioni kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

Taarifa iliyotolewa na Tume kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa, taratibu za kuusafirisha mwili huo zimekamilika chini ya uratibu wa Ofisi ya Ubalozi waTanzania nchini Afrika Kusini.

Baada ya kuwasili, mwili huo utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhifadhiwa na kesho mwili wa Dk. Mvungi utaagwa katika Viwanja vya Karimjee.

Mwili huo utasafirishwa keshokutwa kwenda Kisangara Juu, wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu.

Dk. Mvungi alifariki Jumanne wiki hii baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya tangu ahamishiwe Milpark kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) alikokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa na majambazi na kumkata mapanga nyumbani kwake Mpigi Magohe, Mbezi jijini Dar es Salaam.

Katika ujambazi huo mbali ya kumjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita, majambazi walipora vitu mbalimbali nyumbani hapo ikiwamo kompyuta mpakato, simu za mkononi, nyaraka na fedha.

DEREVA WAKE ASIMULIA
Katika hatua nyingine, aliyekuwa dereva wa Dk. Mvungi, amesema watu wamaosadikiwa kuwa ni majambazi waliosababisha kifo hicho walivunja milango mitatu hadi kuingia sebuleni na kufyatua baruti.

Dereva huyo, Emmanuel Ntarima, ambaye anaishi umbali wa takribani mita 100 karibu na makazi ya marehemu, alisema akiwa nyumbani kwake saa 7:00 usiku, alisikia mlipuko mkubwa na kuhisi kuwa nyumbani kwa Dk. Mvungi si salama na kwamba awali alidhani ni hitilafu ya umeme.

“Nilishtuka na kusikia kishindo kikubwa huku nikitazama nyumbani kwa Dk. Mvungi kupitia dirishani kwangu na kuona taa za tochi zikimulika nje na ndani…moja kwa moja nilijua kumevamiwa, niliwasiliana na jirani mmoja na polisi ili kuomba msaada, ambao walinishauri nisitoke nje kwa kuwa watu hao watakuwa wamejipanga nje kwangu pia,” alisema.

Alisema baada ya taarifa kusambaa watu walianza kupiga kelele na kujitokeza na ndipo wahalifu hao walitokomea na ndipo aliweza kutoka.

“Mimi na jirani yetu mwingine ndiyo tulikuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa Dk. Mvungi, niliongea na fundi aliyekuwa amelala kwenye chumba cha chini, alinieleza jinsi majambazi walivyoingia na kumkamata,” alisema.

Ntarima alisema fundi huyo alimueleza kuwa alishtuka akinyanyuliwa kitandani na kupigwa huku akitakiwa kuonyesha alipo Dk. Mvungi na kwamba mlango wa nje waliuvunja kwa kutumia jiwe maarufu kama ‘Fatuma’.

Alisema walivunja mlango wa pili na kupanda ngazi na kuvunja mlango mwingine wa kwenda sebuleni na ndipo walikutana na Dk. Mvungi akitoka baada ya kusikia purukushani na walimshambulia hapo hapo.

Alisema mjane wa Dk. Mvungi alimueleza kuwa baada ya kuona wamemvamia mumewe, alitoka nje kupitia mlango wa mbele kwenda kumuamsha mlinzi anayeishi nje ya uzio na mmoja wa majambazi hayo alimuona na kumkamata akitaka aonyeshe zilipo fedha.

Alisema baada ya yeye (dereva) na majirani kufika walimchukua Dk. Mvungi na kumpeleka Hospitali ya Tumbi  kupata matibabu na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Kwa njia walizotumia majambazi wale kufika hapa ni wenyeji kabisa, si watu wageni, fundi alinieleza baadhi walificha sura na kubakiza macho na wengine hawakuficha sura,” alisema.

Alisema waliingia kwenye nyumba vingine na kukatakata mabegi wakitafuta fedha, huku wakitoa nguo na kumfunika waliyemkuta kitandani na hawakuruhusu mtu kuwaangalia usoni na kwa aliyekiuka alipigwa kwa ngumi na ubapa wa panga.

DK. BILAL AFARIJI WAFIWA
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, jana aliungana na waombolezaji wengine kuifariji familia ya Dk. Mvungi, nyumbani kwake eneo la Mpiji Magohe, jijini Dar es Salaam.

Dk. Bilal aliwasili saa 8:38 na kupokelewa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, na kwenda kumpa pole mjane wa marehemu, Anna Mvungi na baadaye kuwasalimu waombolezaji na viongozi wengine waliofika nyumbani hapo.

Alisema walishamaliza kufanya uchunguzi katika mwili wake na wanaendelea na taratibu za kuusafirisha.

“Mwili utawasili leo majira ya sa 12:55 jioni katika uwanja wa ndege wa mwalimu Julius Nyerere na kupokelewa na waombolezaji na baadaye kupelekwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo,” alisema Mbatia.

Alisema kesho  asubuhi ibada ya kumuombea marehemu itafanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph. 

Alisema Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, Rogart Kimario, ataongoza ibada ya mazishi inayotarajiwa kuanza Jumatatu  saa 3:00  asubuhi hadi saa 8:00 atakapolazwa katika nyumba yake ya milele.  

‘TUWEKA UTAIFA MBELE’
Mbatia alisema yapo mengi yanayozungumziwa juu ya msiba huo, lakini ni vyema Watanzania wakajipa utulivu wa ndani kutafakari kwa kina ili kulivusha Taifa katika kipindi hiki kigumu cha mjumbe aliyetarajiwa kufanya kazi kubwa kwa manufaa ya Taifa.

Alisema Dk. Mvungi alikuwa mtumishi mzalendo, muadilifu na mwenye kupenda watu na kuhudumia kila Mtanzania bila kujali.

“Alitufundisha Katiba ni jambo la maridhiano, jamii kwa pamoja, tuondokane na dhana kuwa ni ya watawala dhidi ya watawaliwa bali ya umma wa Watanzania kukubaliana…hivyo alikuwa mwalimu wa Taifa letu, kifo chake ni mtihani mzito kwetu, tusiseme Mungu ametaka hivyo ni mapema mno bali tuendelee kutafakari,” alisema Mbatia.

RAIS WA ZANZIBAR AMLILIA DK. MVUNGI
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amempelekea salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kufuatia kifo Dk. Mvungi.

Katika salamu zake, ameeleza kusikitishwa na kupata simanzi kubwa kwa kifo HICHO na kukieleza kuwa ni pigo kwa maendeleo ya Taifa na ni msiba wa Watanzania wote.
“Ni mzalendo mwenye upendo mkubwa kwa nchi yake na mtaalamu wa sheria, vilevile mwanasiasa shupavu na makini,” alisema Dk. Shein.

 ALIongeza kuwa yeye binafsi, wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamehuzunishwa na kifo chake na kwamba wanatoa rambirambi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, familia, jamaa na marafiki na wenzake marehemu.

BARAZA LA VYAMA VYA SIASA LAMLILIA
Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, limesema limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk. Mvungi, na kueleza kuwa wanaungana na watanzania wote katika kipindi hiki cha maombolezo.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray, alisema kuwa Baraza  linatambua mchango mkubwa wa marehemu wakati wa uhai wake kwa taifa.

Alisema kuwa kifo cha Dk. Mvungi kimetokea wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Taifa kwa ujumla vikihitaji ushauri wake adimu wa masuala ya Katiba.

Alisema vyama vya siasa na taifa kwa ujumla limepoteza ndugu, msomi, mtaalamu wa masuala ya katiba na mzalendo wa Taifa.

MCT YAMLILIA
Baraza la Habari Tanzania (MCT), limepokea kwa masikifiko makubwa kifo cha Dk. Mvungi.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema Baraza litamkumbuka kama mtetezi mahiri wa uhuru wa vyombo vya habari na wa kujieleza na haki ya kupata habari. 
Alisema alijitoa kwa hali na mali kutetea mabadiliko ya kikatiba na kisheria iii kuwezesha haki hizo zipatikane nchini.

Alisema Dk. Mvungi alikuwa mjumbe wa bodi ya MCT kuanzia 1997 hadi 2005 na Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza. 

“Atakumbukwa na tasnia ya habari kwa kazi yake kubwa aliyoifanya katika kupigania mazingira bora ya utendaji kazi ya vyombo vya habari nchini kwa kutetea mabadiliko ya kisheria na ya Katiba,” alisema Kajubi.

Alisema pia Dk. Mvungi atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika kutayarisha mapendekezo ya wadau wa habari kwenye mapendekezo ya muswada wa sheria wa Haki ya Kupata Habari na ule wa Huduma za vyombo vya habari.

Alisema Baraza linatoa rambirambi zake kwa familia na rafiki zake, Mwenyekiti, makamishna na wafanyakazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mwenyekiti wa chama cha NCCR¬Mageuzi ambako marehemu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

MAJAJI WAMIMINIKA MSIBANI
Viongozi wengine waliofika kuifariji familia hiyo ni majaji wa Mahakama ya Rufani, Amir Manento, Januar Msofe na majaji wengine 10.

Majaji wengine ni Sekieti Kihuo, Robert Makaramba, Shaaban Lila, Ibrahim Juma na Njegafibili Mwaikugile.

 chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment