Rais Jakaya Kikwete, jana alizindua rasmi ujenzi wa daraja la Kigamboni utakaogharimu Sh. bilioni 214.6 na kusema madai yaliyotolewa dhidi yake kwamba, amemuuzia kinyemela Rais mstaafu wa Marekani, George Bush, eneo la Kigamboni, ni uwongo uliopikwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau, daraja hilo litakalokuwa na urefu wa mita 680, litaunganisha maeneo ya Kurasini na Kigamboni na litakuwa na barabara sita; tatu zikiwa ni za kwenda na tatu kurudi na pia litakuwa na nafasi kwa ajili ya watembea kwa miguu.
Uzinduzi wa daraja hilo ulihudhuriwa na baadhi ya mawaziri, Balozi wa Misri nchini, Hosam Mohram, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, wakuu wa wilaya, mameya wa halmashauri za manispaa, jiji, wabunge na madiwani wa mkoa wa huo, makatibu wakuu na wataalam wa wizara, viongozi wa dini, vyama vya siasa na baadhi ya wakazi wa Jiji.
“Kuna uwongo mwingi uliwahi kusemwa kwamba, eti Kigamboni nimemuuzia George Bush. George Bush anatafuta nini huku? Wale ni matajiri wa mafuta. Sasa Kigamboni anakuja kufanya nini? Kuna watu wana viwanda vya kupika uwongo,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kinyume cha madai hayo ya uwongo, mpango wa serikali ni kuifanya Kigamboni kuwa mji mpya na wa aina yake.
Kutokana na hilo, amewataka wakazi wa Kigamboni watakaohamishwa kupisha ujenzi wa mji huo juu ya stahiki zao, akisema wote watalipwa na kwamba hakuna atakayedhulumiwa, kwa kuwa serikali inajali haki za wananchi.
Rais Kikwete alisema Dar es Salaam ilivyo hivi sasa, hakuna kitu cha kuvutia kinachowafanya watu waende kuona au kukaa.
Badala yake, alisema hata watalii wamekuwa wakilitumia jiji hilo kama njia tu ya kupita kwenda katika miji mingine, kama vile Zanzibar, ili kuburudika na vivutio visiwani humo.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imeanza kuzungumza na baadhi ya mashirika makubwa yenye vitu vya kuvutia, ambavyo alisema vitasaidia mji wa Kigamboni kukaa watu 450,000.
Alisema kwa sasa mji huo una wakazi wanaokadiriwa kuwa 45,000.
Alisema pamoja na mipango mizuri ya serikali ya kuliboresha Jiji la Dar es Salaam, kuna baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya nchi.
Rais Kikwete alisema watu hao inawauma sana kuona hatua iliyofikiwa na serikali kujenga daraja hilo na kuwataka waweke mbele maslahi ya nchi.
Aliungana na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuusifu uongozi wa NSSF chini ya Mkurugenzi Mkuu wake, Dk. Dau, kwa maamuzi mazuri ya kutumia asilimia 60 ya fedha zake (NSSF) kugharimia ujenzi wa daraja hilo.
Hata hivyo, Waziri Magufuli alisema pamoja na maamuzi na kazi nzuri iliyofanywa na NSSF, hajaona serikali ikimpa Dk. Dau nishani ya utumishi uliotukuka, badala yake ni wanajeshi tu ndiyo hupewa tuzo hiyo wanapofanya vizuri.
Waziri Magufuli alisema mara baada ya kukamilika, ni watembea kwa miguu na baiskeli tu ndiyo ambao hawatalipia matumizi ya daraja hilo, lakini magari yatalipa. Malipo hayo ni kwa ajili ya kugharimia uendeshaji wa daraja.
Hata hivyo, alisema watembea kwa miguu watatakiwa kupita na kwamba wale watakaogeuza daraja hilo kuwa sehemu ya kukaa kama inavyofanyika katika daraja la Manzese, watalipa.
Alisema fedha za kuwalipa fidia wamiliki ambao nyumba zao zitafuatwa na barabara za mradi wa ujenzi wa daraja hilo, zimekwishatengwa.
Hivyo, amewataka wakazi wa Kigamboni kutoanza kujenga kwani uthamini umekwishafanyika.
Alisema kila mtu atalipwa kulingana na thamani ya ardhi anayomiliki.
Hata hivyo, alisema watakaojenga sasa zinakopita barabara za mradi huo, wajiandae kuondoka bila kulipwa fidia.
Alisema mradi wa daraja hilo unatarajiwa kukamilika ama mwishoni mwa mwaka 2014 au mwanzoni mwa mwaka 2015.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alisema mradi huo unatarajia kutengeneza ajira 3,000 zitakazohusu vijana na wataalam wa ngazi mbalimbali.
Kutokana na hilo, aliwataka vijana kuchangamkia ajira hizo ikiwa ni pamoja na kuwa waaminifu wakati ujenzi wa daraja unaendelea.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Dau alisema wamekubaliana na serikali kwamba asilimia 60 zigharimiwe na NSSF kwa ujenzi wa daraja hilo na asilimia 40 zilizobaki zigharimiwe na serikali kulipa fidia watu watakaohamishwa kupisha mradi huo.
Alisema kwa mujibu wa mkataba kati yao na mkandarasi, ujenzi wa daraja hilo utakamilika ndani ya miaka mitatu, lakini akasema mkandarasi ameahidi kuwa atajitahidi kukamilisha ndani ya miaka miwili na nusu kuanzia sasa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, pamoja na mambo mengine, alisema daraja hilo litasaidia kumaliza tatizo la usafiri hasa kwa wakazi wa Kigamboni.
Alisema kwa sasa wakazi hao hulazimika kutumia kivuko na mitumbwi au njia ya mzunguko yenye urefu wa kilomita 52 kwenda na kurudi Kigamboni.
chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment