Saturday 3 August 2013

Mgambo matatani kwa kukutwa na bomu, risasi

Askari mgambo wawili wa kijiji cha Kigadye mkoani Kigoma, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na bomu la kutupwa kwa mkono, risasi 10 za bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), magazine mbili na sare za askari wa wanyama pori.

Askari mgambo hao ni Charles Kigye (45) na Ramadhani Omari (40).

Watuhumiwa hao walikamatwa Julai 25, mwaka huu saa 3:00 usiku katika kijiji cha Kigadye Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na taarifa kutoka kwa raia wema kuwa mmoja wa askari mgambo hao, alikuwa ameficha bomu kichakani karibu na nyumba yake.

Kamanda Kashai alisema baada ya taarifa hiyo, askari wake walikwenda hadi eneo la tukio na kufanikiwa kupata bomu moja la kutupwa kwa mkono, risasi 10 za SMG, magazine mbili na jozi tatu za sare za askari wa wanyamapori.


Hata hivyo, alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kutoroka baada ya kupata taarifa kuwa polisi wanamtafuta lakini Julai 27, mwaka huu watuhumiwa wote wawili walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi Kasulu.

Alisema walipopekuliwa nyumbani kwao, walikutwa na silaha, risasi na sare hizo.

Alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment