Wednesday 16 July 2014

Kafulila atua Takukuru akiwahusisha vigogo sita wa serikali.

HATIMAYE Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulia (NCCR-Mageuzi), amewasilisha ushahidi wake kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu tuhuma za wizi katika akaunti ya Tegeta Escrow alizozitoa bungeni akiwahusisha vigogo sita wa serikali.
Katika ushahidi huo, Kafulila anaeleza sababu zake ni kwanini anataka Bunge lichunguze tuhuma hizo badala ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru.
Kwa mujibu wa barua yake kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na nakala kwa Spika wa Bunge na CAG, Kafulila ametoa maelezo yenye kurasa saba akiambatanisha na vielelezo kadhaa juu ya tuhuma hizo.
“Nikichangia hotuba ya waziri mkuu nilitaka uchunguzi ufanyike kupitia Kamati Teule ya Bunge kuhusu tuhuma zinazohusisha kiasi cha dola 270 milioni zilizopaswa kuwa ndani ya akaunti hiyo sanjari na zile dola 122 milioni zilizokwishatolewa na kupewa Kampuni ya PAP,” inasomeka barua hiyo.
Kafulila alisema Takukuru ni chombo chenye jukumu zito, lakini hakina meno kukabiliana na rushwa zinazowakabili vigogo wa serikali kwani mwamuzi wa mwisho katika masuala hayo huwa ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ambaye amekuwa akitupilia mbali mashitaka kwa kisingizio cha mamlaka aliyonayo kikatiba.
Sababu ya pili kwa mujibu wa barua hiyo ni malalamiko ya Ofisi ya Takukuru yenyewe kusema kuwa Ofisi ya DPP inakwamisha ufanisi wa vita dhidi ya rushwa, ilikuwa ni ushahidi tosha wa yeye kukataa uchunguzi ufanywe na Takukuru.
Sababu ya tatu, Kafulila alinukuu taarifa za wikleaks kuwa rais anakwamisha mambo mengi kuhusu vita dhidi ya ufisadi, huku sababu ya nne ikiwa ni uzoefu kuwa ufisadi huu umekaliwa kimya na Ikulu bila kufanyiwa kazi.
“Unakumbuka Dk. Hosea kuwa taasisi yako katika miaka ya 2000 ukiwa mkurugenzi ulipata kuchunguza kuhusu ufisadi wa mkataba wa IPTL namna ulivyofikiwa kifisadi, lakini pamoja na kufanya kazi hiyo nzuri, Ikulu haikuchukua hatua dhidi ya wahusika na wewe unafahamu kuwa ripoti hiyo ingetosha kuwa ushahidi katika Mahakama ya ISCID kuweza kubatilisha mkataba wenyewe ulionyonya uchumi wa nchi yetu kwa muda mrefu, lakini Ikulu imekaa kimya,” ilisomeka sehemu ya ushahidi.
Gazeti hili liliona maeneo yaliyoainishwa na Kafulila kuashiria kuwa hukumu ya Jaji Utamwa haikuhusu fedha ndani ya Escrow kama Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alivyolieleza Bunge mapema mwaka huu.
CHADEMA waunga mkono
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete aitishe tenda kwa utaratibu wa kimataifa ili kuchunguza fedha zilizokwapuliwa katika akaunti ya Escrow.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha hakuna wizi ili kusafisha taifa na kuachana na tabia ya kugeuka ombaomba.
Alisema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndullu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi waache blabla, waeleze ukweli.
Dk. Slaa alisisitiza kuwa katika suala la fedha za Escrow hawawezi kunyamaza na kuona nchi ikiendelea kuliwa na kuongeza kuwa ingawa Bunge lilitoa agizo kwa CAG na Takukuru kuchunguza suala hilo, hana imani na watu hao.
Alisema kuwa hawana imani na Mkurugenzi Takukuru, Dk. Edward Hoseah kwani taasisi hiyo iliwahi kutumika kusafisha sakata la Richmond.
Pia aliishutumu ofisi ya CAG kuwa nayo ilihusika kumsafisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, katika kashfa ya kugawa fedha kwa wabunge ili waiunge mkono na kupitisha bajeti ya wizara hiyo.


Alisema kuwa fedha hizo ni za serikali ndiyo maana gavana anaandika, na kuongeza kuwa ni wakaguzi wa kimataifa pekee ndio watatoa majibu sahihi ikiwemo lini PAP alinunua Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
chanzo:tzdaima

No comments:

Post a Comment