Mwingine hupewa sharti hilo na mganga wa kienyeji eti akimuua mtoto na kuchukua baadhi ya viungo vya mwili wake kisha kumpelekea mganga huyo, atapatiwa dawa ya kupata dhahabu nyingi machimboni.
Wapo mabinti zetu wengi ambao wamefanyiwa unyama huo na watu wazima na kibaya zaidi vitendo hivyo kufanyiwa na ama baba mkubwa au baba mdogo. Hivi baba mdogo kumbaka mtoto wa dada yake huyo siyo mwanae? Kwanini baba huyu amfanyie ukatili huu mtoto huyu?
Ipo mifano ya mabinti waliobakwa na jamaa zao wakati wakiwa wadogo miaka kati ya nane na 15 ambao hadi leo jeraha walilopata halijapona. Wapo wenye majeraha sehemu za siri pamoja na sehemu za makalio ambayo yalisababishwa na kubakwa na ama watu wazima wakiwamo baba zao wakubwa au wadogo. Ni jambo la kusikitisha sana.
Yupo binti mmoja niliwahi kusikia simulizi yake ambapo alibakwa na baba mkubwa wake akiwa na umri wa miaka 12 na hadi leo ana tatizo la uvimbe sehemu ya haja kubwa.
Na kibaya zaidi, binti huyu amekuwa akiandamwa na mikosi/ balaa hata anapopata mchumba hujikuta akimfanyia kitendo hicho hicho kama alichomfanya babake mkubwa.
Hii ni nuksi kubwa sana ambayo mtu anaweza kumwachia binti ambaye angekuwa na maisha yake mazuri lakini yakawa yamekatishwa na fedhuli mmoja anayetaka kutajirika haraka kupitia nyota za wengine. Lakini je, mali zinazopatikana na stahili hii zinadumu?
Na watu wenye ibilisi wa ubakaji hutumia mwanya huo pale wazazi wanapokuwa hawapo nyumbani ambapo ndipo hupata upenyo wa kutimiza ukatili huu. Hadi mtu anajiuliza; je, watu wa aina hii wanajua kuwa Mungu anawaona?
Lipo andiko moja katika Biblia Takatifu kuitabu cha Yeremia 23:23 ambayo yanasema; “Mimi ni Mungu aliye karibu, asema Bwana, mimi si Mungu aliye mbali”.
Hivyo wandugu kila tulifanyalo tusijidanganye kuwa hakuna atuonaye. Tena kwa uthibitisho asema kitabu cha Isaya 44:6; Mimi ni wa kwanza na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu hapana Mungu”.
Mungu wetu atenda maajabu lakini haonekani. Ndiyo maana anakujulisha mapema kuwa yeye yuko karibu wala hayuko mbali. Kwa hiyo mtu aweza kufanya jambo akijua ya kuwa haonekani kumbe yuko amuonaye, naye ni Mungu muumba wetu.
Binadamu hujidanyanga kwa kuona vitu vya mwili na nyama vinavyoonekana, anashindwa kuelewa kwamba vya muhimu zaidi ni vile vitu visivyoonekana kwa macho, yaani vile vilivyoko katika ulimwengu wa roho.
Matatizo mengi tunayopata hayakuanzia nje bali ndani kwenye ulimwengu wa roho. Kwa maana hiyo ukitaka kupatia jawabu tatizo lako, lazima uzame kwenye ulimwengu wa roho kuchimbua mzizi wa tatizo ndipo unaweza kuondokana nalo.
Kwa mfano roho ya ubakaji anayokuwa nayo mtu, kibiblia hilo linaitwa ni pando, yaani ni tabia ambayo Mungu hakuruhusu. Angalia andiko hili kwenye Biblia Takatifu kitabu cha Mathayo Mtakatifu 15:13; Yesu akasema; “Kila pando asilopanda Baba yangu wa Mbinguni litang’olewa”.
Ubakaji ni roho ambayo shetani ameipanda ndani ya mtu kutenda uasi. Roho hii yaweza kumtoka mtu atakapoombewa na baba wa kiroho mwenye upako wa kufichua katika makanisa ya kiroho.
Tatizo kubwa ambalo linasababisha roho hizi chafu kuwavamia watu ni kule kuasi kumcha Mungu. Watu wameasi katika kuutafuta uso wa Mungu na hivyo kutoa nafasi kwa shetani kutawala maisha yao. Kama siyo shetani yawezekanaje mtu kumbaka mtoto wa dada yake? Hili ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mpenzi msomaji, tabia hii ni lazima tuikemee kwa nguvu zetu zote. Tena kama ipo adhabu nyingine kali zaidi inayopaswa kupewa watu wenye ufedhuli huu itolewe ili kutomomeza kabisa ukatili dhidi ya watoto wetu.
chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment