Friday 29 November 2013

Wachimba madini acheni ulevi, vimada

WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wametakiwa kuacha tabia ya kufuja hovyo fedha kwa kufanya matanuzi kwenye mabaa, kumbi za starehe na kubeba vimada pindi wapatapo fedha na kujiona kuwa mabingwa wa matumizi.
 “Wachimbaji wenzangu badilini tabia ya matumizi ya fedha, jengeni utamaduni wa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili fedha mnazozipata ziweze kuwaletea maendeleo endelevu, jengeni nyumba bora, somesheni watoto wenu, yaani tumejijengea mazoea mabaya sana kuwa sisi ni mabingwa wa starehe,” alisema.  
 Changamoto hiyo imetolewa juzi mjini hapa na Rais wa Shirikisho la wachimbaji madiniTanzania (FEMATA), John Bina, wakati akifungua kikao cha kamati ya dhahabu ya FEMATA taifa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati.
 Alisema wachimbaji madini wamekuwa na sifa mbaya kwa madai kwamba wengi hutumia fedha vibaya na kusababisha kazi za madini kutowanufaisha kimaisha.
 Bina alisema matumizi  mabaya ya fedha yana madhara mengi, ikiwemo mhusika kufilisika mapema.
 “Uzoefu unaonyesha kwamba mchimbaji akipata kwa mfano sh milioni 10, kipaumbele chake kinakuwa ni  kuoga mwili kwa  pombe (bia), ataacha kuchimba madini na kutumbukia kwenye anasa hadi fedha zitakapomwishia,” alifafanua rais huyo.
 Kwa hali hiyo, Bina aliwataka wabadilike na kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili fedha wanazozipata ziwasaidie kujiletea maendeleo wao binafsi, familia zao, mkoa wao na taifa kwa ujumla.
 Bina aliwataka wachimbaji madini kujiepusha na uchimbaji haramu, pia wajenge utamaduni wa kulipa kodi ili kujijengea mazingira ya kukopesheka na taasisi za kifedha.
 Katika hatua nyingine, kikao hicho cha kamati ya madini taifa kilimteua Katibu Mkuu wa Chama cha wachimba madini Mkoa wa Singida (SIREMA), Farjala Kiunsi, kuwa katibu wa FEMATA taifa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment