Friday 24 May 2013

Majambazi yatikisa Dar

WATU wanaoaminika kuwa ni majambazi ambao idadi yao haijafahamika, wamepora sh milioni 46, huku polisi wakishuhudia bila kutoa upinzani kukabiliana nao.
Fedha zilizoporwa ni mali ya mfanyabiashara wa bia za jumla jijini Dar es Salaam, Ivon Urio, wa wilayani Temeke.
Wakati majambazi wa Temeke wakipora kiasi hicho bila upinzani, tukio lingine la ujambazi limetokea jana asubuhi katika mtaa wa Sayansi na Kijitonyama wilayani Kinondoni ambapo walipora sh milioni 40, majira ya saa nne asubuhi.
Katika tukio la ujambazi la Temeke ambalo linadaiwa kuwa la nane kwa mwezi huu, lilitokea juzi kati ya saa nne na tano asubuhi katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, wakati mfanyabiashara huyo akijiandaa kupeleka fedha hizo benki.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo kabla ya majambazi hao kupora fedha hizo, polisi wanaokadiriwa kufikia 10, walifika eneo hilo wakiwa wanalifuatilia gari lililokuwa linashusha mafuta ya kula katika moja ya maduka yaliyo jirani na eneo palipotokea wizi huo.

Mmoja wa mashuhuda hao, Humphrey Mwakalinga, aliiambia Tanzania Daima kuwa walianza kutilia shaka mienendo ya baadhi ya watu katika eneo hilo na kupeana taarifa ya kuchukua tahadhari.
Humphrey alisema wakati wanahimizana kuchukua tahadhari hiyo, walimuona mmoja wa watu waliowatilia shaka akizungumza kwa simu na muda huohuo gari la mfanyabiashara huyo wa bia likavamiwa.
“Kulikuwa na askari wapatao 10 ambao walikuwa wamekuja kwa ajili ya gari lililokuwa linashusha mafuta, tukawaambia waangalie watu wanapora na muda huo ndio tukio linatokea lakini hawakufanya lolote; walikuwa kama hawaoni tukio hilo,” alisema Mwakalinga.
Alisema hata baada ya majambazi hao kuondoka kwa pikipiki, walibaki majambazi wengine wakiwa na bastola na raia wakawa wanawaambia askari wakawadhibiti pasipo askari hao kuitikia wito huo wa raia.
“Kama kwenye tukio la mafuta waliweza kuja kwa wingi halafu ujambazi unatokea mbele yao na hawafanyi jitihada kudhibiti, sisi wananchi lazima tuwatilie mashaka polisi,” alisema raia mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke Englibert Kiondo alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kutokea huku akikanusha askari kuwa karibu na tukio hilo.
Alipoelezwa sehemu waliyokuwa askari na tukio lilipotokea kuwa halizidi mita 20, Kiondo alisema askari hawakuwa katika maandalizi ya kupambana na majambazi.
“Muhimu ni kwamba kwa sasa tunawashikilia majambazi wawili na silaha moja huku tukiendelea kuwatafuta wale waliokimbia na fedha; hili la kuniambia askari walikuwa eneo la tukio bila msaada ni kwa sababu hawakuwa na maandalizi ya kupambana na majambazi wakati huo, walikuwa pale kwa kazi nyingine,” alisema Kiondo.
Tukio la ujambazi la eneo la Kijitonyama, wilayani Kinondoni, lilitokea jana, baada ya majambazi hayo kumfyatulia risasi dereva wa gari aliyekuwa akisubiri taa za barabarani ziruhusu.
“Majambazi hayo yalikuwa kama manne hivi, yalikuwa yamepanda pikipiki mbili tofauti, ghafla yakasimama na kulizunguka gari aina Vitz lenye usajili wa namba T929 CCX kwa haraka, mmoja wao akiwa na ‘mashine gun’ na wengine bastola,” alieleza shuhuda huyo.
Shuhuda huyo alieleza kuwa watu hao walifyatua risasi hewani na kumtaka dereva asimame na ashushe vioo vya gari yake, lakini alikaidi ndipo wakalifyatulia risasi kadhaa gari hilo upande wa dereva na kumjeruhi begani dereva huyo.
Baada ya shambulizi hilo, majambazi hayo yaliondoka na begi linalosadikiwa kuwa lilikuwa na sh milioni 40.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliahidi kulizungumzia zaidi tukio hilo leo.

No comments:

Post a Comment