Monday, 5 November 2012

LORD EYEZ ALIVYOPANDISHWA KIZIMBANI!!


MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini kutoka Kundi la Nako 2 Nako Soldiers, Isaac Waziri Makuto ‘Lord Eyez’ (pichani), Ijumaa iliyopita alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kusomewa mashitaka sita ya wizi wa vitu mbalimbali yanayomkabili.
Lord Eyez aliyekuwa na uso wa aibu, akijiziba sura kwa viganja vya mikono yake kukwepa kamera, alipandishwa kizimbani mishale ya saa 5 asubuhi na kuanza kusomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mfawidhi, Betty Mark.
Akisoma mashitaka yaliyokuwa yanamkabili mbele ya Hakimu Betty, karani wa mahakama hiyo, Sharifa Dunia aliiambia mahakama kuwa mnamo Septemba Mosi, 2012, saa 4 asubuhi, maeneo ya Kinondoni Shamba jijini Dar, mshtakiwa alimuibia Richard Mrema, ‘control box’ ya gari aina ya Toyota Colora yenye namba za usajili T 671 APK.
Karani huyo alimsomea mashitaka mengine na kuieleza mahakama kuwa mnamo Septemba 17, mwaka huu, maeneo ya Changanyikeni, Wilaya ya Kinondoni, Dar, mshtakiwa pia aliiba ‘power window’ nne za gari aina ya Toyota Escudo yenye namba za usajili T 675 ATS, mali ya Eliasgar Javiwalla.
Baada ya kuchomolewa kwenye kizimba cha kwanza, Lord Eyez alipelekwa kwa hakimu wa pili, Marko Mochiwa ambako nako alisomewa kesi nyingine iliyokuwa inamkabili ya wizi wa redio na amplifaya za gari lenye namba za usajili T 141 ANM, mali ya Emmanuel Lazaro.
Lord Eyez alipelekwa tena kwa hakimu wa tatu, Anipha Mwingira ambapo alisomewa mashitaka mengine yaliyokuwa yanamkabili; wizi wa laptop, simu aina ya Blackberry na kamera ndani ya gari lenye namba za usajili T 334 AVC mali ya Davies Temple, wizi wa simu aina ya Sumsung na upande wa khanga, mali ya Esther Joseph.   
Msanii huyo ambaye aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’, alikana mashitaka yote yaliyokuwa yanamkabili ambapo kesi zake ziliahirishwa hadi Novemba 15, mwaka huu zitakaposomwa tena ndani ya mahakama hiyo. 
Mpaka mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio, ndugu wa Lord Eyez walikuwa wakihangaika kumuwekea dhamana ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika.
Chanzo:globalpublishers

No comments:

Post a Comment