Moto umezidi kuwaka Zanzibar baada ya Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni watu 12 kufuatia vurugu zilizotokea katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu juzi, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Mtoni (CUF), Faki Haji Makame.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema mbunge huyo alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi Bububu kwa kosa la kupigana hadharani.
“Mbunge wa Mtoni na wezake watatu, wamekamatwa kwa kupigana hadharani huko Bububu na watafikishwa mahakamni baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Kamishina huyo.
Alisema kwa mujibu wa sheria, kupigana hadharani ni kosa la jinai na mbunge huyo na wezake watafunguliwa mashitaka.
Hata hivyo, alisema watu wanne waliachiwa kwa dhamana, akiwemo Mbunge huyo huku watu wanane wakiendelea kushikiliwa katika kituo cha Polisi cha Bububu.
Alisema kati ya watu hao, mmoja alikamatwa akiwa na kisu katika kituo cha wapiga kura na mwingine alikamatwa akiwa na kitambulisho cha mpigakura cha mtu mwingine.
Aidha, alisema watuhumiwa wengine walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya makosa ya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi huo.
POLISI: HATUKUHUSIKA
Kamishna huyo alisema hakuna tukio la vurugu lililotokea katika vituo vya kupigia kura au watu kujeruhiwa na askari wa Jeshi la Polisi.
Alisema Jeshi la Polisi halikutumia mabomu wala risasi za moto baada ya kutokea vurugu nje ya vituo vya kupigia kura.
Kuhusu watu waliokuwa wakifyatua risasi wakiwa wameficha nyuso zao, Kamishna Mussa alisema: “Siwezi kujibu swali hilo kwa sababu polisi hatuhusiki na matukio hayo.”
MBUNGE ANENA
Hata hivyo, Mbunge wa Mtoni, Faki Haji Makame, alikanusha madai kuwa alipigana hadharani.
Alisema juzi saa 3:45 asubuhi wakati akienda kuwasalimia wakwe zake akitembea kwa miguu, alipofika katika kichochoro kimoja eneo la Bububu, alivamiwa na vijana watatu na kuanza kumpiga.
Alisema kabla ya kuanza kumpiga, vijana hao walimhoji kama ni mwanachama wa CUF na kukagua kofia yake. Alisema aliamua kukimbia, lakini baada ya kufika barabarani kiatu kimoja kilimvuka.
Alisema kabla ya kuokota kiatu hicho, vijana hao walimkamata na kuanza kumpiga kwa kutumia mipira maalam na kwa ngumi na mateke.
Alisema tukio hilo lilitokea mita 100 kutoka kituo cha Polisi cha Bububu.
Hata hivyo, alisema askari wawili walifika na kumuokoa na kuwakamata vijana hao.
Aidha, alisema kabla ya kutokea tukio hilo, alikutana na kiongozi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika tawi la Bububu na kuamua kumsalimia, lakini aligoma kupokea salamu yake.
Alisema kiongozi huyo wa CCM alianza kumtolea malalamiko kuwa wanachama wengi wa CCM wamekuwa wakizuiwa kwenda kupiga kura na wanachama wa CUF na kumuonya kuwa chama chake hakitakubali wanachama wake kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo.
Alisema baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Bububu, alipatiwa fomu ya matibabu (PF3) na kuchukuliwa maelezo yake.
ZEC: UCHAGUZI ULIKUWA HURU NA HAKI
Wakati huo huo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesema uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu ulikuwa huru na wa haki.
Aidha, ZEC imesema haihusiki na vurugu zilizotokea mita 200 kutoka katika vituo vya kupigia kura.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi Unguja, Sululu Rashid Ali, alipokuwa akizungumza na NIPASHE kufuatia vurugu za juzi.
Alisema watu wote waliofika katika vituo na kuwa na sifa ya mpiga kura, ZEC ilihakikisha wanapata haki yao ya Kikatiba ya kupiga kura.
“Vurugu zilitokea umbali wa mita 200 kutoka vituo vya wapiga kura, lakini vituo vyote hali ilikuwa shwari,” alisema Sululu.
Alisema vurugu zilisababishwa na makundi ya watu waliokuwa wakizuia watu waliokuwa wamepakiwa kwenye magari kwenda kupiga kura katika vituo.
Alisema katika kila chumba cha kupigia kura, kulikuwa na mawakala tisa wa vyama vya siasa na makarani wa uchaguzi na hakukuwa na sababu watu kuzuiwa kwenda katika vituo vya wapiga kura wakiwa wamepakiwa kwenye magari.
Alisema pamoja na kuwa na mawakala tisa, pia walikuwapo maafisa wa uchaguzi pamoja na orodha ya majina ya wapiga kura na picha, hivyo isingekuwa rahisi wapiga kura mamluki kushiriki kupiga kura.
“Kwa mujibu wa sheria, hakuna mwananchi mwenye haki ya kumzuia mwananchi mwezake kwenda kupiga kura wakati si afisa uchaguzi au wakala wa chama,” alifafanua Sululu.
Alisema wagombea watatu tu ndiyo walisaini fomu za matokeo kutoka vyama vya CCM, Jahazi Asilia na AFP kati ya wagombea watano waliokuwepo wakati wa kutangaza matokeo hayo.
Alisema wagombea wa vyama vya CUF na ADC, waligoma kusaini fomu za matokeo ya uchaguzi huo, lakini alisema suala la kusaini fomu ya matokeo ni jambo la hiari kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi.
MGOMBEA WA CUF KUPINGA MATOKEO LEO
Mgombea wa CUF, Issa Khamis Issa, alisema anatarajia kufungua kesi leo katika Mahakama Kuu ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Alidai kwamba hakuwa uchaguzi wa wananchi, bali ulikuwa wa askari wa vikosi vya SMZ na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walisadia watu wasio na sifa kupiga kura.
Issa alidai kuwa askari hao walitumia nguvu kubwa, ikiwemo kutoa vitisho kwa kupiga risasi hewani na kusababisha watu kukimbia hovyo na wengine kushindwa kujitokeza kwenye uchaguzi huo.
Alisema askari waliokuwa wakitawanya watu kwa kupiga risasi hewani, walificha nyuso zao kwa kutumia vitambaa wakiwa na nguo za kiraia bila ya kuchukuliwa hatua.
Alidai kuwa vitendo hivyo vimesababisha hofu kwa wananchi na wengine kushindwa kujitokeza kwenye uchaguzi huo.
Alisema ZEC hawawezi kukwepa kuhusika na vurugu hizo kwa sababu kwa mujibu wa sheria, Jeshi la Polisi ndilo lenye dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao, lakini waliachia askari wa vikosi vya SMZ kufanya kazi hiyo.
“Nimepata ushaidi wa kutosha ZEC walivyosadia kuvuruga uchaguzi, kwa sasa siwezi kusema hadharani kwa sababu ni ushahidi muhimu katika kesi yangu,” alisema Issa.
Katika tukio lingine, CUF kimeadi kuwa kijana mmoja alipigwa risasi na kulazimika kufanyiwa upasuaji katika sehemu ya paja lake la kulia.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdallah, alidai kuwa kijana huyo, Juma Mohamed Mmaga, alipigwa risasi na watu waliokuwa wameficha sura zao kwa kutumia vitambaa.
Alidai kuwa kijana huyo anaendelea kutibiwa katika Hospitali ya Al-Rahma Kilimani mkoa wa Mjini Magharibi.
MWANDISHI WA CHANNEL TEN ATIBIWA
Katika tukio lingine, mwandishi wa habari wa Channel 10 Zanzibar, Munir Zacharia, amepatiwa fomu maalum ya matibabu (PF3) na kutibiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Munir alivamiwa na kundi la watu waliokuwa nje ya tawi la CCM Kibweni wakati akipiga picha ya watu waliokuwa wakivunja vioo vya gari kwa kutumia mawe.
Akizungumza na NIPASHE, alisema tukio la kushambuliwa na kuporwa pochi, kuharibiwa kamera na kupigwa aliripoti katika kituo cha Polisi Mwembe Madema juzi.
Munir alisema watu waliompiga anawafahamu kwa majina na kazi wanazofanya na anatumaini kwamba sheria itafuata mkondo wake.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment