Monday 16 December 2013

Kijana aambiwa aende kwa baba yake baada ya aliyedhani ni baba kufariki!

Katika ujumbe wake kijana huyu anasema; ndugu zangu wananitenga na kuniambia niende kwa baba yangu eti hapo ninapoishi siyo kwetu! Hivi sasa nina umri wa miaka 28 na mama yangu hakuwahi kuniambia kuwa baba yangu ni mwingine na siyo yule aliyenisomesha ambaye kwa sasa ni marehemu. 
 
“Nimejaribu kumdadisi mama yangu nikagundua kwamba kumbe yule aliyekuwa ananilea tangu nazaliwa akanisomesha, nikakaa vizuri na wadogo zangu kwa kuwa mimi ndiye wa kwanza kuzaliwa, hakuwa baba yangu mzazi. Sikujua kwanini mama alinificha. 
 Baada ya ujumbe huo ilibidi nimpigie simu kijana huyu na kumpa maswali ambayo angemdadisi nayo mama yake mzazi na kunijulisha yafuatayo.
 
Kwa maelezo ya kijana huyu, inasemekana kwamba mama yake kabla ya kuolewa na mume ambaye ndiye aliyejua kuwa ni baba yake(sasa marehemu), alikuwa na urafiki na kijana mwingine.
 
Huyo kijana ndiye aliyekuwa mpenzi wa mama yake hasa lakini akajitokeza kijana mwingine ambaye alimrubuni mama yake akamuacha mpenzi wa awali.
 
Kumbe wakati mama huyu anaanzisha mahusiano mapya na kijana huyo wa pili, tayari alikuwa na mimba ya kijana wa kwanza ambaye ndiye bwana mdogo anaambiwa amtafute kuwa ndiye baba yake mzazi na siyo yule aliyemlea ambaye sasa ni marehemu.
 
Bibie baada ya kumwacha mpenzi wa kwanza akajikamatisha na yule wa pili ambaye ndiye aliyefunga naye ndoa. Lakini kumbe tayari mimba aliyokuwa nayo ni ya mpenzi wa kwanza aliyemuacha. Na mimba hiyo ndiyo kijana huyu anayefukuzwa aende kwa baba yake.
 
Hadi mama huyu anafiwa na mumewe, hakuwahi kumwambia kijana wake huyu kwamba yule hakuwa baba yake mzazi. Lakini sasa ni miaka miwili tangu mumewe afariki ndipo yanaibuka hayo ya ndugu zake wanamwambia aondoke aende kwa baba yake.
 
Kijana huyo ameniambia kwamba amechunguza na tayari ameshaungana na baba yake halisi ambaye naye kimaisha hayuko vizuri lakini anasema atajitahidi kuchakarika ili aweze kuinuka na kumtunza baba yake.
 
 Bila shaka umepata picha kuhusu maisha ya kijana huyu. Kwamba alijua yule anayemtunza baba na mama wote ni wazazi wake halisi kumbe mmoja ni mama mzazi lakini baba ni mlezi siyo mzazi.
 
Hapa lipo somo moja muhimu kwa kinababa. Mwanamme anapokuambia ana ujauzito wako, chunguza kwa makini ili kujiridhisha kuwa mimba ile wakati inatengenezwa ilikuwa ni yako, vinginevyo utabambikiwa mtoto pasipo kujitambua. 
 
 
 
Hatua ya Serikali kuleta nchini kipimo cha Deoxyribonuleic acid (DNA)  kujua uhalisia wa baba wa mtoto anayezaliwa pale yanapoibuka mashaka miongoni mwa wazazi, imesaidia kupunguza migogoro ndani ya familia. 
 
Kwa mujibu wa kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA), Daniel Matata hivi karibuni, kwa takribani mwaka mmoja sasa, ofisi yake imeamua kubadili utaratibu wa kupokea sampuli kutoka kwa wazazi ambao hawana uhakika na baba wa mtoto.
 
Matata katika mahojiano na gazeti la Serikali The Daily News toleo la Jumamosi Machi mwaka huu alisema kuwa baada ya kushuhudia ugomvi wakati wazazi wanapokuja kutafuta uthibitisho, hivi sasa sampuli zinaletwa kwenye maabara kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii na polisi au mahakama.
 
“Tulilazimika kubadili utaratibu kwa sababu hata kabla ya wanandoa hawajalifikia lango la ofisi zetu huanza kutwangana”, alisema.
 
Takwimu bado zinaendelea kukusanywa  lakini kulingana na ripoti ya mwaka 2010, vipimo vilivyochukuliwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2009 kwa watu 250, vinaonyesha wastani wa asilimia 50 ya watoto siyo baba yao. 
 
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa yenye uhakika zaidi ni ya mwaka 2005 na 2006 ikionyesha kuwa asilimia 60 ya watoto ambao walifanyiwa vipimo vinasaba havikufanana na vya baba zao.
 
Sampuli zilizochukuliwa mwaka 2006 na 2007 zilionyesha kuwa asilimia 47 ya watoto waliofanyiwa vipimo vilionyesha havifanani na vile vya baba zao, ambapo uchunguzi uliofanyika pia mwaka huo ukaonyesha asilimia 53 vipimo vilihusiana. 
 
Rekodi nyingine mwaka 2007 na 2008 zikaonyesha asilimia 51 ya watoto hawakuhusiana na baba zao ambapo asilimia 49 vipimo vilihusiana.
 
Mpenzi msomaji, takwimu hizo zitakupa mwanga kuhusu watoto wanaozaliwa ndani ya ndoa zenu. Kijana niliyemjadili mwanzoni mwa makala haya ananyanyaswa na kama baba yule aliyemlea angetilia shaka baada ya kuzaliwa na kumfanyia kipimo cha DNA, bila shaka angegundua uhalisia wa mtoto mapema.
 
Kwa maneno mengine, nadhani mama alijua fika kuwa mimba ile ilikuwa ya mtu mwingine lakini akajikausha akang’ang’ania ndoa na mtu mwingine. 
 
Kijana huyu ingawa anamshukuru baba mlezi kwa kumlea na kumsomesha hadi hapo alipofikia, lakini bado anadhani mama yake hakumtendea haki kwa kumficha baba yake halisi ambaye amemuona hivi sasa na wanawasiliana.
 
Anachofanya kijana huyu hivi sasa anajaribu kuwajua ndugu za baba yake na tayari ameshamjua bibi(mama mzaa baba yake) , shangazi zake na wengineo jambo ambalo linampa raha sana
Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment