Saturday, 5 January 2013

Dk. Ulimboka awagonganisha polisi



NI wazi sasa sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, huenda likawa limefifia bila Jeshi la Polisi kulifanyia kazi kwa kina ikiwemo kumhoji majeruhi huyo.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26 mwaka jana, na kuteswa, kuumizwa vibaya ikiwa ni pamoja na kung’olewa kucha na meno kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wasiojulikana zikiwa ni siku chache tangu kuanza kwa mgomo wa madaktari.
Hata hivyo, kutokana na utata wa tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam chini ya Kamanda wake, Suleiman Kova, liliunda tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi ili kuchunguza sakata hilo lilikokuwa likihusishwa na serikali.
Hatua hiyo ilikuja kutokana na Dk. Ulimboka kuwataja baadhi ya watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini mpaka sasa licha ya mtu mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi, kufikishwa mahakamani akituhumiwa kuhusika na tukio hilo, watuhumiwa wengine hawajawahi kuhojiwa.

Tume hiyo hata hivyo, haikuwahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajawahi kuhojiwa huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, jana limekanusha kuwepo kwa tume hiyo akisema kuwa walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za jeshi hilo.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye alikiri kuwepo kwa tume hiyo, lakini akasema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya kukamilisha wajibu wake.
“Hili suala lipo mahakamani kwanza, na kuhusu kuhojiwa au kutokuhojiwa kwa Dk. Ulimboka hilo lipo kwa mkubwa wangu, sasa unataka mimi niseme kama amehojiwa au la wakati sijui kinachoendelea huko?” alisema Kova.
Lakini Senso aliliambia Tanzania Daima kuwa, hakukuwepo na tume hiyo na kwamba walioteuliwa ni polisi ambao walifanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za jeshi hilo.
Alisema Jeshi la Polisi lisingeweza kuunda tume katika suala zima la Dk. Ulimboka kwa kuwa kilichotokea ni uhalifu kama uhalifu mwingine, na litashughulikiwa kwa mujibu wa jeshi hilo.
“Kwanza hilo ni suala la mwaka jana na sisi ripoti za mwaka huo tumeshafunga, labda nianze kufuatilia sasa hivi kujua limefikia wapi,” alisema Senso.
Alipoulizwa wao kama Jamhuri wanaendeshaje kesi hiyo ikiwa shahidi wa kwanza, Dk. Ulimboka hajachukua maelezo yake, Senso alisema kuwa daktari huyo anaweza kupeleka malalamiko yake kwao ili waweze kuyafanyia kazi.
Aliongeza kuwa, wakati polisi wakiendelea na uchunguzi, mlalamikaji anaweza kwenda kwao kutoa taarifa anazozijua kwa ajili ya kusaidia uchunguzi huo.
Alipotakiwa kuelezea kama walishawahi kumfuatilia Ramadhan Ighondu (Abeid) aliyetajwa na Dk. Ulimboka kuhusika na utekwaji wake, Senso alisema akiwa kama msemaji wa jeshi ana mipaka ya kuzungumzia suala hilo kwa ajili ya kutokuingilia kesi iliyopo mahakamani.
“Hatuwezi kila jambo tukawa tunalitangaza hadharani kuwa tumefanya hivi, tumefanya hivi, na mkumbuke ninyi ni waandishi wa habari peke yake, lakini mimi ni mwanahabari na askari vile vile,” alitamba.
Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk. Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi wenyewe.
Katika tamko lake mwishoni mwa mwaka jana lililosomwa kwa niaba yake na wakili wa kujitegemea, Nanyooro Kicheere, akimwakilisha mwanasheria wake, Dk. Ulimboka, alisema wapo watu ambao hawatapenda kusikia siri iliyojificha katika tukio zima la kutekwa kwake na kwamba hana jinsi zaidi ya kueleza ukweli.
Alisema kuwa tukio la kutekwa kwake, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, lilitokea wakati akiwa kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake ni ofisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu.
Aidha, Dk. Ulimboka alisema hata namba za simu zilizokuja kutambulika baadae kuwa zilikuwa zikitumiwa na Ighondu ndizo hizo alizokuwa akitumia mtu aliyejifahamisha kwa jina la Abeid kutoka Ikulu.
Alisema anamfahamu Abeid (Ighondu) na kwamba hata akikamatwa atakwenda kufanya utambuzi, na kwamba anasikitishwa hadi wakati huo wa kutoa taarifa yake kuwa mtu huyo hajakamatwa, wala hakuna kinachoendelea juu yake.

No comments:

Post a Comment