Monday 2 December 2013

Mkwe wa Lowassa matatani,Asajili kampuni yake kwa nyaraka bandia,

WAKATI nchi ikiendelea kuandamwa na zimwi la kuporomoka kwa majengo,Tanzania Daima Jumapili limebaini udhaifu mkubwa kwenye Bodi ya Makandarasi (CRB).
Uchunguzi wa gazeti hili kwa takribani wikimbili, umejiridhisha pasipo shaka kwamba CRB imeisajili Kampuni ya Visual Storm Co. Ltd kwa kutumia nyaraka bandia na imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa bila kuisajili kwenye bodi hiyo kama sheria inavyosema.
Kampuni hiyo inamilikiwa na Noel Severe (30), mtoto wa mkurugenzi wa zamani wa wanyamapori, Emmanuel Seveve ambaye wakati fulani aliingia kwenye mgogoro wa kiuongozi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo.
Severe ni mkwe wa waziri mkuu aliyejiuzulu ambaye pia ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye amemuoa bintiye aitwaye Dk. Adda Lowassa.
Katika kile kinachoonyesha kuwepo kwa nguvu ya viongozi nyuma ya pazia, Visual Storm iliweza kupewa mkataba wa ukarabati wa tawi la Benki ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB) mwaka 2011 ikiwa bado haijasajiliwa na CRB kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili linazo, kampuni hiyo ilisajiliwa kwa Msajili wa Makampuni (Brella) mwaka 2009 kwa No. 71362 na kisha CRB Februari 23, 2013 kwa No. B5/0674/2/12 daraja la tano.
Gazeti  limebaini kuwa kabla ya usajili CRB, Visual Storm iliingia mkataba na DCB Oktoba 3, 2011 wa kujenga ukumbi wa mikutano katika tawi la Ukonga kwa gharama ya sh 56,676,580 kwa muda wa wiki tano.
Hata hivyo, hadi kufikia Januari 9, 2013 zaidi ya mwaka mmoja, kampuni hiyo ilikuwa imeshindwa kukamilisha kazi hiyo, hatua iliyomlazimu Mkurugenzi Mkuu wa DCB, Edmund Mkwawa kuiandikia akiitaarifu kusudio la kutaka kuvunja mkataba huo.
Nakala ya barua hiyo pia ilipelekwa kwa msajili wa CRB, Boniface Muhegi, ambapo Februari 12, 2013, bodi hiyo kupitia kwa kaimu meneja wa Kanda ya Mashariki, D. J. Karugendo, ilijibu kwa kuiandikia Visual Storm na kuipa siku saba itoe maelezo ya kushindwa kutimiza mkataba huo.
Alipotafutwa Mkwawa ili kufafanua ni kwanini benki yake iliingia mkataba na kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa CRB, alisema kuwa suala hilo aulizwe Visual Storm.
“Tunawasubiri hao CRB tukutane mahakamani, lakini kwanini usiwaulize Visual Storm wakakupa majibu?” alisema.
Hadi gazeti  linafanya uchunguzi huo, CRB inadai kuwa haikuwa na taarifa ya kasoro hiyo ya Visual Storm kuvunja sheria ya kuingia mkataba wa ujenzi bila kusajiliwa, licha ya kupata barua ya malalamiko ya DCB.
Katika kosa hilo, Muhengi anathibitisha kuwa kampuni hiyo inapaswa kuadhibiwa kwa kutozwa faini pamoja na DCB kwa kutoa zabuni kwa kampuni ambayo haikuwa na usajili wa Bodi ya Makandarasi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, kampuni hiyo ililazimika kukimbilia CRB kujisajili baada ya kushindwa kutimiza mkataba wa DCB kwa wakati, na hivyo kuhofia kukumbwa na rungu la adhabu baada ya benki hiyo kuanza kulalamika.
Hata hivyo, katika kujinasua, kampuni hiyo ilitumia nyaraka na vielelezo visivyo halali, hatua ambayo Muhegi anasema itasababisha sasa iadhibiwe kwa kufutiwa usajili wake, na wamiliki wake kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ili kampuni iweze kusajiliwa CRB, Muhegi anasema ni lazima itimize vigezo kadhaa kulingana na daraja husika ambapo wamiliki wanatakiwa kuwa na wataalamu, ofisi na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wa wataalam, kampuni inapaswa kuwa na mkurugenzi wa ufundi ambaye amesajiliwa na Bodi ya Mainjinia (ERB) ambaye atakuwa ameajiriwa na kampuni husika na kuwa mmoja wa wanahisa.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Kampuni ya Visual Storm, awali iliwasilisha vielelezo vya vyeti vya Loserian Sokonoi ambaye hata hivyo alitofautiana na mmiliki Severe na kuamua kuondoka na kuajiriwa serikalini mkoani Shinyanga.
Kampuni hiyo katika kusaka usajili wa haraka, ilitumia cheti cha Kent Kissima na kumtambulisha kama mkurugenzi wao wa ufundi ilhali mtu huyo ni mwajiriwa wa serikali akifanya kazi kama meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) makao makuu.
Awali katika majibu yao, CRB walijikanganya wakidai mkurugenzi wa ufundi wa kampuni hiyo ni Sokonoi, lakini walipobanwa zaidi wakadai ni Kissima ambaye inadaiwa amehamishwa makao makuu Tanroads na kupelekwa kuwa meneja wa Mkoa wa Simiyu.
“Mimi ninamfahamu Kissima kama ‘technical director’ wa Visual Storm wala si Sokonoi,” alisema Muhegi lakini alipoelezwa kuwa Kissima ni mwajiriwa na Tanroads akafichua siri kuwa kampuni hiyo vielelezo vyake vyote vilikuwa vya kughushi.
“Tumekwenda huko TRA (Mamlaka ya Mapato) tumekuta kadi za vifaa walizowasilisha huko sio vya kwao, kinachofuata sasa ni kuifuta na kuanza utaratibu wa kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na vyombo vingine vya kisheria,” alisema.
Hata hivyo, Muhegi alipobanwa alionyesha kuhamaki mara kadhaa na kuhusisha suala hilo na fitna za kisiasa, akisema; “najua aliyekutuma ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.”
Alipoulizwa ilikuwaje hawakujiridhisha na umiliki wa vifaa hivyo kabla ya usajili, alitoa majibu yasiyoridhisha akisingizia kuwa bodi yao haina mtandao wa kuweza kufuatilia makandarasi wote.
Alipotafutwa Sokonoi kuthibitisha kama ndiye bado mkurugenzi wa ufundi wa kampuni hiyo, alijibu kwa msisitizo kuwa; “Huyo jamaa tulifanya naye kazi, lakini wakati tukiwa kwenye mchakato huo wa usajili alionekana kunizika fedha zangu nikajiondoa.
“Mimi kwa sasa niko Shinyanga nimeajiriwa serikalini na nilikwishawaandikia CRB kuwaarifu kuwa vyeti vyangu visitumike popote kwenye taasisi yao kwa namna yoyote, maana sifanyi kazi huko tena.”
Hata hivyo, katika kile kinachoonyesha udhaifu wa CRB, gazeti hili linayo nakala ya makubaliano kati ya Visual Storm na Kampuni ya Fabec/Home base (T) Ltd.
Makubaliano hayo yanaonyesha kuwa wakati wa kukaguliwa vifaa vya ujenzi, Visual walionyesha kwa CRB mkataba huo wakidai vifaa vyao wameikodishia Fabec iliyokuwa na kazi ya ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Mpanda wakati huo.
Msemaji wa Fabec, Ziota, alipotafutwa alilieleza gazeti hili kuwa kampuni yao haijawahi kuwa na mkataba wa aina hiyo na Visual.
“Kampuni hiyo wala sijawahi kuisikia, inamilikiwa na nani?” alihoji Ziota na kufafanua kuwa hata kama wangekuwa wamekodishwa vifaa hivyo, CRB walitakiwa kutembelea mradi wao kujiridhisha kama vipo kweli.
Hata baada ya kusajiliwa CRB, Kampuni ya Visual Storm imeendelea kutekeleza miradi yake mikubwa ikiwemo ile ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) bila kuisajili kwenye Bodi ya Makandarasi kama sheria inavyosema wala kufuata taratibu za kuwa na vibali vya ujenzi.
Severe ajitetea
Alipotafutwa kujibu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Visual Storm, Severe alikiri na kuonyesha mshangao akihoji nani alivujisha suala hilo kwenye vyombo vya habari.
Alidai kuwa ameshangaa kuona nyaraka sahihi alizompatia mshirika wake kwa ajili ya kushugulikia usajili, zilibadilishwa na kupachikwa zile za kughushi.
“Kaka yaani nashangaa kwanini jambo hili linakuwa hivi, mimi hivi vifaa unavyonionyesha hapa kampuni yetu haina na sijui hawa walivitoa wapi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu utata wa mkurugenzi wao wa ufundi, Severe alimtaja Sokonoi kuwa ndiye waliyewasilisha jina lake CRB. Lakini alipobanwa aeleze inakuwaje mhusika anafanya kazi serikalini, alisema walikuwa kwenye mkakati wa kumbadilisha.
Alipoelezwa kuwa CRB wamedai wanamtambua Kissima kama mkugenzi wa ufundi wa kampuni hiyo, Severe alidai kutomtambua mtu huyo huku akionyesha kushangaa alichomekwaje na kuwa mmoja wa wanahisa.
Severe katika kujitetea alimtwisha lawama mtu aliyemtaja kwa jina la Ruben ambaye alidai kuwa alikuwa mshirika wake kuwa ndiye alivujisha siri hiyo kwa sababu wakati wa usajili CRB alihusishwa kwa ukaribu.
Tanzania Daima lilimtafuta Emmanuel Ruben, ambaye alikiri kushirikiana na Severe katika usajili wa kampuni hiyo CRB, lakini akasema kuwa baadaye walihitilafiana katika mgawanyo wa rasilimali na hivyo akajitoa na kuanzisha kampuni yake.
“Mimi pale CRB nina power of attorney (nguvu ya kisheria) kwa kampuni ya Visual Storm kwa vile tulikuwa pamoja, lakini kwa sasa niko kivyangu, sasa hayo ya kwamba nimeleta siri hiyo kwenu ndiyo nasikia kwako,” alisema Ruben.
chanzo:Tanznia daima

No comments:

Post a Comment