Tuesday, 18 August 2015

Miezi minne mimi na mke wangu tunalala mzungu wa nne !

 
 

 Hili ni eneo pia nyeti ambalo wengi wetu tunaliona la kawaida, kumbe ndio chimbuko la migogoro mingi inayozibomoa familia zetu ambako ndiko kila mmoja wetu anaanzia maisha.


Anasema, “ Mimi binafsi napenda sana michezo hasa mpira wa miguu. Kila siku huwa namwambia mke wangu kuwa mimi sinywi pombe wala sivuti sigara.

Yaani kwa kifupi sihangaiki  na starehe za dunia zaidi ya mpira wa miguu hasa ligi ya EPL nay a hapa nyumbani VPL.

Tofauti na hapo baada ya kutoka  kazini huwa nacheza na wanangu kwa mu mwingi sana, hali ambayo inanifanya niwepo nyumbani kwa muda  wote hasa wikiendi. Lakini haisaidii chochote.

Leo ni takriban miezi minne sasa ugomvi upo na tunalala mzungu wa nne kitandani, shuka kila mtu lake na mbaya zaidi mpaka sasa zijachukua hatua yoyote ile najaribu kutatua mwenyewe.

Ila sasa nimeshindwa maana wakati mwingine wiki inaisha bila kuongea, kila mtu ataongea na mtoto. Labda nimechoka dada naomba ushauri wako nifanyeje? @kdm wa Kawe Dar ”, anamalizia ujumbe wake.

Mpenzi msomaji, hayo ndiyo yanayomsibu mwenzetu akitaka ushauri. Hebu jipange umpe ushauri atokeje hapo kwenye tatizo hilo linalompasua kichwa.

Ujumbe wake huo aliotuma kupitia simu ya kiganjani, nilijaribu kuchat naye kidogo. Nilimwambia hivi; Huyo anakuonea. Kama ni mke wa ndoa julisha ndugu pande zote wakiwamo washenga wa ndoa aulizwe anataka nini.

Pengine analo jambo nafsini mwake anashindwa kuliweka wazi.  Vinginevyo anaweza kuwa ana pepo linalomsumbua hivyo anahitaji afanyiwe maombi ili kunusuru ndoa yako.

Baada ya ushauri huo, akanijibu kama ifuatavyo; “Asante dada kwa ushauri wako. Ila kama ni hivyo sasa ni mtu wa maombi,  yeye Jumamosi anaenda maombi, Jumapili tunaenda kusali wote, Jumanne na Jumatano yeye anaenda maombi”.

Msomaji wangu, hebu tuitizame familia hii kwa macho mawili tuishauri. Binafsi nataka pia nimuulize ndugu huyu kwamba; kama mkewe ni mtu wa maombi kama alivyoeleza hapo juu, mbona anakuwa kinara wa kuvunja amani ndani ya nyumba yao?

Nilidhani kuwa kama mama kweli ni mcha Mungu wa kweli na anakwenda kwenye maombi ya nguvu mara tatu hivi kwa wiki, hayo anayoeleza mumewe huyu yasingekuwepo.

Maombi yanavunja ngome yoyote iliyosimama mbele ya yule aombaye kwa bidii na kwa imani, akijua kuwa hakuna lisilowezekana mbele za Mungu.

Sioni kwa nini mama anayeomba kwa bidii amtie hofu mumewe kiasi hicho, hata kuruhusu kulala mzungu wa nne huku kila mtu na shuka yake. Huyu ana agenda gani ya siri?

Mume huyu yafaa achunguze kama vituko hivi havikuwepo huko walikotoka, kwanini vimeanza miezi minne anayosema. Hapa dhahiri ajue ibilisi tayari ameanza kuishambulia ndoa yake.

Lazima pia achunguze je, ni kweli siku hizo za maombi mkewe huwa kweli kanisani au anakuwa ‘pembe za chaki’? 

Wengine husingizia hivyo kumbe wamebanisha kwa hawara zao wanaowapepea kwa kipande cha khanga. Upo hapo? Maisha Ndivyo Yalivyo!

Kama nyumbani amani ilikuwepo mwanzoni kisha ghafla ikapotea, ni kwa nini? Lipo tatizo hapo, tena kubwa sana.

Uzoefu unaonyesha kuwa mwanamke au mwanaume akipata hawara nje huanza taratibu kuzira (hupuuza) penzi la nyumbani na kuelekeza nguvu zake huko nje. Matokeo yake maswali mengi yanaanza kujitokeza.

Na zaidi ninachokiona kwenye familia hii ni mwanamke kufikia hatua ya kumuonea mumewe bila sababu ya msingi. Amechukua upole wake akaugeuza silaha ya kumbamiza.

Na kweli silaha hiyo inampiga vilivyo.
Lipo andiko ndani ya Biblia Takatifu linaloonyesha jinsi mtu anawe kuwa mwema lakini mwenzake anamuumiza bila sababu ya msingi.

Zaburi 35:12 Wananilipa mabaya badala ya wema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Andiko hili linafanana na lingine Zaburi 109:5 linasema Wamenichukuza mabaya badala ya wema, Na chuki badala ya upendo wangu.

Naam. Huo ndio ukweli wa maandiko ya Mungu, kwamba unaweza kujitahidi kumfanyia mtu jambo jema lakini yeye anakusaliti.

Kwa hiyo usione ajabu kwa sababu pia imeandikwa na neno la Mungu limehakikishwa, lazima litimie katika maisha yetu ya kila siku.

Baba huyu hakika, anajaribu kuwa karibu na mkewe lakini inashindikana na ndio maana yakamfika kooni akaona kwanini anakufa na kijiba cha roho peke yake pasipo kupata ushauri kwa wengine?

Hatari nyingine ninayoiona hapa ni picha ya maisha wanayowajengea watoto wao. Watoto ni malaika na wanayo macho ya rohoni ya kuona mambo mengi. Kile kinachofanywa na wazazi wao wanakiona.

Naona kabisa kwamba lipo tatizo kati ya baba na mama yao. Wanaona vile wazazi hawa hawaongei, muda mwingi hawapo pamoja, hilo nalo haliwapi afya watoto wao, hata kama ni wadogo.

Watoto hupenda na hufurahi sana wapowaona wazazi wao wakiwa pamoja, wakicheka pamoja na mambo mengine ya ushirikiano.

Lakini wanapoona ukimya mwingi kati ya wazazi hawa, ipo aina ya hofu hujengeka ndani ya watoto hawa.

Wazazi wasipokuwa makini, wanaweza kuwapa watoto malezi ya hovyo kutokana na watoto kuwa na tabia ya kuiga yale wayafanyayo wazazi wao. Maisha Ndivyo Yalivyo.

chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment