WAKILI wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Albert Msando na Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana walichuana vikali katika kesi namba 1/2014 iliyofunguliwa na Zito akitaka Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA izuiliwe kujadili uanachama wake hadi atakapopewa fursa ya kujitetea katika Baraza Kuu la chama hicho.
Mawakili wengine waliokuwa wakisaidiana na Lissu katika mnyukano huo wa kisheria, ni PeterKibatala na John Mallya.
Mchuano kati ya mawakili hao ulioanza majira ya saa 5:53 asubuhi na kuisha saa 12:38 jioni ulimlazimisha Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, John Utamwa, kuahirisha kesi namba hiyo hadi Jumatatu ijayo kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Wakati ndani ya mahakama mchuano wa mawakili ukiwa mkali kwa kutetea na kupinga hoja mbalimbali, nje ya ukumbi wa mahakama wafuasi wanaounga mkono uongozi uliopo madarakani na wale wanaomuunga mkono Zitto, nao walikuwa na mabishano makali hali iliyowafikisha katika kurushiana makonde mbele ya askari polisi.
Mbali ya kutoleana maneno makali na kushikana mashati, wafuasi hao walishindana kuonyeshana mabango ya kutetea wanachokiamini katika mgogoro huo kati ya Zitto na uongozi wa CHADEMA.
Katika hoja ya msingi iliyowasilishwa na Zitto kupitia wakili wake Msando mahakamani hapo juzi, anaiomba Mahakama Kuu kuwazuia washitakiwa kwa pamoja ambao ni Kamati Kuu ya CHADEMA au chombo chochote kwa makusudi, kujadili au kuamua suala la uanachama wake.
Maombi mengine ya Zitto ni kutaka apatiwe nakala za uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi hivi karibuni na kumvua uanachama ili aweze kukata rufaa kwa Baraza la Uongozi la CHADEMA.
Katika ombi la tatu, Zitto anaiomba mahakama iwazuie washitakiwa kuingilia kati wajibu na majukumu yake ikiwemo majukumu yake kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kufuatia maombi hayo, CHADEMA kupitia mawakili wake walizipinga hoja hizo na kuiomba mahakama iangalie maslahi ya walio wengi badala ya mtu mmoja.
Katika kutetea hoja zake, Msando alisema kama kamati kuu itaamua kumjadili na kumvua unachama Zitto, watu wa Kigoma Kaskazini watapoteza haki ya kutumikiwa na mtu waliyemtaka.
Msando alisema waliomchagua Zitto katika jimbo lake sio wafuasi wa CHADEMA pekee, bali wa vyama vyote, na kwamba akivuliwa uanachama, atapoteza haki ya kuwa mtumishi wa watu waliomchagua.
Lissu katika kupinga hoja hiyo aliieleza mahakama kuwa CC haiukusema kama inaenda kumvua uongozi, bali lengo ni kujadili uanachama wake hali inayoweza kumfikisha katika hatua ya kumuonya, kumsamehe au kumfukuza moja kwa moja.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na wakili Msando aliyeieleza mahakama kuwa katika barua aliyopewa Zitto ya kutakiwa kujitetea, haikueleza suala la kuonywa au kusamehewa zaidi ya kueleza kuwa atavuliwa uanachama au kufukuzwa kabisa ndani ya chama.
Katika mabishano hayo ya kisheria, Msando aliiomba mahakama isikitambue kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya wateja wake, kwa kile alichoeleza kuwa katika baadhi ya vipengele vya kiapo amekiri kuambiwa baadhi ya mambo pasipo kuyafahamu mwenyewe.
Hoja hiyo ilipingwa vikali na Lissu aliyeieleza mahakama kuwa anashangazwa na hatua ya Msando kutoifahamu katiba ya chama chake licha ya kuwa kiongozi wa CHADEMA.
Lissu alisema kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, mkurugezi yeyote ndani ya chama hicho ni mjumbe wa Kamati Kuu na kwamba Kibatala ni Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa CHADEMA.
Kutokana na hoja hizo Lissu aliiomba mahakama isikubali kupokea maombi ya Zitto kwa kile alichoeleza kuwa hayajakidhi viwango.
Baada ya Jaji Utamwa kupokea hoja za pande zote mbili, aliwaeleza wahusika kuwa uamuzi wa shauri hilo utatolewa Jumatatu na kabla ya kuahirisha, Kibatala aliomba mahakama itoe amri ya mijadala ya kesi hiyo izuiwe katika mitandao ya kijamii.
Katika uamuzi wa ombi hilo, Jaji Utamwa alilitupilia mbali na kueleza kuwa ni ngumu kuzuia mihemko ya watu katika kesi hiyo.
Wafuasi wadundana
Katika hatua nyingine, nje ya mahakama hiyo jana kuligeuka uwanja wa masumbwi baada ya wafuasi wanaounga mkono uongozi wa CHADEMA na wale wanaomuunga mkono Zitto kunyukana na kutambiana kwa mabango.
Wale wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Zitto walikuwa na mabango yaliyosomeka “Zitto kama Mandela”, “Zitto kwanza na chama baadae”, huku wale wanaounga mkono uongozi wa CHADEMA wakiwa na mabango yanayomueleza Zitto kuwa msaliti.
Katika hatua nyingine, licha ya mahakama kuahirisha kutoa uamuzi hadi Jumatatu, CHADEMA imesema kuwa itaendelea kujadili uanachama wa Zitto ndani ya kikao cha CC kinachoendelea.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment