Friday, 4 January 2013

Mahabusu wakesha juu ya paa


KATIKA hali isiyo ya kawaida baadhi ya mahabusu katika Gereza la Keko jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana walikesha juu ya paa la jengo hilo wakinyeshewa mvua ikiwa ni shinikizo la kutaka kesi zao zipangiwe tarehe za kusiklizwa haraka.
Chanzo chetu cha habari kutoka gerezani humo, kilieleza kuwa mahabusu hao walianza mgomo huo tangu juzi mchana na kuendelea hadi jana bila kujali mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha huku wakitishia kujiua endapo hawatasikilizwa.
Kwamba walifikia hatua hiyo ili kuonesha kuwa wamechoshwa na vitendo vya uonevu wanavyotendewa na uongozi wa gereza hilo kwa muda mrefu kwa kesi zao kutopangiwa tarehe za kusikilizwa haraka kama watuhumiwa wengine.
Habari za ndani zinadai kuwa mahabusu hao, walionekakana kumtupia lawama Mkuu wa gereza hilo kwa kushindwa kusikiliza shida zao kila walipomweleza kilio chao hicho.
“Hali ni ya hatari kwani mvua yote imewanyeshea usiku kucha, Bwana jela hawasikilizi shida zao na hivyo walikuwa wanatishia kujiua,” kilisema chanzo chetu.
Alipoulizwa msemaji wa Jeshi hilo la Magereza, Omar Mtiga, kuhusu kitendo hicho, alisema hizo ni taarifa za kawaida katika gereza na wananchi hawapashwi kushtuka.
Mtiga alisema kuwa suala kupangiwa tarehe za kusikilizwa kesi za mahabusu si la Magereza bali kazi hiyo inafanywa na Mahakimu, kwamba kitendo cha kuushinikiza utawala wa magereza si sahihi.
“Kazi kubwa ya Magereza ni kuwalinda mahabusu na wafungwa wasitoroke pindi wa wapo gerezani. Sasa kama mahabusu amepanda juu ya paa, mti, kugoma kula na wakati mwingine hata kujipaka kinyesi kwa lengo la kuonyesha malalamiko yake ni sawa tu, utawala utamuacha hivyo ili mradi anafanya hayo akiwa ndani ya gereza,”alisema.
Mtiga aliongeza kuwa mahabusu wanayo haki ya kuandika barua ya malalamiko ili kutekelezewa kile wanachokihitaji.
Hata hivyo, alisema hakuona haja ya kujua ukweli wa tukio hilo kutokana kwamba hayo ni matukio yakawaida, ambapo pia yamekuwa yakimalizwa na utawala wenyewe wa gereza husika.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment