TUKIO la wasichana wawili wa Tanzania waliokamatwa na dawa za kulevya Afrika Kusini, limechukua sura mpya baada ya kujulikana kwamba, siku ambayo watuhumiwa hao walisafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, mbwa wanaohakiki usalama wa mizigo hawakuwapo. Chanzo chetu cha habari kiliiambia MTAZANIA, kwamba pamoja na uwepo wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya uwanjani hapo, kitengo hicho kina kasoro kadhaa zinazotakiwa kurekebishwa
“Mimi niko hapa, najua kila kinachoendelea, nakwambia siku hiyo ambayo wale wasichana walipitisha dawa hizo, hapakuwa na mbwa wa kunusa, naamini kama mbwa wangekuwapo, lazima siri ingefichuka,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, katika viwanja vya ndege kuna vitengo vingi vikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na askari polisi ambapo kila kitengo kina majukumu yake.
“Kwa hiyo, ninachotaka kukwambia ni kwamba, jukumu la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambayo baadhi ya watu wanasema inachangia kupitisha dawa za kulevya, haihusiki kwa sababu jukumu lakekuu ni kuzuia vitu vinavyohatarisha usalama wa ndege na abiria.“Kuhusu uzito wa mizigo na malipo, hilo linafanywa na shirika la ndege husika na baada ya shughuli zote kufanyika, mizigo hukaguliwa kwa mashine na kunuswa na mbwa kabla ya safari kuanza,” kilisema chanzo hicho.
Pamoja na hayo, utata mwingine juu ya hali ya usalama na uwajibikaji wa watumishi wa uwanja huo wa ndege umejionyesha kupitia nyaraka zilizopatikana.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa siku kadhaa sasa, umebaini dawa hizo kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8 zilizokamatwa na wasichana hao, zilimhusisha pia mshirika wao kibiashara aliyefahamika kwa jina la Mangunga ambaye majina yake matatu tunayo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wasichana hao, Agness Gerald (25) na Melisa Edward (24) walisafiri ndege moja na Mangunga wakitoka Dar es Salaam kwenda Afrika Kusini.
Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba, wakati Manguga na wasichana hao wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), namba SA 189, Julai 5 mwaka huu, walikuwa na mabegi tisa.
Nyaraka hizo zinaonyesha jina la Agness Gerald, kwamba ndiye aliyelipia mabegi hayo, lakini katika sehemu inayotakiwa kuandikwa barua pepe, imeandikwa barua pepe ya Mangunga inayosomeka, Nmangunga@Gmail.com.
Mabegi hayo, yalikuwa na kilo 150 za dawa za kulevya lakini kila mmoja alitakiwa kusafiri na kifurushi cha kilo 20 na hivyo kutakiwa kuwa na kilo 60 wote kwa pamoja.
Baada ya kila mmoja kuwa na kilo 20, zilibaki kilo 90 ambazo walizilipia Dola za Marekani 94 badala ya Dola 450.
Nyaraka zinaendelea kuonyesha kuwa, Mangunga, Agness na Merisa wakati wa safari yao walikaa kiti kimoja kilichokuwa na namba tofauti.
Agness alikaa kiti namba 23B, Mangunga alikaa kiti namba 23D na Melisa alikaa namba 23A.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman Suleiman, alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu taarifa hizo, alikataa kulizungumzia kwa undani na kusema hana majibu kwa kuwa suala hilo liko katika uchunguzi.
Agness na Melisa, walikamatwa Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya.
Wakati wanakamatwa, walikuwa na mabegi sita kati ya tisa waliyokuwa nayo wakati wanapanda ndege jijini Dar es Salaam.
Inasemekana mabegi matatu yaliondoka na Mangunga ambaye hadi sasa hajulikani alipo
No comments:
Post a Comment