MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Moses Bushamaga ‘Mez B’ usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita alinusurika kuuawa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana maeneo ya Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
Mez B alisema alivamiwa na watu asiowafahamu akiwepo baunsa ambaye alimwelekeza cha kufanya mtu huyo ambaye alimjeruhi vibaya maeneo ya usoni.
“Nilitoka kwa Noorah, nilipofika maeneo ya White Inn – Sinza nikashuka kwenye gari, baada ya hapo nikamuona baunsa anakuja mbele yangu, alikuwa na jamaa mmoja hivi, huyo baunsa akamwambi yule jamaa fanya kazi yako, huyo jamaa akatoa kisu na kuanza kunijeruhi maeneo ya usoni, yaani hapa sitamaniki kabisa lakini nashukuru Mungu bado napumua,” alisema Mez B.
Alisema wakati akifanyiwa unyama huo, walinzi wa hapo walimuangalia tu hawakutoa msaada wa aina yoyote mpaka yule jamaa alipoacha mwenyewe kumfanyia unyama huo.
Mez B ni kati ya wasanii ambao wanatikisa katika muziki wa bongo flava, kutoka kundi la Chamber Squared ambalo lilikuwa likiongozwa na mkali wa ‘free style’, marehemu Albert Mangweha ‘Ngwea’ na msanii Athumani Kapongo ‘Dark Master’.
Msanii huyo alishawahi kutamba na ngoma zake kama ‘Kikukuu cha Mama Rhoda’, ‘Kidela’ na ‘Kama Vipi’ ambao alishirikiana na mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’ kabla hajapotea katika soko la muziki huo.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment