Saturday, 3 August 2013

Sintah akubali ameteleza, umaarufu haurudi kwa kupigana


INASIKITISHA sana kuona wanawake wenzetu wanatangaziana bifu hadharani tena ya kutaga kupigana huku wakijua wazi kuwa ni kinyume cha sheria na maadili ya mwanamke wa Kitanzania.
Watu hawa naweza kusema kuwa wamelewa na umaarufu waliokuwa nao zamani na kutokana na kuchuja wanaona njia sahihi ni ya kutangaziana ugomvi usiokuwa na kichwa wala miguu huku wakidhani kwamba ni jambo ambalo linaifurahisha jamii.
Hawa si wengine ninaowazungumzia bali ni Christina Manongi ‘Sintah’, mtangazaji wa kipindi cha Harusini, kinachorushwa na kituo cha DTV na Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye ni muigizaji wa filamu na mwanamuziki wa miondoko ya mduara.
Kwa wale ambao hamkubahatika kufuatilia ugomvi huu labda niwakumbushe kwamba malumbano yalianza pale Shilole aliporejea hivi karibuni akitoka Marekani katika ziara yake ya kimuziki.
Mwanadada huyo aliporudi alisema amejifunza mambo mengi wakati akiwa huko na lengo lakeni siku moja kuja kuimba na mwanamuziki mkubwa wa nchini humo Jenifer Lopez ‘J. Lo’.
Baada ya maneno hayo, Sintah alitoa mawazo yake kwenye mtandao wake maneno ambayo kwa wenye kufikiria mbali kama mimi yalikuwa sio ya kistaarabu na kwani yalikuwa ya kumkatisha Shilole tamaa. Kipande hiki ni baadhi ya maneno ‘aliyotupia’ baada ya watu kukerwa na kauli yake hiyo.
“Mtu anayekupenda lazima akwambie ukweli, ukweli humfanya mtu kuwa huru; sasa sielewi kwa nini sie Watanzania hatupendi kukosolewa isipokuwa tunapenda urahisi wa maisha vitu vitokee tu pap. Ndiyo maana mabinti wanaamua kubeba dawa za kulevya n.k. TUSIPENDE KURAHISISHA MAISHA!!!!

“Kichekesho cha mwaka ni pale mtu hana hata albamu, nyimbo mbili/tatu tu za mdumange anakuja kutuambia eti Jenifer Lopez kafurahi anataka kufanya naye nyimbo kiruuuuuu. Umaarufu wako huanzia nyumbani, hujawagusa hata kina Lady Jaydee sogeasogea mpaka kwa kina Wahu na Juliana Kanyomozi kwanza ndo angalau uje utudanganye Lolest. Kuna tofauti gani sasa kati ya huyu na wale waliotuambia tutaenda Brazil 2014?????
“Tukijipanga timu yetu ya taifa itashiriki Kombe la Dunia. Inawezekana tu! Msanii ukijipanga hakuna kinachoshindikana, nini JLO unaweza fanya ‘featuring’ hata na Jay Z lakini sio kutuletea mambo ya mfalme njozi kwa kuwa umepata mdhamini kakusafirisha basi mburula mwanzo mwisho.
“Kuona ng’ambo ukubwani linaelekea kuwa janga la kitaifa sasa....Usiwachukie wanaokupinga; unaweza kujifunza mengi toka kwao!
“Imenibidi kusema hivyo kwa kuwa nasumbuliwa sana na vyombo vya habari kila mara simu na mahojiano; Shilole hana kitu cha ajabu cha kunifanya nikamchukia... kila mara mimi ni mpenda ukweli. Nasubiri kupigwa sasa kama alivyoahidi Lolest.
“Kwa wale mliokuwa na mtazamo kama mie; sio wanafiki, Mungu anapenda sana wasema ukweli.
“Sitaki tena vyombo vya habari vya aina yoyote ile sasa viniulize hili swala; habari ndiyo hiyo. Huu ndio ukweli wangu na sipendi kupigiwa simu kwa sababu sitaki kumpa mtu ‘heshima’ ya kumtajataja, nina mambo mengi muhimu zaidi ya kufanya kuliko kujadili mambo ambayo hayana kichwa wala miguu,…...!”
Kwa maneno hayo binafsi siungani hata kidogo na Sintah na badala yake nampongeza Shilole kwa malengo yake hayo kwani hakuna jambo linaloshindikana chini ya jua na kila kitu ni kujipanga na kuweka malengo, kwani nani aliyejua kama Ali Kiba siku moja angesimama jukwaa moja na kuimba na mwanamuziki Robert Kelly ‘R.Kelly’.
Watu kama kina Sintah naweza kuwalinganisha na wale wanaoanza kujinyanyapaa wenyewe kwamba hawawezi jambo fulani mpaka asaidiwe na mtu fulani bila kujua kinachotakiwa ni kuwekeza nguvu.
Sintah anapaswa kujiuliza kuwa kuna wasanii wangapi huko nyuma waliokuwa na majina makubwa lakini leo hii hawaingizi fedha kama wanavyoingiza wasanii walioibuka miaka mitatu ya nyuma na kupata mialiko mbalimbali.
Hivi ni kweli Sintah anataka kutuambia wakati ule jina lake likivuma katika uigizaji na kuhojiwa na vyombo mbalimbali hakuwahi kuelezea malengo yake ikiwemo ya kung’aa kimataifa au kwa kuwa jina lake kwa sasa limechuja basi anatafuta namna ya kurudisha umaarufu kwa kuanzisha ugomvi na wasanii wengine!?
Mbona alijiita J’Lo wa Bongo na hakuna aliyemkejeli pamoja na mpaka leo kujisifu kwamba Lopez ni dada yake wakati hana hata chembe ya udugu na yeye? Hii yote ni kwa sababu kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake na kueleza lile analojisikia ili mradi tu asivunje sheria.
Kumbuka kwamba kama binadamu huwezi kupendwa na kila mtu au kuchukiwa na kila mtu na kwa Shilole ndivyo hivyohivyo kwani wakati Sintah anamponda, wako mashabiki wake waliokerwa na alichomfanyia mwenzake na kama yeye anaona hana analolifanya katika sanaa basi wako wanaomuona anafaa.
Kwa upande wa Shilole namshauri aachane na mpango wake wa kutaka kwenda kumpiga Sintah kwani hiyo sio njia sahihi ukizingatia hata sheria za nchi zinatueleza hivyo na kwa hili kama mwenzio akipata akili ya kwenda kukuchukulia RB polisi unaweza ukajikuta unaingia katika matatizo mengine.
Kuna usemi usemao dawa ya mjinga ni kumnyamazia, na Shilole ni vyema akafanya hivyo kwani matunda yake yatakapoonekana baadaye ndiyo itakuwa hukumu ya Sintah na pia akumbuke wasanii wamebeba jukumu kubwa la kuielimisha jamii kupitia kazi zao, sasa kama mtaanza kupigana tuwaeleweje na wasanii wanaochipukia watajifunza nini kwenu?
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment