Dar es Salaam. Mwanamke aliyekamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, yupo chini ya ulinzi wa polisi huku akiendelea kutoa pipi za heroin kupitia njia ya haja kubwa.
Hadi kufikia jana mchana alikuwa ametoa pipi 72.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kuhisiwa kumeza kete hizo.
Kamishna wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema mwanamke huyo anaendelea kutoa pipi hizo.
“Anaendelea kutoa kete zaidi na ndiyo maana hatukuweza kusema idadi kamili ya mzigo alioumeza kwa sababu wakati mwingine wanadanganya, hawasemi ukweli kuhusu kiasi cha mzigo walioumeza, wana mbinu nyingi hawa,” alisema Nzowa
Alisema baada ya kushikwa mtuhumiwa aliwaambia polisi kuwa amemeza pipi 61, lakini baadaye alisema amemeza pipi 40.
Alisema ukweli kamili utabainika baada ya upelelezi.
Alisema mtuhumiwa huyo pia amekataa kuwataja watu waliomtuma licha ya kubanwa kwa mbinu zote.
Nzowa pia alisema, watuhumiwa wanaomeza dawa za kulevya huzitoa pipi hizo kwa njia ya haja kubwa ambapo mwili wenyewe kupitia mfumo wake, unazitoa wakati mtu anapokula.
“Hatuwapi kitu chochote cha kuwafanya wazitoe, lakini anapoendelea kukaa, akila chakula basi na zenyewe kupitia mfumo wa mwili hutoka. Ndiyo maana huyu mwanamke mpaka sasa anaendelea kuzitoa taratibu, mpaka zitakapoisha,” alisema.
Nzowa alisema endapo itatokea pipi hizo hazikufungwa vyema zinaweza kupasukia tumboni na aliyemeza kupoteza maisha na kwamba kwa mtuhumiwa jinsi anavyozitoa taratibu upo uwezekano wa kupasuka.
“Ikitokea zikapasuka tumboni mwake hatuna la kufanya kwa sababu jambo hilo lipo kama ambavyo unawasikia vijana wengi wanapoteza maisha kwa njia hiyo,” alisema
Pia Nzowa alizungumzia suala la mwanamke wa Kinigeria, aliyekamatwa JNIA Septemba mwaka jana, akiwa na kete 99 za dawa za kulevya.
Alisema mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani juzi na kusomewa shtaka.
Mwanamke huyo, alikuwa amezihifadhi dawa hizo kwenye chupa ya mafuta ya kupaka na nyingine kwenye kopo la poda za watoto.
Alikuwa mbioni kwenda Roma Italia, kupitia Ufaransa.
Mwanzoni mwa mwaka huu, raia mwingine wa Nigeria, Okwubili Agu, alikamatwa JNIA akiwa na pipi 71 za heroin zenye thamani ya zaidi ya Sh 54 milioni alizokuwa amezimeza tumboni.
Meneja Mkuu wa Usalama wa JNIA , Clemence Jingu alisema kuwa, kukamatwa kwa dawa hizo kunafuatia kufungwa kwa mashine za kisasa za kukagulia mizigo katika uwanja huo.
Alisema mashine hizo zina uwezo mkubwa wa kubaini vitu mbalimbali zikiwemo dawa za kulevya zilizomezwa.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment