Friday 6 December 2013

Nchimbi abebeshwa zigo la Prof Kapuya

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi ameingia lawamani kwa kudaiwa kumlinda Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), anayedaiwa kumbaka na kumtishia kumuua binti wa miaka 16.
Akizungumza kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi wa simu (sms) na TanzaniaDaima jana, binti anayelalamika kutishiwa maisha na Profesa Kapuya, amemtuhumu Waziri Nchimbi kushindwa kulishughulikia suala hilo mapema licha ya kuwa na taarifa za tukio hilo muda mrefu.
Binti huyo alisema kuwa Dk. Nchimbi ni miongoni mwa mawaziri na viongozi wa CCM waliokuwa wakifahamu kila kinachoendelea dhidi ya malalamiko husika.
Alibainisha kuwa makada hao wa CCM walikuwa wakifanya jitihada za kuhakikisha manyanyaso na vitisho kutoka kwa Profesa Kapuya haviwekwi hadharani.
Katika kile kinachoonekana ni kukata tamaa juu ya usalama wake pamoja na dada yake, binti huyo alisema amewasiliana na Waziri Nchimbi asubuhi ya jana na kwamba waziri huyo hakuonyesha dalili yoyote ya kujali madhila yao.
Alisema kutokana na Waziri Nchimbi kutokutilia uzito malalamiko yao, waliamua kumuandikia ujumbe mfupi wa maandishi wakimshutumu kuendelea kumlinda Profesa Kapuya.
“Nimemwambia katika ujumbe mfupi wa maneno (sms) kuwa jukumu la polisi iliyo chini ya wizara yake ni kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya manyanyaso na vitisho vya aina yoyote, na kwamba katika kadhia hii ya Kapuya Jeshi la Polisi limekuwa kimya.
“Matukio mbalimbali ya kihalifu yenye kutatanisha yametokea nchini, lakini serikali inasema haiwajui wahusika na kwamba hata hili la kutishiwa maisha pia serikali inasubiri nife,” alisema binti huyo.

Binti huyo alisema katika ujumbe huo aliomtumia Waziri Nchimbi, pia amemdokezea kuwa haogopi kitakachompata ilimradi yupo katika msitari wa kutafuta haki yake.
Amedai kuwa hivi sasa bado kuna jitihada kubwa za watu walio karibu na Kapuya kuwataka waachane na suala hilo.
“Juzi mtu aliye karibu na Kapuya ametuhoji tunataka nini ili tuachane na jambo hili… sisi tumemjibu tunataka haki si kingine chochote,” alisema.
Jitihada za Tanzania Daima kumpata Waziri Nchimbi ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) haukujibiwa.
Wanaharakati walia na polisi

Wakati sakata hilo la Kapuya likiwa kwenye hali ya kutoeleweka, baadhi ya wanaharakati na watetezi wa masuala ya jinsia wamelitaja Jeshi la Polisi kwa kuchangia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia (TGNP).
Joseph Mathias, alisema vitendo hivyo vya ukatili vinaongezeka kutokana na polisi kuwalea na kuwalinda baadhi ya vigogo wanaovitenda.
Bila kumtaja jina, Mathias alisema hivi karibuni kiongozi mmoja anahusishwa na ubakaji na kutishia kuua, lakini hadi sasa hajafikishwa mahakamani.
Mathias, alisema pamoja na dawati la kupinga ukatili wa kijinsia kupata taarifa hiyo, lakini hadi leo halijamchukulia hatua yoyote ile kama inavyofanya kwa watu wengine waliofanya makosa kama hayo.
Aliongeza kuwa polisi bado ni tatizo katika mapambano hayo, na kama hawatabadilika kiutendaji kuna uwezekano tatizo hilo likazidi kushamiri.
“Kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria watu kama hawa, kumekuwa chanzo cha baadhi ya watu kuyachukulia matendo haya ya ukatili wa kijinsia kuwa ni haki yao,” alisema Mathias.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TGNP, Anna Sangai, alisema changamoto kubwa inayochangia vitendo hivyo katika jamii ni mila potofu.
“Sisi TGNP tunalichukulia kuwa ni la kirasilimali, hivyo tunaishauri serikali ijaribu kutenga fedha za kutosha na kuzielekeza kwenye Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili zifikishe elimu bila vikwazo kwa jamii,” alisema.
Anna alisema endapo jamii itapatiwa elimu kuhusu ukatili huo, anaamini kuwa vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa vitapungua.
Aidha, jamii nayo imetakiwa kuondokana na mila potofu kwa kuwaona wanawake si lolote katika kuchangia masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Mwakilishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Judith Kizenga, alisema serikali imejipanga kukamilisha sheria zote ambazo zitaweza kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Kuruthumu Mikidadi, ambaye ni mwakilishi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, alikiri kuwa dawati la jinsia linakabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini hali hiyo inatokana na uchanga wake.
Awali kwa nyakati tofauti, washiriki zaidi ya wanne kutoka mikoa ya Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam, walilishambulia dawati hilo kuwa watendaji wake wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kushindwa kutoa haki.
Walisema wakati mwingine mhalifu anamfikishwa kwenye dawati hilo, lakini cha kushangaza kesho unamkuta ameachiwa katika mazingira tata.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment