Tuesday 6 November 2012

WATUHUMIWA WENGINE WA MAUAJI YA KAMANDA BARLOW WAKAMATWA!! !!!


Jeshi la Polisi limewanasa watuhumiwa wengine wawili waliokuwa wakisakwa kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Oktoba 13 mwaka huu katika eneo la Minazi Mitatu, Kata ya Kitangiri jijini hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, aliwataja watuhumiwa hao waliokamatwa jana katika maeneo tofauti ya Mji Mwema na Kilimahewa kuwa ni Abdurahman Athumani (28), mkazi wa Mji Mwema na Abdalah Petro “Ndayi” (32), mkazi wa Mtaa wa Mkudi Mwanza.
Sambamba na watuhumiwa hao, alisema kwamba Jeshi hilo pia lilikamata simu ya upepo (radio call) aliyokuwa nayo Kamanda Barlow pamoja na ufunguo wa gari aliyokuwa akiitumia kabla ya kuuawa.
Alisema vitu hivyo vilikutwa vikiwa vimetupwa kwenye shimo la maji taka (septic tank) katika nyumba moja iliyopo maeneo ya Nyanshana jijini Mwanza.
Aidha, alisema Jeshi hilo limemkamata mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Rioba Matiku au “Mama Nyangi”, mkazi wa Nyakabungo Miembeni jijini hapa ambaye anadaiwa kuhifadhi kundi la majambazi wakiwemo wanaodaiwa kumuua Kamanda Barlow.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunafanya jumla ya waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya Kamanda Barlow kufikia wanane.
Habari zilizopatikana awali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilisema kwamba mtuhumiwa Abdallah Petro anadaiwa alikuwepo kwenye uwanja wa Nyamagana wakati wakazi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani walipokuwa wakiuaga mwili wa Kamanda Barlow.
Kwa mujibu wa habari hizo, kuanzia wakati huo, Makachero wa Jeshi la Polisi walianza kumfuatilia kwa karibu Abdallah hadi walipomtia mbaroni jana.
Aidha, habari hizo zimeeleza kuwa mtuhumiwa Abdalah ni ndugu yake na mtuhumiwa namba moja, Muganyizi Michael ambaye anadaiwa kukiri kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi Kamanda Barlow. Yeye na wenzake wanne waliokamatwa wiki mbili zilizopita tayari wamefikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la mauaji.
Kaimu Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Mwanza, alisema baada ya kuhojiwa, watuhumiwa hao wawili walikiri kushiriki katika tukio la mauaji ya Kamanda Barlow na kwamba walidai siku hiyo walikuwa na teksi ambayo ilikuwa ikiendeshwa na mtuhumiwa namba moja Muganyizi.
Alibainisha kuwa watuhumiwa hao walikiri kwamba baada ya kumuua Kamanda Barlow, pamoja na vitu vingine waliondoka pia na “radio call” na ufunguo wa gari, vitu ambavyo Muganyizi alishauri vikatupwe kwenye shimo la maji taka ili kupoteza ushahidi.
“Baada ya kuwahoji watuhumiwa walikiri kuhusika katika mauaji ya Kamanda Barlow, na walikubali kwenda kuonyesha mahali walikotupa radio call na ufunguo wa gari, na kweli maofisa wetu walipokwenda walifanikiwa kuvikuta kwenye shimo la maji taka katika nyumba moja huko Nyanshana,” alisema Matola.
Aliongeza kwamba hatua hiyo iliwawezesha maofisa wa Jeshi hilo kwenda kufanya upekuzi katika makazi ya watuhumiwa hao na kufanikiwa kukuta vitu mbalimbali vinavyosadikiwa kuwa vya wizi zikiwamo sare za Polisi na za kampuni mbalimbali za ulinzi.
Miongoni mwa sare hizo za polisi ni pamoja na kofia (crown), mashati na suruali zinazofanana na sare za mgambo wa Jiji la Mwanza na kuwa suruali moja ilikutwa ikiwa na matone ya damu.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, watuhumiwa hao pia walikutwa na simu kadhaa na line (simcard) takribani nane za mitandao mbalimbali, tv, deck, radio kaseti (subwoofer) na vifaa vinavyotumika kuvunja nyumba kama vile vipande vya nondo, bisibisi na mtalimbo mmoja.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment