Friday 29 November 2013

UNATEMBEZA OFA BAA, MKEO ANAVAA MIDABWADA, INAHUU?

Kikubwa nilichodhamiria  hapa ni kwamba, wapo baadhi ya wanaume ambao wanajikuta wakiishi na watu wasio na mapenzi ya dhati kwao kwa sababu ya tabia yao ya ubahili.
Mwanaume anakuwa mgumu kumpatiliza mkewe katika mambo ya msingi. Mke hana nguo nzuri, anakula ilimradi ameweka kitu tumboni lakini ukifuatilia unakuta mwanaume ana pesa na anazitumia kwa kuwahonga mademu na kulewea.
Hivi katika mazingira hayo, mwanamke huyo atakuwa na penzi la dhati kweli kwa mumewe? Kwa kifupi ni ngumu sana na ukifuatilia kwa karibu utabaini kuwa, wanawake wengi wanawasaliti waume zao kwa kukosa huduma muhimu ambazo uwezekano wa kuzipata upo.
Sisemi mwanamke asipopatilizwa na mumewe basi atafute mwanaume mwingine wa kumtimizia ila ninachomaanisha hapa ni kwamba, wapo wanaume ni kama wanawalazimisha wenza wao kuwasaliti.
Tukumbuke furaha ya penzi ni wawili waliotokea kupendana kwa dhati kutimiziana katika yale ambayo yamo ndani ya uwezo wao. Kama una pesa ya kutosha, mfanye mkeo awe wa kipekee mtaani kwenu. Avae vizuri, ale vizuri, aishi kwenye nyumba nzuri, aendeshe gari zuri na mengineyo yaliyo ndani ya uwezo wako.
Lakini usimtimizie katika hayo kisha ukawa ni mtu wa kurudi usiku wa manane ukiwa umelewa, hapo bado utakuwa hujafanya kitu kwani mapenzi hayaashii kwenye kumpatiliza mkeo katika hayo tu. Kuwa naye karibu, kumpa haki zake za kindoa na mambo mengine ni wajibu wako kumfanyia ili kumfanya asifikirie kukusaliti.
Lakini hili lisifanywe na wanaume tu. Wapo wanawake pia ambao wana fedha lakini hawawajali waume zao. Mke anapokea mshahara lakini hata siku moja hajawahi kusema leo nimnunulie mume wangu nguo ya ndani.
Hilo nalo linaashiria mapenzi ya dhati hakuna na matokeo yake sasa mume akipata mtu wa kumnunuliamara leo fulana, kesho kiatu, keshokutwa saa, taratibu anapumbazwa na unaweza kushangaa unaachwa solemba.
Nini dhamira hasa ya kuandika makala haya? Ni kwamba, ubahili kwa watu tuliowapa nafasi kwenye mioyo yetu haufai. Kila unachokipata hakikisha mnakitumia na mwenzako wako na kama hamjajaaliwa kuwa nazo basi ridhikeni ilimradi mnapendana kwa dhati.
Itakuwa ni jambo baya sana kama unapokea mshahara kisha unaishia kuutumia kuwasaidia ndugu zako na kufanya mambo yako bila kumjali mwenza wako.
Utaonekana kituko kama utakuwa ni hodari wa kutoa ofa kwa washikaji wakati mkeo akikatiza mtaani anaonekana kavaa midabwada.
chanzo:

No comments:

Post a Comment