Dar es Salaam.Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ametoa ufafanuzi juu ya uhusiano wake na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Hatua hiyo ya Mkono imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu kuwa aliwahi kumpa Zitto magari mawili.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mkono alisema kuna magari mawili yanayohusishwa na Zitto na kuyataja kuwa ni Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.
“Sijawahi kumpatia Zitto magari, isipokuwa kuhusu hiyo Land Cruiser, nilitoa msaada wa kuwanusuru Zitto na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), kule Tarime kwenye msiba wa marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema), kwani walikuwa wakitishiwa kupigwa.”
Alisema alitoa gari hilo lililokuwa na Bendera ya Bunge liwachukue Mbowe na Zitto na kuwapeleka Mwanza... “Walipofika Mwanza, Zitto aliwasiliana na mimi kuhusu ununuzi wa gari hilo na kupitia wakala wangu nilimuuzia,” alisema Mkono.
“Hata nyaraka za umiliki wa gari hili ninazo mimi mwenyewe kama mmiliki halali. Ninamiliki magari mengi tu hata wewe mwandishi ukitaka Vogue (aina ya gari) nitakukodisha tu,” alisema Mkono.
Alisema wanafahamiana kwa siku nyingi hata kabla ya Zitto kuwa mbunge na kwamba aliwahi kufanya mazoezi kwa vitendo katika ofisi yake (Mkono), alipokuwa mwanafunzi.
Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.
Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto jana kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati tofauti na kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.
Zitto akana
Katika hatua nyingine, Zitto ameitaka Chadema kumwandikia mashtaka mapya yaliyoibuliwa na Lissu ili aweze kujitetea.
“Mashtaka yangu ni yale tu ya waraka na kugombea uenyekiti na shtaka moja la masuala ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kwa kuwa hawakuniandikia mashtaka hayo kinachobakia ni majungu tu, masuala ya kuhongwa magari ni tuhuma zinazorudiwarudiwa bila ushahidi wowote,” alisema na kuongeza:
“Mkono ananihonga ili nimpe nini? Yeye mbunge na mimi ni mbunge pia. Hiyo hongo tunabadilishana na nini? Katika kumaliza Shahada yangu ya Uzamili ya Sheria na Biashara nilifanya `internship’ (mafunzo kwa vitendo) kwa Mkono na hivyo kuna uhusiano wa kikazi wa baba na mtoto.”
Zitto alisema kuwa Mkono ni kama mzee wake na suala la kumpa chochote kile si hoja.
Kitila amruka Slaa
Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo amesema kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa kuwa alikiri kwamba Zitto alikuwa akiujua waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, ni za kutunga.
Juzi, wakati akieleza uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kuwafukuza uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Arusha,Samson Mwigamba na Dk Kitila, Dk Slaa alisema wakati akihojiwa na Kamati Kuu, Dk Kitila alisema Zitto alikuwa akiujua waraka huo.
“Siyo kweli. Hata siku moja sijawahi kukiri kwamba Zitto alikuwa akiufahamu waraka, kilichosemwa na Dk Slaa ni uongo.”
Mwigamba afafanua
Mwigamba alisema hakuhojiwa na Kamati Kuu kwa sababu yeye ni Msabato na Siku ya Sabato, hairuhusiwi kufanya jambo lolote zaidi ya kumwomba Mungu.
“Waliniita Ijumaa (Januari 3) ili nihojiwe lakini mpaka saa 12 jioni sikuwa nimehojiwa na niliwaeleza kuwa jua likizama sitakubali kuhojiwa kwa sababu itakuwa imeanza Siku ya Sabato,” alisema.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kiliendelea Januari 4, mwaka huu, pia hakuweza kwenda kuhojiwa kwa sababu ilikuwa Sabato, pia alikuwa kanisani, “Niliwaambia kuwa nipo tayari kuhojiwa Jumapili, hawakunijulisha kama wameridhia.”
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment