TUKIO la kutekwa na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda linatarajia kuteka mjadala wa Bunge leo.
Jambo hilo linatarajiwa wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2013/2014 itakayowasilishwa bungeni leo.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa Machi 6 mwaka huu, nyumbani kwake Mbezi Juu jijini Dar es Salaam.
Mhariri huyo akiwa getini kwake akisubiri kufunguliwa, akapigwa kwa nondo kichwani, kutobolewa jicho la kushoto, kukatwa kidole, kung’olewa kucha na meno mawili.
Hata hivyo, pamoja na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuunda kikosi kazi cha wataalamu kwa kushirikiana na maofisa wengine wa makao makuu ili kuchunguza tukio hilo, hadi sasa hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa.
Kwa mijibu wa vyanzo vyetu mbalimbali, baadhi ya wabunge hawaridhishwi na jinsi uchunguzi huo unavyofanyika kiasi cha kuongeza hofu kuwa watuhumiwa wanalindwa kwa maslahi ya watu fulani.
Kambi rasmi ya upinzani kupitia kwa msemaji wake mkuu kwa wizara hiyo, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, imejipanga kulizungumzia sakata hilo kwa undani katika maoni yao ikiwa ni pamoja na kuhoji baadhi ya mambo yanayoonesha mizengwe katika uchunguzi huo.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa wapinzani wataibana serikali ieleze ni kwanini matukio hayo pamoja na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, mazingira yake yanafanana lakini Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vimekuwa vikilegalega.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment