Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, amekerwa na tabia ya baadhi ya wananchi mkoani hapa kutokutumia vyoo na badala yake wanajisaidia holela na kuchafua mazingira.
Amesema mkoa huu ni miongoni mwa mikoa ambayo bado iko nyuma katika matumizi ya vyoo.
Amesema uchafuzi unaofanywa wa kujisaidia hovyo unaharatisha afya za watu kwa kuambukizwa maradhi ya milipuko.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi ya viongozi wa mkoa kuhusu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira ya miaka minne ambayo inafanywa mashuleni na kwenye kaya.
Alisema lengo la kitaifa linaitaka mikoa iwe na matumizi ya vyoo katika mashule na kaya na kwamba mkoa huo unafanya uhamasishaji wa kutekeleza malengo hayo kutoka asilimia 12 hadi kufikia asilimia 53 ifikapo mwaka 2015.
Alisema iwapo lengo hilo litafanikiwa, mkoa utapunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kujisaidia holela katika maeneo ya makazi.
Mulungo alisema kampeni hiyo iliyozinduliwa Juni 5 mwaka jana na Rais Kikwete, inahusisha mikoa 12 na halmashauri 42 zikiwemo nne za Longido, Ngorongoro, Karatu na Meru za mkoani hapa.
Alisema kaya nyingi mkoani hapa hazina vyoo hali inayochangiwa na mila na desturi ambazo haziruhusu wanaume kujisaidia ndani ya vyoo.
Alisema katika kukabialiana na tatizo hilo, wamejipanga kutumia viongozi wa mila kama mbinu za ushirikishaji ili kuhamasisha uchimbaji na ujenzi na matumizi ya vyoo.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment