Wednesday, 6 February 2013

Kova afafanua sakata la wizi wa mil. 150/-


KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ametamba kuwa hawezi kuruhusu wala kumwonea aibu askari yeyote ambaye atabainika kuhusika katika sakata la wizi wa sh milioni 150 zilizopotea mikononi mwa askari waliokuwa wakizima tukio la ujambazi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam Desemba 14 mwaka jana.
Kova alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Tanzania Daima kuripoti uwepo wa mkorogano ndani ya jeshi hilo katika sakata zima la kuwachukulia hatua watuhumiwa.
Akizungumza kwa simu, Kova alisema kuwa yako mambo mawili yanafanyika kwa wakati mmoja sasa katika kutafuta ukweli wa tukio zima.
Alifafanua kuwa baada ya upelelezi kukamilika, jalada la tuhuma limepelekwa kwa wakili wa serikali wa kanda hiyo ili kupitia na kujiridhisha kama watuhumiwa walihusika ama la.
Kamanda Kova alisema kuwa walichelewa kidogo katika hatua ya upelelezi kutokana na baadhi ya mashahidi akiwemo mwenye mali aliyeibiwa kuwa nje ya nchi.
“Mwenye mali kwa bahati mbaya aliondoka kwenda nje ya nchi baada ya tukio lile, hivyo tukachelewa kidogo wakati wa upelelezi, lakini tayari amerudi na tumemhoji, hivyo mwanasheria akikamilisha kazi yake watakaobainika watatajwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria,” alisema.
Kova aliongeza kuwa wakati hatua hiyo ikiendelea, vile vile taratibu za kijeshi nazo zinaendelea kwa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa hao watano ili nao wajitetee kisha watakaobainika watavuliwa uaskari na kushtakiwa katika mahakama za kiraia.
Kwa kujiamini, Kova aliapa kuwa hakuna usiri wowote katika sakata hilo na kwamba yeye kama kamanda hawezi kuruhusu wala kumonea aibu askari anayevunja sheria za kijeshi.
Ni hivi karibuni Kamanda Kova alidai kuwa jeshi hilo linawashikilia askari watano wote wakiwa wanaume ambao wanatuhumiwa katika ukwapuaji wa fuko hilo la fedha walizotakiwa kuziokoa kwa majambazi.
Alisema dalili za awali zinaonesha kuwepo kwa hali ya ushiriki wa askari watano katika upotevu wa fedha hizo na kwamba askari hao wanashikiliwa huku uchunguzi zaidi ukifanyika.
Aliongeza kuwa askari wanaoshikiliwa ni stafu sajenti mmoja na wengine wanne ni makoplo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment