Wednesday, 8 January 2014

Amtoa roho mumewe kisa 25,000

MKAZI wa Kijiji cha Ntewa, Kata ya Ntuntu, Tarafa ya Mungaa, wilayani Ikungi, mkoani Singida, Juma Abdallah (25) amefariki dunia baada ya kupigwa kichwani kwenye paji la uso na mkewe, Veronica Hamis (25) na kufariki dunia papo hapo.
 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa saba mchana katika Kijiji cha Ntewa, Tarafa ya Mungaa, wilayani Ikungi.
Alisema siku ya tukio katika muda huo wa saa saba mchana wana ndoa hao walirejea nyumbani kwao wakitokea kwenye klabu cha pombe za kienyeji aina ya ‘Mtukuru’.
Kwa mujibu wa Kamwela wana ndoa hao vijana  wakiwa nyumbani kwao, Juma alichukua pochi ya mkewe Veronica na kisha kuchukua sh 25,000 zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya pochi hiyo bila idhini ya mkewe huyo.
“Wana ndoa hao vijana wakiwa nyumbani kwao ndipo Juma alipochukua pochi ya mkewe Veronica na kuchukua sh 25,000 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye pochi hiyo bila idhini ya mkewe,” alifafanua Kamanda Kamwela.
Kamanda huyo wa Polisi, alisema baada ya Juma kuchukua fedha hizo bila idhini, mkewe alimsihi sana azirudishe mahali zilipokuwa lakini  mumewe alikataa.
“Hata hivyo Veronica alipoona jitihada za kumtaka mumewe azirejeshe fedha hizo zimeshindikana, ndipo alipowaita wanaume wawili ambao majina yao hayajajulikana, ambao walipofika walimshika Juma, hapo ndipo mwanamke huyo alipopata fursa ya kuchukua kipande cha mti na kumpiga nacho mumewe kwenye paji la uso na kusababisha kifo chake,” alisisitiza Kamwela.
 Alisema baada ya wanaume hao kuona mume wa mwanamke huyo amefariki dunia, walitimua mbio kwenda kusikojulikana.
 Alisema jitihada za kuwasaka wanaume hao zinaendelea wakati mke wa marehemu Veronica tayari anashikiliwa na polisi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment