Uchunguzi wa mauaji ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, umeingia katika hatua mpya, baada ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuingilia kati kuchunguza ili kujua kama kuna mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika mauaji hayo.
Hatua hiyo imechukuliwa na Tume hiyo baada ya kamati pamoja na timu tofauti, ikiwamo ile inayoongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kuendelea na uchunguzi kufuatia mauaji hayo.
Timu nyingine inayofanya uchunguzi ni ile iliyoundwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pamoja na kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Amiri Manento, alithibitisha Tume yake kuanza kuchunguza mambo hayo alipozungumza na NIPASHE jana.
Alisema uchunguzi huo unafanywa na Tume yake kutekeleza moja ya majukumu yake iliyopewa na Ibara ya 130 Kifungu cha 1 Sehemu (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
“Ndiyo, tunachunguza. Tunaendelea vizuri. Tutatoa taarifa. Katiba inatupa madaraka hayo katika Ibara ya 130 Sehemu C,” alisema Jaji Manento alipokuwa akijibu maswali ya NIPASHE kuhusiana na Tume yake kufanya uchunguzi huo.
Sehemu hiyo ya Katiba ya nchi inaeleza jukumu la Tume hiyo kuwa ni: “Kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Uchunguzi huru wa NIPASHE umegundua kuwa timu ya Tume hiyo iliyokwenda Iringa inawajumuisha wajumbe watatu wakiongozwa na Kamishna Benadetta Gambishi. Wengina ni maofisa wa Tume hiyo, Yohana Mcharo na Gabriel Rubyagila.
Uchunguzi wa Tume hiyo unafanyika baada ya MCT kwa kushirikiana na TEF kuunda timu ya waandishi watatu Septemba 3, mwaka huu, kuchunguza kifo hicho.
Timu hiyo inaongozwa na Meneja wa Utafiti na Machapisho wa MCT, John Mirenyi. Wajumbe wengine ni Mhariri wa masuala ya Siasa wa gazeti la Mwananchi, Hawra Shamte na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Simon Berege.
Timu hiyo, ambayo ilipewa siku nane, ilitarajiwa kuanza rasmi kazi yake Septemba 5, mwaka huu, taarifa ya uchunguzi wake itakabidhiwa kwenye bodi ya MCT.
Pia Septemba 4, mwaka huu, Waziri Nchimbi, aliunda kamati inayohusisha wajumbe kutoka tasnia za sheria, habari, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi nia ya kuunda kamati hiyo ni kupata matokeo yasiyoegemea upande wowote kwa kuwa ni kamati huru.
Kamati hiyo inaongozwa Jaji Mstaafu Stephen Ihema. Wajumbe ni Theophil Makunga kutoka TEF, ambaye pia ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited; Ofisa Mipango wa MCT, Pili Mtambalike; mtaalamu wa milipuko kutoka JWTZ, Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu.
Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita na itafanya kazi kwa siku 30 kuanzia Septemba 5.
Hadidu hizo ni kuchunguza chanzo cha kifo cha Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya waandishi wa Iringa na Polisi, kama kuna orodha ya waandishi watatu waliopangwa kushughulikiwa na polisi mkoani humo.
Hadidu rejea nyingine ni kama kuna taratibu za kukata rufaa ya vyama vya siasa dhidi ya polisi pindi mikutano yao inapozuiwa, je, kuna tatizo la mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa kwa ujumla wake na kama ukubwa wa nguvu zilizotumika katika tukio la Iringa ni sahihi.
Waziri Nchimbi alikaririwa akisema kuwa kuna maneno mengi yanayozungumzwa kuhusu kuuawa kwa mwandishi huyo, hivyo matokeo ya uchunguzi wa kamati yataweka wazi uhalisia wa mauaji hayo. Kamati hiyo imekwisha kuanza kazi.
Juzi Waziri Nchimbi alithibitisha kukabidhiwa taarifa ya awali ya uchunguzi wa polisi juu ya mauaji ya Mwangosi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri Nchimbi alisema uchunguzi huo wa awali ulibaini mambo makubwa mawili; la kwanza likieleza kuwa mlipuko uliotokea uliotokana na bomu na la pili, bomu hilo lilifyatuliwa na askari huyo.
Katika taarifa hiyo ambayo Waziri Nchimbi iliisaini alisema kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka kwa IGP Mwema, alimweleza Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi kuwa aipeleke kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili afanye uamuzi wa kisheria juu ya uchunguzi huo.
Alisema juzi mwendesha mashtaka alikamilisha kulisoma jalada la uchunguzi huo na kuandaa mashtaka dhidi ya askari huyo.
Waziri Nchimbi alisema juzi hiyo hiyo aliliagiza Jeshi la Polisi kumpeleka mahakamani kama ilivyotakiwa na DPP.
Hata hivyo, alisema kamati aliyoiunda chini ya Jaji Ihema itaendelea na kazi yake ili kupata suluhisho la kudumu la migongano ya kikazi kati ya polisi na waandishi wa habari na polisi na vyama vya siasa na kuboresha uhusiano kati ya polisi na raia.
“Wakati mkondo wa sheria umeanza kufuatwa, nawaomba wadau wote kutoa nafasi kwa utaratibu huo wa kisheria kufanya kazi. Wizara yangu na mimi mwenywe tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika jitihada za kujenga taifa bora,” alisema Dk. Nchimbi.
Mwangosi aliuawa akiwa kazini baada ya kupigwa na bomu lililosambaratisha sehemu kubwa ya mwili wake.
Alikumbwa na mkasa huo wakati polisi wakiwatawanya viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kuwazuia wasifungue tawi la chama hicho katika Kata ya Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Mauaji ya mwandishi huyo yalilaaniwa vikali na makundi kadhaa ya jamii, ambao walitaka uchunguzi huru ufanyike kubainisha hasa chanzo cha kadhia hiyo.
Wakati sauti hizo zikipazwa, waandishi wa habari karibu nchini kote, Septemba 12 na 13, mwaka huu, walifanya maandamano makubwa ya kimya kimya kulaani mauaji ya mwenzao.
Pamoja na mambo mengine, waandishi walilitaka jeshi hilo lirejeshe vitendea kazi vilivyokuwa vikimilikiwa na Mwangosi, ikiwamo kamera, kompyuta (laptop) pamoja na simu ya mkononi, alivyokuwa navyo wakati akiwa mikononi mwa askari polisi zaidi ya wanane kabla ya kuuawa.
Kadhalika, IGP Mwema, pamoja na maofisa wengine waandamizi wa jeshi hilo, walikutana na viongozi wa Chadema na kuzungumzia hali ya baadaye baada ya kutokea kwa mauaji hayo.
Juzi askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya Mwangosi, alifikishwa mahakamani kwa shitaka la mauaji.
Askari huyo mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simon (23), mkazi wa FFU Manispaa ya Iringa, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi ya Wilaya ya Iringa akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mwandishi huyo wa habari.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment