Wednesday, 4 December 2013

Ndugu washuhudia maiti Yahaya mochwari Temeke, akakutwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,Mtanzania Yahya Msemakweli, 34, (pichani) alifariki dunia, akawekwa chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari), ndani ya jokofu kwa siku tano na ndugu zake akiwemo mkewe, waliushuhudia mwili wake na kujiridhisha kuwa ni yeye.

Hata hivyo, siku ya sita ambayo ndiyo ilikuwa tarehe ya mazishi, walipoufuata mwili wa Yahya hawakuukuta mochwari, droo aliyowekwa, ilikutwa maiti ya kike, majokofu yote yakafunguliwa lakini hawakuuona.
Siku iliyofuata, yaani siku ya saba, Yahya akakutwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Alitokaje mochwari Temeke hadi Muhimbili wodini? Hakuna anayejua!
Nyongeza ni kwamba kaburi lilishachimbwa, sanda ilishanunuliwa tayari kwa mazishi ya Yahya lakini mambo yalipogeuka, ilibidi wazike mgomba kwa kile kilichoelezwa: “Kimila kaburi huwa halifukiwi tupu.”

MKE WA YAHYA ANASIMULIA
Mke wa Yahya, Mwanjaa Juma, alisema: “Mimi na mume wangu tunaishi Mtoni Madafu, Temeke. Mume wangu ni dereva wa bodaboda.”
Mwanjaa aliendelea kusimulia kuwa Novemba 22, mwaka huu, saa 5:15 usiku, alipigiwa simu na Yahya akamwambia yupo njiani anarudi nyumbani.
“Wakati huo aliniambia yupo Kilwa Mivinjeni. Mpaka saa 6:00 usiku alikuwa hajarudi, nikampigia simu ikawa haipatikani.
“Niliingiwa na wasiwasi sana, kulipopambazuka tu nilikwenda Mtoni Kwa Azizi Ally ambako ndiyo kituo chake cha kupaki bodaboda. Niliwauliza wenzake, wakanijibu kuwa tangu apeleke abiria jana yake saa 4 usiku, hakurudi tena,” alisema na kuongeza:“Nilirudi nyumbani na kuanza kuwapigia simu baadhi ya ndugu na jamaa lakini sikupata jibu la mahali mume wangu alipo. Baada ya siku mbili nilikwenda Kituo cha Polisi Mtongani, nikakuta pikipiki yake ikiwa imeharibika vibaya kutokana na ajali. 
“Nilipowauliza polisi walisema mwenye pikipiki hawamjui na alipelekwa pale usiku wa siku mbili zilizopita na msamaria mwema akiwa hajitambui, ikabidi wamkimbize Hospitali ya Temeke kwa matibabu.
“Tulipofika Hospitali ya Temeke mapokezi jina lake halikuwepo katika kitabu cha orodha ya wagonjwa waliopokelewa, tulikwenda ICU nako hatukumuona.
“Kesho yake asubuhi, tulilazimika kwenda mochwari ya Hospitali ya Temeke, tukakuta mwili wake kwenye jokofu na kujiridhisha ni wenyewe. Wahudumu wakakiri kwamba ule mwili una siku tatu pale.
“Hatukuwa na cha kufanya zaidi ya kupanga taratibu za mazishi. Tuliwataarifu ndugu, tukapanga tarehe ya mazishi iwe Novemba 27, kaburi likachimbwa.
“Siku ya mazishi, watu walikwenda na gari kufuata mwili hospitali lakini hawakuukuta kwenye jokofu alilokuwa amehifadhiwa. 
“Walipokwenda kuulizia kwa uongozi wa hospitali, wakasema kwanza waende kituo cha polisi wapate askari wa usalama barabarani, wakapime ajali ndipo watapewa mwili.
“Ikabidi waende Kituo cha Polisi Mtongani, wakaambiwa waende Kituo Kikuu cha Mkoa wa Polisi, Temeke, Chang’ombe, pale alipatikana askari wa usalama barabarani, wakaongozana hadi eneo la ajali na kupima na kuchora ajali ilivyokuwa.
“Baada ya mchoro, polisi walitoa kibali cha mazishi. Ndugu walikwenda na kibali kwa uongozi wa hospitali wakaomba wapewe mwili lakini danadana zikaendelea, maana haukuonekana mochwari.
“Wakiwa na sanda mkononi, waliuliza maiti ilipokwenda lakini hawakujibiwa, hakuna aliyekuwa na maelezo ya kueleweka. 
“Ulifanyika msako pale mochwari lakini hakuna kilichopatikana.
“Ikabidi ndugu warudi Kituo cha Polisi Mtongani, wakapewa askari hadi Hospitali ya Temeke. Yule askari alipouliza ndiyo wahudumu pale hospitali wakasema kuna mgonjwa mahututi alihamishiwa Muhimbili pale Moi (Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu).
“Kweli walikwenda Moi, walimkuta mume wangu akiwa ICU anaendelea na matibabu.”
NINI KILIFANYIKA
Mwanjaa alisema, baada ya kumkuta Yahya yupo ICU, hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kurudi nyumbani na kuwataarifu kila kitu ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya mazishi.
“Hakuna aliyeamini haraka, wengine walikwenda mpaka Moi kuhakikisha, waliobaki waliamua kuzika mgomba kwa sababu kimila kaburi halifukiwi bila kitu.
“Japo tulitumia fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi, tuliandaa chakula kingi lakini kimedoda, ila yote kwa yote namshukuru Mungu mume wangu bado mzima.
“Namuomba Mungu amponye mume wangu haraka, arudi nyumbani tuendelee na maisha yetu. Hivi sasa kila mara nipo Moi kwa ajili kuhakikisha anapata huduma kwa ukaribu na anapona haraka,” alisema Mwanjaa.
DADA MTU AZIMIA MARA SABA
Zafarani Msemakweli ambaye ni dada wa Yahya, alizimia mara sita mara ya kwanza alipopewa taarifa ya msiba.
Habari ambazo zimethibitishwa na Zafarani mwenyewe, zinasema kuwa baada ya kupewa taarifa kaka yake yupo hai ICU Moi, alizimia tena, hivyo kufikisha mara saba.
Zafarani alisema: “Nilipopokea taarifa kwamba kaka yangu amekufa niliishiwa nguvu, unajua yule ni tegemeo la familia yetu. Ndugu zangu wanasema nilizimia mara sita.
“Nilipoambiwa ni mzima kwa mshtuko nilizimia tena. Ni maajabu, mtu amehifadhiwa mochwari na madaktari wamethibitisha amekufa baadaye tunaambiwa yupo hai, inashangaza sana.”
UWAZI LAMSHUHUDIA YAHYA ICU
Mwandishi wetu alikwenda Moi kumwangalia Yahya na kujiridhisha kweli yupo hai anaendelea na matibabu.
Jitihada zinaendelea za kumtafuta mganga mkuu wa Hospitali ya Temeke, aseme nini kilitokea kwenye hospitali yake mpaka Yahya akawekwa mochwari na kuwekwa ndani ya jokofu kwa siku tano kisha kupelekwa Moi akiwa mgonjwa mahututi.
Awali mwandishi wetu alikwenda hospitalini hapo na kuomba kuzungumza na mganga mkuu lakini alikosa fursa na kila akipiga simu yake haipatikani.

Chanzo:.globalpublishers

No comments:

Post a Comment