Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21), anayetuhumiwa kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, ameiomba mahakama impeleke Balozi wa Kenya mahakamani bila kufafanua.
Aliomba suala hilo jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Agnes Mchome, baada ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Awali, Mulundi alihoji sababu za upelelezi wa kesi hiyo kuchelewa kukamilika na pia sababu za upande wa mashtaka kutopeleka mashahidi mahakamani ili kesi hiyo iishe.
Pia alidai kuwa ameanza kugoma na mgomo wake unaendelea, hivyo, akasisitiza kuiomba mahakama impeleke balozi huyo mahakamani.
Hata hivyo, Hakimu Mchome alisema suala la kumpeleka balozi huyo mahakamani, liko nje ya mahakama hiyo, kwa sababu haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kwamba, yenye uwezo huo ni Mahakama Kuu.
Pia alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kumshinikiza balozi kufika mahakamani, badala yake kuna taratibu, ambazo mtuhumiwa anatakiwa kuzifuata, ikiwamo kumuandikia balozi wake barua.
Hata hivyo, maelezo hayo ya Hakimu Mchome hayakumridhisha Mulundi, hivyo akaomba kwenda kuonana na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, IIvin Mgeta.
Mtuhumiwa huyo aliruhusiwa kwenda kuonana na Mgeta, ambaye alimweleza kuwa upelelezi wa kesi yake unacheleweshwa.
Hata hivyo, Mgeta alimjibu kwa kumweleza kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuliamuru Jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi kwa sababu kesi hiyo iko chini ya jeshi hilo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 23, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa tena.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka.
Katika kesi hiyo, Mulundi anadaiwa kuwa Juni 26, mwaka jana, akiwa eneo la Leaders Club, jijini Dar es Salaam, alimteka Dk. Ulimboka.
Katika shtaka la pili, anadaiwa katika tarehe hiyo hiyo, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande, eneo la Tegeta, jijini humo, kinyume cha sheria, alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Julai 13, mwaka jana.
Chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment