Monday, 9 April 2012

LULU AELEZA KILICHOTOKEA!!!!!!!


ELIZABETH Michael ‘Lulu’ anayeshikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na kifo cha msanii nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba, ameanika kilichotokea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa, katika mahojiano, Lulu alisema kwamba alimuona Kanumba akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini.
Kamanda huyo alisema kuwa, tukio hilo lilitokea baada ya ugomvi uliotokea kati yake na Kanumba.
Alisema kabla ya ugomvi huo, kutokea kati yao wakiwa chumbani, simu ya Lulu iliita na akaamua kutoka nje kupokea kitendo kilichomuudhi Kanumba.
Kenyela alisema Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti akitaka aelezwe kwanini alitoka nje kupokea simu, akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.
Aliongeza baada ya Lulu kuona Kanumba akimfuata, aliamua kukimbia kutoka nje ya geti, lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba alimkamata na kumrudisha ndani.
Kamanda Kenyela, alisema Kanumba akiwa amemshikilia Lulu, waliingia wote chumbani na kufunga mlango. 
Hata hivyo, alisema haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu anadai kuwa Kanumba ndiye aliufunga. 
Kamanda huyo alisema, Lulu anaeleza ya kwamba, baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, taarifa ya uchunguzi wa awali ilisema kuwa, mbali na maelezo ya mdogo wa marehemu, Seth Bosco (24), pia panga, pombe aina ya ‘whisky’ ikiwa robo glasi na soda aina ya sprite vilionekana chumbani kwake.
Kamanda Kenyela alisema kuwa vinywaji hivyo vitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo na uchunguzi zaidi.
Alipoulizwa kama marehemu Kanumba alikuwa amekunywa pombe siku hiyo, Kamanda Kenyela alisema ni vigumu kubaini hilo ila ukweli wake utajulikana kwenye uchunguzi wa mwili wake (postmortem). 
Akifafanua zaidi kuhusu chanzo cha kifo cha Kanumba, Kamanda Kenyela alisema kwa mujibu wa mdogo wake, Bosco, ambaye pia ni msanii wa kikundi cha The Great Filamu Production, siku ya tukio aliambiwa na kaka yake kuwa ajiandae ili amsindikize sehemu.
Alisema kuwa baada ya kumweleza hivyo, Kanumba aliingia chumbani kwake kujiandaa na kwamba baada ya muda kidogo alimwita mdogo wake chumbani kuwa kuna mgeni, ndipo Bosco akamwambia akiwa tayari angemuona.
Kamanda alisema kuwa muda mfupi baadaye Bosco anasema alisikia kelele ambapo kaka yake alikuwa akimtuhumu mpenzi wake Lulu.
Kenyela alisema kuwa Bosco alieleza kwamba alisikia sauti ya Kanumba akimhoji Lulu: “Kwa nini unawapigia simu mabwana zako wengine?”
Ghafla Bosco aliitwa na msichana huyo na kumuambia kuwa akamwangalie kaka yake amezidiwa.
Bosco alieleza kuwa aliingia chumbani na kumkuta Kanumba amelala sakafuni huku akitokwa na povu mdomoni akiwa haongei.
Alisema kuwa alitoka nje na kumwangalia Lulu, lakini hakumuona na hivyo kuamua kumpigia simu daktari wa Kanumba ambaye baada ya kufika aligundua kuwa amekwishafariki.
Kenyela aliongeza kuwa mwili wa marehemu Kanumba haukukutwa na jeraha lolote na kwamba umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku Lulu ambaye ni mkazi wa Tabata Relini akiendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
 “Uchunguzi ukikamilika tutampeleka Lulu mahakamani kwa tuhuma za mauaji,” 
aliongeza Kenyela.

No comments:

Post a Comment