KIWEWE: Aliyepata umaarufu kwa kuvunja watu mbavu,
SANAA ya vichekesho kwa hapa nchini imekuwa ikishika kasi kila kukicha kiasi cha kuweza kuliteka soko la filamu katika siku za hivi karibuni.
Kama hiyo haitoshi, sanaa hiyo imeweza kuwanufaisha wengi ikiwemo baadhi yao kuajiriwa, huku wengine wakiweza kuishi maisha mazuri.
Robert Augustino Mbumira, maarufu kama Kiwewe ni mmoja kati ya wasanii ambaye ameweza kujipatia umaarufu mkubwa kupitia sanaa hiyo ya vichekesho hapa nchini.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, Kiwewe anasema anamshukuru Mungu kwa kuweza kupata ajira kupitia kipaji chake, kwani kwa sasa ni muajiriwa katika kituo cha televisheni cha EATV akifanya kazi katika kundi la Ze Comedy Show linalorusha michezo yake katika kituo hicho.
Anasema yeye pamoja na wenzake; Bambo, Mtanga, Master Face, Masawe Mtata na Dokta Rushwa walipata ajira hiyo baada ya kushinda katika shindano la Ze Comedy Search lililoandaliwa na kituo hicho, likiwa na lengo la kuwapata wasanii watakaoziba nafasi iliyoachwa wazi na wasanii wengine waliohamishia kazi zao katika televisheni ya taifa ya TBC1.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata ajira kupitia kipaji changu kwani nilisota sana katika kupata mafanikio katika tasnia hii, kweli Mungu ni mkubwa,” anasema.
Kiwewe anaongeza kuwa pamoja na ajira hiyo, pia mwajiri wao amewapa fursa ya kwenda kujiendeleza kimasomo katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment