Saturday 11 January 2014

Wafuasi Chadema na Zitto waonywa

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imewaonya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kutokana na vurugu zilizotokea Mahakama Kuu Kanda ya Dar esSalaam.

Vurugu hizo zilikuwa baina ya wafuasi wa Zitto ambaye amevuliwa wadhifa wa Unaibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa na wafuasi wa chama hicho ambao wako upande wa uongozi uliomvua madaraka.

Zilitokea Januari 6 na 7, mwaka huu, wakati wa usikilizaji wa kutolewa uamuzi wa kesi ya Zitto dhidi ya chama chake, akiweka pingamizi la Kamati Kuu kumjadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la Chadema.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ilisema vurugu hizo zilichangia uvunjifu wa amani katika maeneo ya Mahakama kiasi cha kulazimika Jeshi la Polisi kuingilia kati.

“Nachukua fursa hii kukemea, vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani uliofanywa na wafuasi wa pande zote mbili katika maeneo ya Mahakama,” taarifa ilisisitiza.
Jaji Mutungi aliwaasa viongozi wa Chadema na Zitto kuwazuia wafuasi wao kujihusisha na vitendo vya vurugu na uvujifu wa amani wa aina yoyote wakati mgogoro baina yao unaendelea. 
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment